WASIFU WA DK, BARNABAS MBOGO ANAYENUIA, UBUNGE NYAMAGANA

Dk Barnabas Mbogo
Dk Barnabas Mbogo

Wasifu na nia ya Dk Barnabas Mbogo kugombea Ubunge wa Nyamagana kupitia CCM.

Dk Barnabas Mbogo ni nani?


Mwenyeji wa Igogo Kaskazini, Wilaya ya Nyamagana, Mkoani Mwanza. Kijana wa pili wa Mzee Africanus Mbogo (RIP) na Bi Magreth Masanja. Alihitimu masomo yake katika shule ya Msingi Mlimani, Shule ya Sekondari Mwanza, Mazengo High School, Dodoma na alihitimu masomo ya Shahada ya Udaktari wa Afya ya Kinywa na Meno toka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam sehemu ya Muhimbili.

Ni nini uzoefu wake wa uongozi?


Wakati akiendelea na masomo yake ya Chuo Kikuu, alipata kufanya kazi ya kujitolea (Volunteer) katika Shirika la Tanzania Youth Alliance (TAYOA) lililopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam. Shirika hili linajihusisha na utoaji wa elimu ya Ukimwi kwa vijana, linajenga uwezo wa uongozi kwa vijana, vilevile linajihusisha na kuwapatia vijana elimu ya ujasiriamali. Kwa kuzingatia sifa na uwezo wake wa uongozi, Dk. Mbogo alipanda ngazi za uongozi kwa haraka na kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika hilo. Baada ya kuhitimu masomo ya Chuo Kikuu, Wizara ya Afya, Tanzania ilimpangia Dk. Mbogo kufanya kazi katika Hospitali ya Manispaa ya Temeke. Huko alikuwa Mkuu wa Idara ya Afya ya Kinywa na Meno. Mwaka 2009 mwanzoni alipata fursa ya kufanya kazi katika Wizara ya Afya, Serikali ya Botswana. Huko aliendelea na kazi zake za utabibu wa afya ya kinywa na meno, uongozi na utawala bora mpaka mwaka huu wa 2015 alipoamua kurejesha nyumbani uzoefu aliopata kimataifa ili kuwatumikia Watanzania.

Agenda yake ya siasa ni nini?


Akiongea na mwandishi wetu, Dk Mbogo aliainisha masuala manne yanayomsukuma kutia nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Nyamagana. Masuala hayo ni pamoja na mosi, ombwe baina ya wananchi na viongozi ambapo viongozi wengi hawawashiriki wananchi kwenye kufikia maamuzi kuhusu masuala yanayohusu wananchi. Mbaya zaidi, hata wanapowashirikisha maamuzi ya Wananchi hayatiliwi uzito unaostahili. Pili kudorora kwa elimu ambapo wahitimu wengi kutoka ngazi mbali za elimu hawana uwezo wa kutosha kuchanganua masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ili kubaini uzuri na ubaya wake. Tatu, kuendelea kuzorota kwa hali ya afya miongoni wa Watanzania hata baada ya kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya Afya. Nne, hifadhi ya jamii hususani suala la ukosefu wa ajira kwa vijana na sintofahamu ya maisha ya uzeeni.

Aliongeza kwamba, masuala haya yanaendelea kuliumiza taifa kwa vile viongozi wetu wengi wa kuchaguliwa hawana falsafa za kisayansi zinazoongoza kazi zao za uongozi na utawala bora. Hivyo anakusudia kutumia falsafa yake ya uongozi yenye nguzo tatu ambazo ni utafiti, kujenga uwezo na uchechemzi (Advocacy). 



Ni lini ameanza kujihusisha na masuala ya siasa?

“Nimekuwa ni muumini wa masuala ya siasa kwa muda mrefu sana, rasmi nilianza kuzama kwenye siasa mwaka 1992 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nyumbani. Nakumbuka mwaka 1995, wakati nipo Mazengo High School, Dodoma, tulikuwa na Mwalimu Chitinde alikuwa akifundisha somo la Kemia. Wakati huo chama cha NCCR-Mageuzi kikiongozwa na Mhe. Augustino Mrema na akina Wakili Mabere Marando na Masumbuko Lamwai ndio kilikuwa kikiongoza siasa za upinzani hapa nchini. Mwaka huo (1995) Mwalimu Chitinde aligombea Ubunge kupitia NCCR-Mageuzi kwenye Jimbo la Bahi, Dodoma. Kwenye uchaguzi ule Mwalimu wetu hakupata kura za kutosha kuwa mbunge”. 
Alitoa kumbukizi na kuongeza kwamba 
“pia nimeshuhudia namna NCCR-Mageuzi ilivyohama toka kuwa chama cha upinzani chenye nguvu nafasi na kuwa chama cha kawaida huku nafasi ya chama kikuu cha upinzani ikihamia kwa CUF. Hivi karibuni nafasi hiyo ya Chama Kikuu cha upinzani imechukuliwa na CHADEMA”. 
Hivyo basi, nimeanza kujihusisha na siasa kwa takribani miongo miwili sasa, alihitimisha.

Kwa nini anatia nia mwaka huu?

Suala la uongozi unaohitaji kuombe ridhaa ya wananchi ili wakupitishe kuwa kiongozi wao kupitia sanduku la kura linahitaji kujitafiti binafsi kabla hujaweka nia yako hadharani. Nimekuwa nikijitafiti kwa miaka mingi kuona kama ninatosha kuwa nyenzo ya kuwatumikia wananchi. Baada ya kupata fursa mbalimbali za kufanya kazi na makundi mbali ya jamii kwenye ngazi ya kitaifa na kimataifa, naamini ninatosha kuwa nyenzo ya kutumikia wananchi. Ninaamini huu ni wakati muafaka kujitolea kuutumikia umma ili tushirikiane kujibu masuala ya msingi yanayoiumiza jamii yetu. 
Alisema.

Dk Barnabas Mbogo
Dk Barnabas Mbogo

Kwa nini kupitia CCM?


Dk Mbogo alisema kwamba 
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chombo cha kisiasa chenye dhamira ya kuboresha maisha ya Watanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii. CCM inazo sura mbili kama ilivyo sarafu. Kwa wanaotazama upande mmoja tu wa sarafu wanaona kwamba CCM haijafanya lolote lenye manufaa kwa ustawi wa nchi yetu. Hawa siwalaumu. Bali nawatia nguvu watazame pia upande wa pili wa sarafu”

Aliongeza kuwa yeye ametazama pande zote mbili za sarafu hii (CCM) na kuona kwamba kwa kiasi fulani wanaolalamika wanazo hoja za msingi kuhusu CCM kuchelewesha maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo alisema kwamba sehemu ya majibu kuhusu kuchelewa huku kwa CCM yanapatikana kwenye upande wa mazuri ya sarafu hii (CCM). Alinukuliwa akisema 
“kimsingi CCM imeendelea kudhihirisha ubora wake wa kimuundo, kiutawala na kiuwajibika. Ni CCM pekee inayoonesha kuvumilia tofauti za fikra sio tu miongoni mwa wanachama wake, bali pia miongoni mwa makundi ya Watanzania. Wanaoibeza wanasahau kwamba ni CCM ndio imetoa “model” ya muundo wa vyama vingine vya siasa hapa nchini. Hata hivyo ili demokrasia iendelee kukua na kustawi hapa nchini, hatuna budi kuwa na wakosoaji wa CCM”. 
Vile vile alisisitiza kwamba ili hoja za wakosoaji zibebe mantiki yenye uzito unaostahili, ni budi wakosoaji hawa wakatazama pande zote mbili za sarafu hii.

Alihitimisha kwa kuainisha kuwa ameona ni vema kusimama na kuomba fursa ya kugombea ubunge wa jimbo la Nyamagana kupitia CCM kwa vile amezingatia ubora wa muundo, utawala bora na uwajibikaji wa CCM ikiwa ni pamoja na mapungufu yake. Anaamini kuwa fikra mpya na chanya ndizo zitaboresha Chama Cha Mapinduzi.

Ikiwa utapata ridhaa ya chama na hatimaye kushinda nafasi ya Ubunge, utafanyaje kufikia malengo yako?

Kwa maoni yangu, nafikiri ni mapema sana kuzungumzia kushinda nafasi ya ubunge wa Nyamagana. Maana bado kuna michakato mingi ndani ya chama, pia sio kazi rahisi kumshinda mbunge aliyepo madarakani Mhe. Wenje. Hata hivyo, kama alivyopata kusema Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara Mhe. Pius Msekwa kwamba “ushindi wa uchaguzi hauji kama mvua, bali hufanyiwa kazi”, ninaamini kwamba mimi binafsi kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Nyamagana tunafanyia kazi ushindi dhidi ya vyama pinzani.

Uongozi wa kushirikishana baina ya Wananchi na Viongozi wao ndio silaha kubwa itakayofanikisha kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakazi wa Nyamagana na Tanzania kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA