TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inapenda kutoa taarifa kuwa hadi jana tarehe 03 Mei, 2015 raia wa Burundi waliongia nchini kuomba hifadhi walikuwa 1,852. Raia hawa wa Burundi waliingia nchini kupitia vijiji mbalimbali vya mkoa wa Kigoma. Vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Kigaye, Sekeoya na Kakonko. Vingine ni Kosovo, Kagunga na Kibuye, huku wengine wakiwa wamepitia katika Kituo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mkoani Kigoma.

Baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina katika kituo maalumu kilichopo mjini Kigoma, 1,252 kati yao wamehamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na mahojiano yanaendelea kwa waliobaki na wanaoendelea kuwasili.

Shughuli ya kuwahoji na kuwahamishia katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu inafanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), pamoja na wadau wengine.

Aidha Serikali za vijiji zinasaidia kuwapokea na baada ya kufanyiwa ukaguzi, hatimaye wanasafirishwa hadi mjini Kigoma.

Pamoja na ujio wa raia hawa wa Burundi, hali ya ulinzi na usalama katika maeneo wanapoingilia ni shwari na hadi sasa hakuna matukio yoyote ya uhalifu yalitolewa taarifa. Vyombo vya ulinzi na usalama vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vilivyopo katika maeneo hayo vinaendelea na kazi zake kama kawaida.

Hata hivyo raia wanaoishi katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi mkoani Kigoma wametakiwa kutoa taarifa kwa Serikali za Vijiji vyao kuhusu wageni wanaofika katika maeneo yao, badala ya kuwahifadhi kiholela majumbani mwao, na kuwa watakaobainika kukiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.

Raia hawa wa Burundi ambao wamekuwa wakiingia nchini wakiwa katika vikundi vidogovidogo wataendelea kupokelewa kufuatana na taratibu na sheria zinazotawala upokeaji wa waomba hifadhi.

Imetolewa na:
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

04 MEI, 2015

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA