AINA MPYA YA UTAPELI TANDO - Barua yenye mhuri, tarehe na saini!


Kadiri siku zinavyosonga, ndivyo na watu wanavyotumia
intaneti na kadiri ya matumizi ya intaneti yanavyoongezeka ndivyo na vitendo vya kidanganyifu na wizi wa mitandaoni vinavyoongezeka.

Kujifunza kung'amua mbinu wanazozitumia matapeli katika kufanikisha malengo yao ndicho kiokozi muhimu katika kujilinda wewe binafsi na wale unaowajali dhidi ya upotevu wa fedha na mali.

Kwa bahati mbaya, matapeli kama ilivyo kawaida yao, hawakomi kujaribu kuvumbua mbinu mpya za kuiba pale wanapogundua kuwa watu wengi wameshazifahamu na kuzizoea mbinu zao.

Siku tatu zilizopita nimepokea ujumbe kama unavyosomeka kwenye picha inayoonekana hapo (bofya kuikuza ili kupata ukubwa unaosomeka kirahisi zaidi) na katika ujumbe huo, hakukuwa na maelezo zaidi ya 'respond to the subject matter'.

Nilifungua kiambatanisho hicho na kusoma maelezo hayo.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya haraka niliyotumia kung'amua kuwa ujumbe huu ni wa kitapeli.

1. Tarehe iliyopo katika mhuri ni 05.05.10, mbona bado hatujamaliza hata mwezi Aprili?
2. Kuulizia namba yangu binafsi? Ukishaona mtu anaulizia habari binafsi, kuwa makini.
3. Ati wametenga kiasi cha fedha na mikataba kwa kampuni yangu. Najiuliza, 'mbona sina kampuni?
4. Wanaahidi kulipa fedha mwanzoni. Hii inanipa wasiwasi, biashara ya kulipa kabla ya kutoa huduma?
5. Tishio kuwa nisipojibu ndani ya wiki mbili watafuta kampuni nyingine kwa ajili ya kazi hiyo. Najiuliza, Wiki mbili za kuanza kuhesabika tangu lini? Kwa kigezo kipi? Wana uhakika gani kuwa ninasoma barua pepe kila leo? Na kama wana-track kujua nimesoma lini barua pepe, kwa nini wanitishe?
6. Mwisho, ni jina la mmoja wa Wakuu wa nchini Nigeria walilolipachika cheo ambacho kinanipa walakini.

Niliishia kutupa ujumbe huo kapuni na kuwaasa wengine kuwa makini na aina hii mpya ya wizi.

TAHADHARI:
Tafadhali usiige tabia ya kufungua viambatanisho vyovyote navyotumiwa ikiwa huna usalama wa anti-virus katika kompyuta unayoitumia. Baadhi ya watu hufungua viambatanisho wasivyotarajia kupokea kwa kuwa wana tamaa ya kujua kilichomo ndani. Matokeo yake ni kufungulia virusi wanaoharibu tarakilishi taratibu au kuisababisha iwe 'misukule' (zombie) kwa ajili ya kutumika kutuma virusi kenye tarakilishi nyingine bila ya wao kufahamu. Mara nyingi viambatanisho (attachments) huwa ni vyanzo vya kusambaza virusi kwenye tarakilishi.

taarifa hii ni kwa hisani ya www.wavuti.com

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA