HabariLeo: Mizigo yapungua bandarini Dar tofauti na matarajio


source
WAKATI Mamlaka ya Bandari (TPA) ikithibitisha ufanisi katika upakuaji na uondoshaji mizigo na usalama wa mali katika Bandari ya Dar es Salaam, imebainika idadi ya mizigo katika bandari hiyo, imepungua tofauti na matarajio.

Akizungumza wakati akifunga warsha ya Wahariri wa Habari mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, alitoa mfano wa shehena ya magari yanayokwenda Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa Mhanga, shehena ya magari yanayokwenda katika nchi hiyo kutoka Januari 2015 mpaka Januari 2016, imepungua kwa asilimia 50 huku shehena ya Zambia ikipungua kwa asilimia 46. Beira Mhanga alisema walipochunguza sababu ya kupungua kwa shehena hizo, walibaini sehemu ya shehena hiyo hasa iliyokuwa ikienda Zambia, DRC na Malawi, inashushwa katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji.

Sababu za kushushwa katika Bandari ya Msumbiji, badala ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndiyo yenye unafuu wa umbali kutokana na jiografia yake, Mhanga alisema ni unafuu wa kusafirisha shehena hiyo kwa reli ya Beira mpaka Malawi, tofauti na ilivyo kwa barabara.

Alisema usafirishaji wa reli ni nafuu kwa asilimia 30, ikilinganishwa na usafirishaji wa barabara na kwa kuwa Msumbiji wameshakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa, wafanyabiashara wameona unafuu wa kupitisha mizigo katika Bandari ya Beira kuliko ya Dar es Salaam.

Athari hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam, huenda ikawa mbaya zaidi baada ya kukamilika kwa reli ya kisasa inayoanzia katika Bandari ya Mombasa mpaka DRC, kwa kuwa itaongeza unafuu wa usafirishaji wa mizigo katika bandari hiyo shindani kwa Tanzania.

Katika warsha hiyo, ilifafanuliwa kuwa dunia nzima bandari zimekuwa na mafanikio, kutokana na kuwa na mfumo wa reli za kisasa unaotoa mizigo bandarini na kufikisha kwa mteja, jambo linalokosekana katika Bandari ya Dar es Salaam.

Durban Shehena nyingine iliyokuwa ikipitia nchini, imebainika kupelekwa katika Bandari ya Durban nchini Afrika Kusini kutokana na unafuu uliotokana na matumizi ya fedha ya nchi hiyo, Rand, katika utozaji wa gharama za kutoa mizigo, tofauti na Tanzania ambako gharama hutozwa kwa Dola ya Marekani.

Akifafanua hali hiyo, Mhanga alisema kwa sasa Rand imeshuka thamani na hivyo mfanyabiashara mwenye Dola ya Marekani, atatumia Dola chache za Marekani kulipia tozo hizo kwa Rand ya Afrika Kusini iliyoporomoka thamani.

Kutokana na hali hiyo, ingawa gharama za utoaji mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Durban zinalingana, lakini mfanyabiashara akipitisha mzigo Afrika Kusini, atatakiwa kubadilisha Dola ili apate Rand ya kulipa gharama hizo; na kwa kuwa Rand imeporomoka thamani, atatumia Dola chache kuliko ilivyo kwa Tanzania.

Utambuzi wa mizigo Changamoto nyingine aliyotaja Mhanga ni ya mfumo wa kutambua shehena zilizoko katika meli, unaotumiwa kukadiria gharama za utoaji wa mizigo bandarini pamoja na kodi. Akifafanua, Mhanga alisema mzigo unapopakiwa katika nchi unakotoka, mpakiaji anapaswa kueleza aina ya mzigo katika fomu maalumu ya kutambulisha mzigo.

Fomu hiyo inayojazwa na mpakiaji, ikifika Dar es Salaam kabla ya kupakua mzigo, hutumiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kukadiria kodi. Hata hivyo Mhanga alisema fomu hiyo inapokosewa na mpakiaji, TRA wakati wa kuhakiki mzigo huhisi harufu ya ukwepaji kodi na hivyo utaratibu wa utoaji wa mzigo husika, huchukua muda kuliko kama fomu hiyo isingekosewa.

Mhanga alisema wakati utaratibu wa kurekebisha makosa hayo ya fomu ukichukua muda mrefu kabla ya kuruhusiwa na TRA, mzigo huo huchajiwa adhabu ya kukaa bandarini kwa muda mrefu na kama ni wa nje ya nchi, mteja hulazimika kukaa Dar es Salaam kwa kosa lililofanywa na mpakiaji wa mizigo.

Meneja huyo wa Bandari ya Dar es Salaam, alisema mteja huyo anaporuhusiwa na TRA kuchukua mzigo, wakati ameshaingia gharama ya kuishi Dar es Salaam kwa muda mrefu, akifika bandarini na kukutana na adhabu ya kuhifadhi mzigo ambayo hakuisababisha, wengi hukasirika na hajui wanapeleka ujumbe gani kwa wateja wengine katika nchi zao.

Ufanisi Pamoja na changamoto hizo, Mhanga alisema kama wadau wengine wakikamilisha taratibu za ukaguzi wa mzigo mapema, mzigo huchukua muda mfupi kupakuliwa katika meli na kuondolewa mapema bandarini, ili umfikie mteja katika muda mfupi zaidi.

Alitoa mfano wa mwaka 2011, ambapo mteja alitumia siku 4.7 kusubiri mzigo wake utoke bandarini, lakini leo mteja huyo huyo atasubiri siku 0.2 mpaka apate mzigo wake na hilo limesababishwa na uboreshaji wa utaratibu wa kupata vibali vya nyaraka, ambao kwa sasa unafanyika kwa mtandao.

Mhanga alisema bandari hiyo kwa sasa inakamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa 35, ambalo litakuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati, litakalohifadhi wadau wote wa bandari katika jengo moja, ili mteja akiingia katika jengo hilo, akitoka akatoe mzigo wake moja kwa moja.

Kwa sasa mteja anaweza kujikuta akihangaika na nyaraka zake kwa wadau mbalimbali wa Bandari ya Dar es Salaam kupata vibali, ikiwemo Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchikavu (Sumatra), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Idara ya Uhamiaji, Idara ya Afya, Mkemi Mkuu na wengine.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA