Taarifa ya Wizara kuhusu mambo ya kuzingatia katika kulitumia daraja la Kigamboni

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KUHUSU MATUMIZI YA DARAJA LA KIGAMBONI

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inapenda kutaarifu Umma kuwa Daraja la kigamboni litaanza kutumika siku ya Jumamosi tarehe 16, Aprili, 2016 kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Katika siku za mwanzo, magari yatapita bila kulipia tozo hadi Serikali itakapokamilisha taratibu na kutangaza utaratibu wa kulipia. Aidha, watembea kwa miguu na waendesha baiskeli watavuka bure katika Daraja la Kigamboni. Hata hivyo maguta na mikokoteni haitaruhusiwa kutumia daraja hilo kutokana na sababu za kiusalama.

Magari yatakayoruhusiwa kupita katika Daraja la Kigamboni katika siku hizo za mwanzo ni yale yenye uzito usiozidi tani 10, hatua ambayo itasaidia kufuatilia mwenendo wa upitaji wa magari katika daraja, barabara za juu (Interchange) katika eneo la Kurasini, pamoja na kuhakikisha kwamba magari yanayotoka au kuingia katika daraja hayasababishi msongamano wa magari katika Barabara ya Nelson Mandela, Barabara ya Kilwa na maeneo mengine ya jiji. Baada ya utaratibu kukamilika magari ya aina zote yenye uzito unaoruhusiwa kisheria yataruhusiwa kupita katika daraja.

Mambo muhimu ambayo madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatakiwa kuzingatia ni:-
  1. Kuzingatia sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kufuata mwendo kasi unaotakiwa ili kuepuka ajali na kuepuka uharibifu miundombinu ya daraja
  2. Kufuata alama za barabarani zilizowekwa katika ‘Interchange’ ya Kurasini ili kwenda kwenye uelekeo sahihi.
  3. Kuzingatia alama zilizowekwa kwenye milango (Toll Gates) ya Kituo cha kulipia tozo (Toll Plaza) ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ya kituo hicho.
  4. Madereva na watumiaji wa barabara wengine watakaosababisha uharibifu wa aina yeyote wa miundombinu ya daraja watatozwa faini au kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
  5. Kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa takataka katika eneo la daraja.
Aidha, Wizaraya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inawataka madereva wa magari ya mizigo wanaoegesha katika barabara ya Nelson Mandela wakisubiri kuingia bandarini watafute eneo stahiki la maegesho na kuyaondoa magari hayo kwani hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaoenda kinyume na agizo hili.

Msongamano wa magari hayo husababisha uharibifu wa barabara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara katika eneo hilo.

Imetolewa na;
Eng. Joseph M. Nyamhanga
Katibu Mkuu (Ujenzi)
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

14 Aprili, 2016

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA