RAIS WA KENYA UHURU KENYATTA AIZURU UJERUMANI

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimkaribisha rasmi Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta mjini Berlin ambapo Merkel alisisitiza haja ya kuimarsiha uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwa kuitaja Kenya kuwa ni mahala thabiti.
Rais Kenyatta amesema kuwa vita dhidi ya ugaidi ni suala linalolikumba bara la Afrika kwa jumla akigusia makundi ya waasi wenye itikadi kali katika nchi kama Nigeria na Mali na hata nchi yake Kenya ambako kumeshuhudiwa mashambulizi ya kigaidi.
Kenyatta amesema Umoja wa Afrika sharti ujiimarishe katika ukusanyaji wa taarifa za kijasusi na kuhimiza ushirikiano zaidi miongoni mwa nchi za Afrika ili kukabiliana na kitisho cha itikadi kali na ugaidi.
Hata hivyo Kenyatta amesema kitisho cha ugaidi sio tatizo barani Afrika pekee bali ni kitisho kwa ulimwengu mzima na hivyo jitihada za dunia nzima zinahitajika kupambana dhidi ya ugaidi.
Merkel aitaja Kenya mahali Thabiti
Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesifu juhudi za Kenya za kulinda amani katika nchi jirani ya Somalia ambako wanajeshi wa Kenya wanapambana dhidi ya waasi wa Al Shabab, kundi lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.
Ziara ya Kenyatta nchini Ujerumani inakuja huku nchi za Ulaya zikijaribu kufufua uhusiano na nchi za Afrika. Merkel amesisitiza haja ya kuwepo kwa uhusiano imara zaidi akisema kwa miaka kadhaa bara la Ulaya liliisahau Afrika.
Merkel amesema China ndiyo ilijaza pengo hilo lakini sasa wananuia kubadilisha hali ilivyo na kurejesha uhusiano kati ya Ulaya na Afrika.
Kansela huyo wa Ujerumani amesema Kenya na Ujerumani zinaweza kushirikiana kuhusu masuala mengi yakiwemo utalii, kupambana dhidi ya ugaidi, usalama, kupambana dhidi ya umaskini , kuwashajaisha vijana na kuhimiza utawala bora.
Ujerumani na Kenya zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi. Ujerumani ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Kenya kama taifa huru mnamo mwaka 1968 na Kenya ni mshirika mkubwa wa Ujerumani kibiashara barani Afrika.
Idadi kubwa ya watalii wanaoizuru Kenya kila mwaka hutokea Ujerumani na taifa hilo pia linapokea kiwango kikubwa cha misaada ya maendeleo kutoka Ujerumani.
Lakini ziara ya kiongozi huyo wa Kenya nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa jumla ilichukua muda tangu kuingia madarakani miaka mitatu iliyopita kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili katika mahakama ya uhalifu ya ICC.
Ulaya yanuia kuimarisha uhusiano na Kenya
Nchi nyingi za magharibi ziliupa utawala wa Kenyatta kisogo kutokana na yeye kukabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Hata hivyo mwaka jana mahakama hiyo ya ICC ilifutilia mbali kesi dhidi yake.
Rais Kenyatta alifanya mkutano pia na mabalozi wa nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Ujerumani ambako alizushukuru nchi za Afrika kwa kusimama na Kenya kuhusu suala la ICC.
Hii leo jioni, kiongozi huyo wa Kenya anatarajiwa kukutana na wakenya wanaoishi Ujerumani kabla ya kukamilisha ziara yake nchini humu hapo kesho

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA