IKIWA LEO NI SIKUKUU YA NANE NANE, MWL DENIS MPAGAZE ANASEMA "NENDA SHAMBANI UONE MZIKI WAKE"

Denis Mpagaze,

Ni takribani miongo mitano toka uhuru tunaendelea kuaminishwa kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Na katika hili uhamasishaji ulienea kwa kasi sana. 


Kwa wale waliopitia shule za msingi bila shaka waliimba shairi hili, “ Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali. Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili. Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali. Wakataka na kauli iwafae maishani. Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli. Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali. Roho naona yachinjwa, Kifo kimenikabili. Kama mnataka mali, mtayapata shambani”.

La kusikitisha kila aliyejaribu kilimo cha moto alikipata. Sahriti la kwanza ilikuwa ni kuchakaa, na shariti la pili ilikuwa ni kula msoto. Waulize wazee wetu walioishi kwa kutegemea kilimo uone wanavyokilaani. Ilifikia kipindi kilimo kikatumika kama ‘tusi’ kuwatukana watoto waliochukia shule. Nakumbuka wazazi wangu kila siku walikuwa wakitutishia, “atakayefeli darasa la saba ataishia kuwa mkulima”. Na kweli tulisoma kwa bidii ili kuepuka laana hiyo. “Chezea kilimo cha kufa na kupona weye??”


Leo hii sidhani kama kunashule inasisitiza watoto kuimba nyimbo za kilimo na hata kama wataimba basi wataimba kwa malengo ya kujibia mitihani na kusahau kila kitu baada ya mitihani. Siku moja nakutana na katoto kadarasa la tatu kamekazana kuimba, “nani kamwaga pombe yangu!!!!nauliza…ee…nauliza…Nani kamwaga pombe yangu”. Ni burudani inayomuandaa mtoto kuwa mlevi na si mkulima. Pengine ndiyo maana takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka jana zinaonyesha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye walevi wengi zaidi wa pombe ukilinganisha na nchi nyingine. Miongoni mwa nchi 55 za Afrika zilizo chini ya uangalizi wa WHO, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanywaji wengi zaidi wa pombe baada ya Nigeria na Uganda.


Jaribu kilimo uone mziki wake!
Pamoja na kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanaendesha maisha yao ya kila siku kupitia kilimo, hakuna anayetamani kuwa mkulima. Ni miongo takribani mitano na nusu toka uhuru kilimo kimeshindwa kumkomboa Mtanzania. Leo hii watanzania ‘walioukata’ kimaisha ni wachache sana watakwambia ‘wameukata’ kupitia jembe. Chanzo ni jembe la mkono. Bila aibu tunashabikia mbwembwe za “kilimo kwanza” kwa kuja na matreka makubwa ya milioni mpaka arobaini eti kumkomboa mkulima na kilimo cha kisasa. Ni wakulima wangapi Tanzania yetu wanaweza kununua trekta na wakati hata jembe la kukukotwa kwa ngo’mbe limeshindikana? “Ama kweli akutukanaye hakuchagulii” tusi, walisema wahenga.


Takribani miongo mitano toka uhuru kilimo chetu kinategemea mvua. Sio siri kilimo cha kutegemea mvua katika nchi yenye maziwa na mito mingi duniani ni laana. Mvua zikichelewa wakulima roho zinakuwa juu maana ndiyo inakuwa mwisho wao. Nilikuwa nasoma taarifa moja huko india kwamba wakulima wanaongoza kwa kujiua. Sina takwimu kwa hapo kwetu Tanzania na ninadhani watakuwepo tu wengi, ni jukumu letu waandishi wa habari kufanya utafiti. Unajua tatizo letu waandishi wa habari tumejikita mijini kuandika habari za wanasiasa na kusahau wakulima. Leo ukisikia habari ya mkulima basi ujue itakuwa ya maajabu.


Kila mtu leo hii anataka kumlalia mkulima. Mjini Songea kuna kampuni (jina kapuni) inanunua mahindi kwa bei ya kutupwa, yaani ni sh 250 (mia mbili na hamsini) kwa kilo. Ukipiga mahesabu pamoja na kunyeshewa shambani na kupigwa baridi mkulima anaishia kupata sh 30,000 kwa gunia zima. Achilia mbali gharama za mbolea na pembejeo nyingine. Na bado mkulima huyo anapiga magoti mahindi yake yanunuliwe. Hii kama siyo laana kwa mkulima ni nini? Kama mnataka mali, mtayapata shambani: sasa nenda shambani uone mziki wake!


Sasa acha hayo makampuni dhalimu maana tunajua ni ya mabepari wageni, kinachouma zaidi ni pale ambapo watanzania wenzetu wanapokuwa mstari wa mbele kumnyonya huyu mkulima. Siyo siri vyama vya ushirika vinawatenda vibaya wakulima wetu kwakweli. Mzee mmoja katika pitapita yangu huko kijiji cha Mgombasi Namtumbo anasema ni takribani mwaka mmoja sasa hajapata malipo yake ya tumbaku. Hela yenyewe shilingi laki mbili na nusu tu. Sasa kama Rais mwenyewe amechoshwa na wizi huu, vipi kwa wakulima? Sio utani! Gazeti la serikali, “Habari Leo, 19 July” limekiri lenyewe kwamba Rais amechoshwa na wizi unaofanywa na vyama vya ushirika, “Kikwete achoshwa na wizi kilimo”. Kama mnataka mali, mtayapata shambani:Nenda shambani uone mziki wake!


Taarifa kutoka huko Tabora nazo zinadhirisha kwamba mkulima mdogo Tanzania kazi anayo. Huwezi amini eti gharama za usafirishaji wa mfuko mmoja wa mbolea kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora, ni Sh 12,000 na wakati ule wa saruji unasafirishwa kwa Sh 2,000 tu. Ni laana kumnyonya mtu anayekulisha namna hii. Wanajulikana wanaofanya madudu haya, wachukuliwe hatua. Ukimya huu siyo mzuri kwa afya ya wakulima wetu.


Masoko na usafirishaji wa mazao ya mkulima ni janga lingine linalomsumbua mkulima mdogo nchini. Kule Kaisho Milongo wilayani karagwe ndizi za wakulima zinaozea shambani na wakati ndizi hizo hizo ni almas pale jijini Mwanza. Ni kukosekana kwa usafiri, kitu ambacho kinawezekana ila kwa kuwa mkulima si lolote si chocho ndiyo maana ameachwa. Kama mnataka mali, mtayapata shambani: Nenda shambani uone mziki wake!


Anayepanga bei ya kahawa ya mkulima wa Mbinga na Bukoba eti ni mzungu anayeishi huko soko la Dunia. Kulima ulime wewe bei apange mwingine, majanga! Mbona mjapani anatengeneza gari na kupanga bei mwenyewe? Huu ni utumwa mwingine ndani ya nchi huru. Nayakumbuka sana maneneo ya Robert Mgabe kwamba, “ what do you expect from colonizer of yesterday?” yaani unategemea nini kutoka kwa mkoloni wa jana?


Leo kunamashirika lukuki yanashindana kuja Tanzania kufanya biashara dhalimu na mkulima aliyejikatia tamaa. Karibu mikoa yote ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania kunamashirika yamewapatia wakulima mbegu za majaribio. Hili ni balaa lingine. Hawa siyo wajinga mpaka watoe mbegu bure. Hata kanuni za uchumi zimesema, “ No free good under the sun”. 

Napenda kuwakumbusha tu watanzania wenzangu wa uzao wa mkulima kwamba Kuna makampuni zaidi ya 50 yanayotawala biashara ya mbegu za viini tete (GMO) duniani kwa kuhakikisha kwamba mbegu zetu asilia zenye kuhimili ukame na magonjwa ya mimea, zimefutika. Nikutajie machache pengine ukiyaona utachukua tahadhari, ‘Sandoz na Ciba-Geigy ya Switzerland; Royal Dutch/Shell ya Netherlands na UK; Upjohn, ITT, Monsanto, Pfizer na Celanese ya Marekani”.

Tusubiri matokeo yake. Kuna kulia na kusaga maneno. Yatatokea ya huko nchini India ambapo shirika la mbegu na madawa liliwakopesha wakulima wadogo na wengi kwa kushindwa kulipa wameishia kujinyonga. Unaambiwa karibu kila mwezi wakulima 1000 wanajinyonga kwa kushindwa kulipa madeni. Sasa kama unataka mali, we chukua mbegu za majaribio na utaona mziki wake!

Balaa lingine naloliona kwa mkulima mdogo ni pale anapogeuka kuwa “manamba” katika ardhi yake, na kukosa mwanya wa kuendeleza kilimo na maisha. Kunabinti mmoja anaozea ndani baada ya kufanya kazi ya umanamba katika shamba kubwa la uwekezaji pale Lipokela Songea. Binti huyo wakati anatoka shambani aligongwa na gari na kukosa hela ya matibabu. Nawashangaa wanaojiita watetezi wa haki za binadamu na wakati wanaodhulumiwa haki zao wako kibao. Kazi kula pesa ya wafadhili tu ndani ya magari yenye viyoyozi huko Dar es Salaam na Arusha. 

Sasa badala ya kugeuka nyuma na kumsaidia mkulima naye aishi kama binadamu, tunaendelea kupigana vikumbo ulaya kuleta wawekezaji wenye kila nia ya kumuondoa mkulima mdogo kwenye uso wa dunia. 

Mwandishi ni Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari SAUT-Songea. Anapatikana kwa denis_mpagaze@yahoo.com, 0753665484

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA