NAPASUA JIPU: NIDA HAYA MAKOSA MPAKA VITAMBULISHO VYA TAIFA VINATOKA HAMJAYAONA?


Kuna wakati unapoandika vitu vya msingi kama hivi hasa unapoongelea swala linalogusa tabaka tawala unaonekana kama umetumwa na chama pinzani au una malengo fulani ambayo si mazuri ya kuikosoa serikali iliyoko madarakani. Kwa kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ibara ya 18, ibara ndogo ya (1) inanipa uhuru na nguvu ya kutoa mawazo kama mwananchi bila ya kuathiri sheria za nchi.  Sheria inasema hivi “ Bila ya kuathili sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta na kupokea na kutoa habari na dhana zozote na chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Napenda kuangazia jicho langu katika makosa yaliyojitokeza katika vitambulisho vya Taifa, vitambulisho hivi vimechua takribani mwaka mmoja mpaka sasa hivi kuanza kutolewa katika jiji la Dar Es salaam kwa wananchi wa kawaida, usajili wa vitambulisho hivi ulianzia kwanza kwa watumishi wa serikali waliopo jijini Dar Es Salaam kabla ya mikoa mingine. Zoezi la usajili kwa sasa lipo mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara. Serikali inatakiwa kupongezwa kwa hatua waliofikia japo imechelewa kuvitoa ukilinganisha nchi nyingine za Afrika Mashariki. 

Kwa jinsi mchakato wake ulivyoendesha ulikuwa na malalamiko mengi  kutoka kwa wananchi, wananchi walidamka mapema sana kuwahi maeneo ya kujiandikishia walichokikuta uko ni siri yao, foleni zilikuwa ndefu kuliko hata zile za benki tulizozizoea, wengine waliambulia matusi kutoka kwa wafanyakazi wa NIDA mpaka hivi juzi wakati wa kuvipokea mambo yaliendelea kuwa vile vile, badala ya wafanyakazi wa NIDA  kutumia lugha ya ukarimu na kutoa maelekezo kwa wananchi lakini eneo la kuvigawa ikawa ni uwanja wa matusi, aibu gani hii tena unakuta kijana mdogo na mzee ndio wanarushiana maneno mazito mazito na matusi juu.

Hapa ndipo hasa napenda kupaangalia kwa undani zaidi,napenda kunukuu  neno kutoka kwa mkurugenzi Mkuu Bwana Dickson Maimu kutoka katika tovuti ya mamlaka ya vitambulisho vya Taifa NIDA. “Mfumo huu unalenga kujibu maswali makuu manne  ambayo ni  nani ni nani, yuko wapi, anafanya nini na anamiliki nini?  kuwapo kwa mfumo na teknolojia ya smart card ambayo inatumika kutengenezea Vitambulisho vya Taifa ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa  na kutaimarisha ulinzi, amani na usalama wa nchi Tanzania”.
Baada ya kutoa vitambulisho hivi vya Taifa kuna taarifa muhimu na za msingi kabisa hazipo na zinaonekana kutojibu maswali makuu manne kama yalivyosema na Mkurugenzi mkuu.
katika kitambulisho hiki, napenda kusema kwamba nimebaini makosa makuu 4 yaliyofanywa kwa uzembe na mamlaka husika NIDA, imefikia hatua sasa unaona kabisa kile kitambulisho cha mpiga kura bado kinaonekana kuwa bora kwa kuwa na taarifa sitahiki na muhimu zote zimewekwa katika kitambulisho hicho. Kwa uzembe huu uliotokea kwa vitu vidogo vidogo kama hivi kusahaulika msishangae kabisa kuona watu wasio watanzania kuwa na vitambulisho vya Taifa.

KOSA LA KWANZA: kitambulisho hakina tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa wa mwenye kitambulisho, kwa kawaida kitambulisho chochote cha taifa, passport, leseni ya udereva, kitambulisho cha mpiga kura kinapaswa kuonyesha tarehe ya kuzaliwa na mwaka waziwazi, lakini kitambulisho hiki ambacho serikali imetoa mabillion ya pesa hata hiki kimesahaulika,na kama sio kusahaulika labda hizi namba nyingi zilizopo yawezekana zikawa zimefichwa zisijulikane kwa haraka ,sasa picha tu na jina ndio litaridhisha? Kwa nini passport, leseni ya udereva na kitambulisho cha mpiga kura wameweka? Kitambulisho hiki ndicho mama kinatumika sehemu nyingi katika upataji wa huduma, mfano shule, afya, mawasiliano, huduma za kifedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), BRELA, mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF,PPF,PSPF, mahakama, polisi, nk  kuna wakati wanataka kujua umri wa mtumiaji wa kitambulisho hicho. NIDA kuna lolote la kujitetea hapa, obvious watasema iko kwenye system sasa sijui ili tuweze kuona umri hizo mashine zitakuwa kila ofsi ili kujua.
Tarehe na mwaka wa kuzaliwa hiki ni cha Uganda

KOSA LA PILI: Kitambulisho hakionyeshi makazi rasmi ya mwenye kitambulisho,(Permanent residence) hata ili hamkuliona kwenye vitambulisho vya mwanzo kabisa, kitambulisho hiki kilipasa kuonyesha mtumiaji wake anakaa Mkoa gani, wilaya ipi, kata ipi, mpaka mtaa na nyumba namba, hata kama amepanga siku akiama eneo ilo  lakini taarifa zake zitakuwepo kwenye nyumba aliyokuwa akiishi itakuwa rahisi kumpata.  Swala la kuonyesha makazi katika kitambulisho ni muhimu sana mfano wakati wa ajali,kupata huduma za kifedha kama mikopo lazima taasisi za kifedha ijue mteja wao anaishi wapi  lakini pia pindi kitambulisho kinapo potea inakuwa ni rahisi kukirudisha eneo au mkoa husika kwa kuwa watu wanasafiri kila siku kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuna swala la majanga, Serikali hupata changamoto kubwa ya kuwalipa fidia au kuwasaidia pindi wananchi wake wanapopatwa na majanga mbalimbali, mfano mabomu ya Mbagala, Gongo la Mboto na mafuriko ya Kilosa, mwisho wa siku watu wanaotakiwa kupata msaada hawaupati lakini kitambulisho hiki kiwekwa taarifa zake za makazi pale juu inakuwa rahisi kuhudumiwa, vipi kuhusu mtu anapojihusisha na vitendo vya kiuharifu polisi inawasaidia kufanya upelelezi kirahisi kuanzia sehemu anapoishi na kujua mwenendo wake eneo la makazi sio tena kwenda NIDA kitambulisho chake kinamsaidia afsa wa jeshi la  polisi kufanya upelelezi.
Sample ya Marekani wameweka mpaka group la damu, shughuli ufanyazo,mahali unapoishi, rangi ya nywele


KOSA LA TATU: Kitambulisho hakina sahihi ya mtumiaji, basi hata kama mwananchi haujui kusoma na kuandika lipo dole gumba, Bank wameanza kuvikataa kwa kuwa hakuna sahihi ya mwenye kitambulisho,kwa taratibu za kibenki inapaswa kuoanisha sahihi iliyopo kwenye kitambulisho chako kama passport, leseni ya udereva na kile kinachotumika benki, sasa kutokana na mapungufu haya imefikia hatua hata benki yenyewe kuona hakifai.
sehemu ya sahihi na dole gumba imewekwa, hiki ni cha KENYA.


KOSA LA NNE: Kitambulisho kina mwisho wa matumizi yake (EXPIRE DATE) Hapa napo pameniachana na maswali mengi bado sijapata jibu kamili labda mpaka litakapotolewa ufafanuzi tena ukaniingia, leseni za udereva ni sawa kabisa kwani kuna kuwa na utaratibu wa kubadilisha madaraja sasa tukirudi kwenye hoja ya msingi kulikuwa kuna maana gani ya kuweka expire date? Ina maana ndio siku mwenye kitambulisho anakufa!! jibu hakuna Mungu ndie anayejua siri hii, au ndio mwisho wa dunia!!!.........bado najiuliza basi tuseme ndio utakuwa ukomo wa kuwa wananchi wa Tanzania labda nchi itakuwa chini ya mwekezaji na kuamua kubadilisha jina nacheka kimoyo moyo, haya yote ni mawazo tu niliyonayo mimi Nyanja juu ya kuweka expire date huku taarifa za msingi mnaziacha, lakini mwishoni nimepata jibu si watarudishwa tena ikifika mwaka huo 2023 kupata tena tenda ya kutengeneza vipya ili watengeneze tena madudu yao na serikali iingine gharama mpya kwa maana kwamba vitakuwa vimefikia ukomo wa matumizi yake, havitakuwa halali tena. Japo kuna baadhi ya nchi nyingine wanatumia na ukiona kwenye specimen wameonyesha lakini swala linabaki kwa nchi yangu na tayari makosa yanaonekana hapo.

Nahitimisha kwa kusema kwamba,Mkurugenzi mkuu wa NIDA, Dickson Maimu pamoja na watendaji wenzake wa mamlaka hii angalieni makosa hayo kwa undani na mtafute suruhisho mapema kabla ya kuendelea kutengeneza vitambulisho vingine vyenye makosa, kwani kwa kuwa ni mkoa mmoja tu ambao mmeshatoa vitambulisho hivi na sio wote wameshavipata na bado zaidi ya mikoa 20 bado havijatolewa tafadhari chukueni hatua ya kurekebisha mapungufu hayo mapema.

Imeandikwa na Nyanja Kelvin Poti.
Mawasiliano: 0715 019393
Mail:kelvinnyanja@gmail.com
Twitter:nyanja255
instagram: nyanja255
Think positive to help your national.

Comments

  1. Tarehe ya kuzaliwa ipo kwenye hizo namba za juu angalia vizuri wameanza na mwaka,mwezi,tarehe

    ReplyDelete
  2. Ni kweli kabisa.hii ni kutokana na haraka,vitu hivyo ni muhimu

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA