Hotuba ya KUB - Wizara ya Fedha na Mipango na maoni kuhusu hali ya uchumi, makadirio na matumizi
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
_________________________
1. UTANGULIZI Mheshimiwa Spika, Mwanafalsafa Baron Montesquieu aliwahi kuandika ifuatavyo kuhusu mgawanyo wa madaraka “Pale ambapo madaraka ya Bunge na ya Serikali kuu yanakuwa yamehodhiwa na mtu mmoja, au katika chombo hicho hicho cha hukumu, hakutakuwa na uhuru, kwa sababu hofu itazuka, utawala huo huo au bunge litatunga sheria kandamizi na kuzitekeleza kwa mfumo kandamizi. Pia hakutakuwa na uhuru endapo madaraka ya Mahakama, Bunge na Serikali hayatatenganishwa. Pale ambapo madaraka ya Serikali kuu yanapokuwa yamefungamanishwa na Bunge, uhai wa Bunge na Uhuru wake unakuwa katika hatari kubwa ya kudhibitiwa kiholela: kwa kuwa Jaji hawezi kuwa mtunga sheria. Pale ambapo Serikali kuu imefungamanishwa na mahakama, basi Jaji anaweza kuwa na tabia ya mabavu na ukandamizaji. Inakuwa mbaya zaidi, pale ambapo mtu huyo huyo au chombo hicho hicho, iwe ni wateule wa Serikali au watu wengine wanapotumia hayo madaraka ya kutunga sheria, kutekeleza maazimio ya umma na kutoa hukumu za jinai au tofauti za watu”
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa mada iliyowasilishwa na Profesa P.J. Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juu ya “Mafundisho ya Mgawanyo wa Madaraka na jinsi yanavyotumiwa Tanzania” (Doctrine of Separation of Powers and its Application in Tanzania: Success, Challenges and Prospects) ni kwamba; hakuna mgawanyo dhahiri wa madaraka baina ya mihilimili mikuu ya dola na kwamba bado Tanzania ina ‘hang-over’ ya ulevi wa siasa za chama kimoja . Sehemu ya Mada hiyo inasomeka hivi: nanukuu; “Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 bado inatumika mpaka leo pamoja na kuwa marekebisho yalikuwa mfano wa Ustawishaji wa mfumo wa chama kimoja nchini Tanzania. Katiba pia iliendelea kustawisha dhana ya Ukuu wa Chama kushika hatamu. Ibara ya 3 na 10 zilibainisha kuwa CCM ndio chama pekee cha Siasa Tanzania na kuwa shughuli zote za Serikali ilibidi zifuate sera na miongozo ya chama. Hii ilimaanisha kuwa Bunge na Mahakama vilitakiwa kufuata maelekezo ya chama katika kutenda majukumu yao. Zaidi ya yote, kama ilivyokuwa kwa Katiba ya Mpito, ibara ya 63(4) ya Katiba ililifanya Bunge kuwa kamati maalumu ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa. Ilikuwa ni jambo la kawaida pale ambapo bajeti ya wizara imekwama basi wabunge waliahirisha mkutano na Bunge lilikaa kama kamati ya Chama ili kujadili hilo suala. Mara tu uamuzi unapofikiwa basi Bunge linarejea na bajeti inapitishwa bila kuwa na upinzani mkubwa”
Katiba ya mwaka 1977 imerekebishwa mara kadhaa. Marekebisho makubwa zaidi yalikuwa ni yale ya tano, ambayo yaliingiza Haki za Binadamu katika Katiba, na marekebisho ya nane yaliyofanyika mwaka 1992 yaliyorejesha tena Mfumo wa Vyama Vingi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maudhui ya nukuu ya mwanafasafa wa kale wa Sayansi ya Siasa Montesquieu, mada ya Profesa Paramagamba John Kabudi, na tabia isiyokubalika ya Serikali kuendelea kushawishi Mahakama na kulidhibiti Bunge kwa hila mbalimbali ni kwamba, Tanzania sasa iko katika hatari kubwa ya kuingia katika mfumo wa Dola la Kidikteta na tayari dalili zote za utawala wa namna hiyo zimeanza kuonekana.
Mheshimiwa Spika, vitendo vya hivi karibuni vya Serikali hii kukanyaga uhuru wa vyombo vya habari kwa kufuta kabisa usajili wa baadhi ya vyombo vya habari, kupiga marufuku urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya mijadala ya Bunge kupitia televisheni ya Taifa, kuingiza polisi ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwapiga na kuwadhalilishwa wabunge; kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni sehemu tu ya tabia za utawala wa kidikteta.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakemea kwa nguvu zote ukandamizaji wa demokrasia na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Serikali ya Tanzania dhidi ya watu wake. Aidha, tunataka Jumuiya ya Kimataifa ijue na dunia ijue kwamba sasa Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia tena – kinachofanyika ni utekelezaji wa amri za Rais – yaani Presidential decrees.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Serikali ya 2016/17, napenda kuweka rekodi sawa kuhusu upotoshaji unaofanywa na Wabunge wa CCM kwamba Wabunge wa Upinzani wanaisaini mahudhurio bungeni na kuchukua posho bila kufanya kazi. Napenda mkumbuke kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikisisitiza kufutwa kwa posho za vikao kwa maana ya “Sitting allowance”, lakini serikali imekuwa ikipata kigugumizi, hivyo basi Kambi Rasmi inasema kama kweli Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inania thabiti ya kubana matumizi ya Serikali basi inoneshe uthabiti huo kwa kuifuta posho ya vikao na fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo hususani kuwapatia Watanzania maji safi na salama. Hata hivyo, tunashauri, wale wanaokaa bungeni bila kuchangia hata kwa maandishi na kuchukua posho, wafuatiliwe na wakatwe mishahara yao, kwa kuwa hawajafanya kazi na hansard itumike kuwabaini.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada kuongeza mapato, Serikali katika bajeti hii imekusudia kukata kodi ya asilimia 5 kwenye kiinua mgongo cha wabunge. Kambi Rasmi ya Upinzani haina tatizo na pendekezo hilo, ila inaitaka Serikali kwenda mbali zaidi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa ambayo kwa sasa imewapa misamaha ya kodi ya viinua mgongo viongozi wakuu wa kisiasa kama Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Spika, Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili sasa na wao walipe kodi hiyo. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaikumbusha Serikali kwamba kiinua mgongo cha wabunge hutolewa mwisho wa uhai wa bunge husika, hivyo haioni mantiki ya kutoa pendekezo hili sasa kwa kuwa halina impact kwa bajeti ya 2016/17.
2. HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, tunaposema hali ya uchumi tunaangalia uchumi kwa ukubwa wake (Macro economy) katika nchi, mataifa yanayotuzunguka na kwa dunia nzima, na ni kwa vipi sera zetu za uchumi zinavyoathirika na uchumi wa dunia, na ni kwa jinsi gani watunga sera wanatakiwa kuwa na mikakati itakayoweza kukabiliana na sera za wale tunaotengamana nao kibiashara.
Mheshimiwa Spika, Na katika hili ni lazima tuangalie ni jinsi gani uchumi mdogo (micro-economy) ambao ndio nguzo kuu ya nchi kwa maana unaowafanya wananchi waweze kuishi, au sera za uchumi zinazoendesha biashara ndogo ndogo kati ya kampuni na kampuni, na zinaangalia jinsi biashara zinavyoweza kufanikiwa kwa kiwango cha juu na aidha, namna gani maamuzi ya biashara yanatakiwa kufanywa ili biashara ziweze kufanikiwa, kwa maana nyingine ni kushughulika na “supply and demand”, jinsi ya kufikisha uchumi kwenye mifuko ya watu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, kukua au kutokukua kwa uchumi kutaonekana na jinsi pato la taifa litakavyokua ambalo ni matokeo ya shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma katika mzunguko mzima wa uchumi. Katika makadirio yaliyokuwa yametolewa na serikali katika mpango wa maendeleo awamu ya kwanza kwenye ukuaji wa uchumi ilitarajiwa kuwa ukuaji wa pato la taifa lifikie asilimia 8. Hii iliwekwa kutokana na ukweli kuwa kwa mwaka 2011 GDP ilikuwa 7.9%, 2013 GDP ikawa 7.3% na miaka miwili mfululizo GDP ikawa 7.0% na matarajio kwa mwaka 2016 ni 7.2%.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho ukuaji wa baadhi ya sekta za uzalishaji pamoja na shughuli za utoaji wa huduma ulikuwa kama ifuatavyo; Mawasiliano (14.9%), Huduma za fedha na Bima (10.4%), Ujenzi (10.3%), Kilimo - kwa maana ya mazao, ufugaji,misitu na uvuvi (3.1%) kwa kulinganisha na 3.4% mwaka 2014. Sekta hii licha ukuaji wake kuwa mdogo kwa kulinganisha na mwaka wa nyuma lakini mchango wake katika Pato la Taifa uliongezeka na kuwa 31.4% kulinganisha na 28.9% kwa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za Serikali, inaonesha kuwa kiwango cha riba za amana za muda maalum kiliongezeka kutoka wastani wa asilimia 9.02 Januari, 2015 hadi asilimia 9.08 Januari, 2016, kiwango cha riba za amana kwa mwaka kiliongezeka hadi 11.01% kutoka 10.66% 2015. Riba za mikopo kiliongezeka kutoka 15.75% Jan. 2015 hadi asilimia 16.28 Jan.2016, wastani wa riba za amana za mwaka na riba za mikopo za mwaka iliongezeka kutoka wastani wa 3.14% Jan.2015 na kufikia 3.33% Jan.2016 Kambi Rasmi ya Upinzani inasema riba hizi zingeweza kuongezeka kama Serikali isingekuwa inafanya biashara kubwa na mabenki na hivyo kupelekea mabenki kushindwa kuhamasisha wananchi kufanyabiashara nayo.
2.1 USIMAMIZI WA TAASISI NDOGO-NDOGO ZA FEDHA
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inapenda kusisitiza tena kwa Serikali kuleta muswada wa sheria ambao utaanzisha mamlaka ambayo itatoa kisheria muundo wa kudhibiti na kusimamia taasisi ndogondogo za fedha nchini ambazo kwa sasa zimekuwa zikisimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na taasisi nyingine za kifedha kama mabenki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona haja ya kuwa na mamlaka huru iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania ya kusimamia taasisi ndogondogo kama ambavyo Benki Kuu ya Tanzania imeruhusu uanzishwaji wa mamlaka za kusimamia mifuko ya hifadhi za jamii, bima na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa chombo chenye mamlaka ya kusimamia taasisi ndogondogo za fedha ni lazima kwa kuwa kwa sasa hakuna mrandamo wa viashiria kwa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha. Kutokana na utofauti wa muundo wa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha, inakua ni vigumu kudhibiti riba na utoaji wa vigezo vya kifedha katika kuhudumia wananchi na kutoa mikopo yenye unafuu.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani ni kuwepo na chombo chenye mamlaka tofauti na Benki kuu ya Tanzania itakayosimamia na kuratibu taasisi ndogo ndogo za fedha na kuziwezesha katika kutoa mikopo kwa wananchi hasa walio katika sekta isiyo rasmi. Hivi sasa kumekuwapo na taasisi ndogondogo za kifedha ambazo zinawapa fursa wananchi kujiunga katika vikundi vidogo vidogo na kuwapa elimu ya ujasiriamali kisha kuwasaidia katika suala la mikopo ambayo utakaoweza kuwapa fursa watanzania waliopo katika sekta isiyo rasmi kama wamachinga, mama lishe, mafundi uashi na wajenzi, mafundi magari na seremala ambao chombo hicho kingeweza kusimamia ukusanyaji wa fedha kutoka katika makundi haya na kuweza kuwekeza kwa ajili ya kusaidia kutoa mitaji pale inapohitajika.
Mheshimiwa Spika, hili ni suala zuri ambalo linalenga kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini na maeneo mbalimbali ya mijini. Pia, zipo Saccoss (vyama vya kuweka na kukopa) na benki jamii (vicoba) ambazo zimekuwa na wanachama wengi wanaoendelea kujiunga ili kujikwamua kiuchumi. Lakini kumekuwa na mapungufu kwa kuwa taasisi ndodondogo za fedha zimeendelea kutumia masharti sawa na zile za mabenki ambazo zimekuwa ni mzigo kwa mlengwa ambaye ndiye analipa riba kubwa kutokana na masharti mazito yenye kulingana na vigezo vya kutoa mikopo kwa mabenki chini ya Benki kuu ya Tanzania. Kwa mfano, taasisi za fedha chini ya Benki Kuu bado zimeendelea kumtaka mtu awe na dhamana ya mali isiyohamishika na zile wanazojidhamini kwa vikundi. Je, itawezekanaje kwa Mwananchi mwenye hali duni kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika?
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa chombo chenye mamlaka pia itasaidia kuwa na Credit Reference Bureau itakayokuwa na taarifa za wakopaji kutoka taasisi ndogondogo za fedha tofauti na itakayosimamia wadaiwa wa mabenki na taarifa hizi zitasaidia udhibiti wa wateja wa taasisi hizi kuchukua zaidi ya mkopo mmoja kwenye taasisi tofauti tofauti ambapo hali hii husababishwa na uchelewashaji wa mikopo unaotolewa na taasisi hizi pamoja na uhafifu wa mikopo katika kumsaidia mlengwa.
3. MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO 2016/17
3.1. Ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017
Mheshimiwa Spika, moja ya sifa kubwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliomaliza muda wake (2011/12 – 2015/16) ni kuweka msingi wa kibajeti ulioitaka Serikali kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mpango ulisema hivi: nanukuu, “kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uhalisia kwamba Mpango huo haukutungiwa sheria ya utekelezaji; Serikali ilijificha katika kichaka cha udhaifu huo; na matokeo yake kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo, Serikali haikuwahi hata mara moja kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuna wakati mwingine haikutenga hata senti moja. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali haikutenga fedha yoyote kutoka katika mapato yake ya ndani kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kugoma kutoa asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi mingi ya maendeleo haikukamilika hadi mwisho wa muda wa utekelezaji wa Mpango.
Mheshimiwa Spika, kutokana na aibu ambayo Serikali iliipata kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo kwa kushindwa kutekeleza utaratibu iliyojiwekea yenyewe wa kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kugharamia mpango wa Maendeleo; safari hii Serikali imefuta utaratibu huo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21).
Mheshimiwa Spika, tafsiri rahisi ya uamuzi wa Serikali hii ya CCM inayojinasibu kwa kauli ya “hapa kazi tu” kufuta msingi wa kibajeti wa kugharamia mpango wa maendeleo kwa kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani ni hofu ya kushindwa kutekeleza commitment hiyo kama ambavyo ilishindwa kufanya hivyo katika Mpango uliomaliza muda wake lakini pia ni kukwepa kuwajibika au kuwajibishwa na Bunge kwa hofu hiyo hiyo ya kushindwa kutekeleza. Kwa hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inadhani ni bora Serikali hii ikakubali uhalisia kwamba imetawaliwa na hofu tu na sio kazi tu kwa kuwa inakimbia kivuli chake yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kwamba: “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake, Bunge laweza; kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo; hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta Muswada wa Sheria ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaopendekezwa kabla ya kupitishwa na Bunge. Aidha; Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Muswada huo uitake Serikali kutenga asilimia 40 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, suala la kutuga sheria ya kutekeleza Mpango huu sio ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – ni takwa la kikatiba. Ikiwa Serikali hii itapuuzia jambo hili basi ijulikane na iingie kwenye rekodi kwamba Serikali imevunja Katiba ya Nchi.
Mheshimiwa Spika imebidi sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ichukue jukumu la kusimamia misingi ya Katiba ili Serikali hii isiendelee na tabia yake ya kuwa na ndimi mbili katika jambo moja. Nasema hivi kwa sababu; Serikali hii imekuwa na historia ya kulidanganya bunge, na kwa kuwa wanajivunia wingi wa wabunge CCM basi mambo yamekuwa yakipitishwa kiholela bila kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria za Nchi na hata Kanuni za Bunge. Kwa mfano; Serikali imesema katika Mpango wake wa Maendelo wa 2016/17 kwamba imetenga shilingi trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini ukisoma kitabu cha Matumizi ya Fedha za Maendeleo (Public Expenditure Estimates Development Votes) VOLUME IV, fedha zilizotengwa ni shilingi trilioni 10.511.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapokuwa na tarakimu tofauti katika suala nyeti kama hili la Bajeti ya Serikali, tunapata mashaka makubwa sana na weledi wa watendaji wa Serikali akiwemo kiongozi wao mkuu. Katika hali kama hiyo, ni lazima kuwa na sheria itakayotoa mwongozo kwa Serikali juu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ambao unatumia fedha za umma.
3.2. Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Agenda 2030 ya Dunia ya Maendeleo Endelevu
Mheshimiwa Spika, tarehe 25 Septemba, 2015 Dunia iliingia mkataba wa kutekeleza malengo 17 ya agenda 2030 ya kuibadilisha Dunia na kuwa mahali salama zaidi pa kuishi kwa kuweka malengo ya kuwa na maendeleo endelevu. Malengo hayo ni kama ifutavyo:
Lengo Na. 1. Kuondoa umasikini wa aina zote
Lengo Na. 2. Kuwa na kilimo endelevu, Kuondoa njaa na kuwa
na uhakika wa chakula na lishe bora kwa watanzania wote.
Lengo Na. 3. Kuhakikisha kuwa jamii ya rika zote inakuwa na afya bora.
Lengo Na. 4. Kuhakikisha fursa ya elimu bora na iliyo shirikishi kwa watanzania wote.
Lengo Na. 5. Kutoa usawa kwa jinsia zote na kuwawezesha akina mama na wasichana wote.
Lengo Na. 6. Kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa watanzania wote.
Lengo Na.7. Kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati endelevu na ya kisasa kwa wote.
Lengo Na. 8. Kukuza ajira endelevu na zenye staha na ukuaji wa uchumi shirikishi.
Lengo Na. 9. Kujenga miundombinu bora na shirikishi ili viwanda viwe endelevu kwa kupokea mabadiliko yoyote.
Lengo Na. 10. Kupunguza tofauti za ndani na baina ya mataifa kwa walionacho na wasio nacho.
Lengo Na. 11. Kufanya miji yetu na makazi shirikishi, endelevu na salama.
Lengo Na. 12. Kuhakikisha uzalishaji endelevu utakaoendana na matumizi.
Lengo Na. 13. Kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Lengo Na.14. Kutunza na matumizi endelevu kwa maendeleo ya rasilimali za baharini.
Lengo Na.15. Kulinda na kuwa na matumizi endelevu ya ‘terrestrial ecosystem’, kutunza misitu na kupambana na ukame na kurudisha uhalisia wa ardhi.
Lengo Na.16. Kuwa na taasisi imara ili kuwa na haki na amani,
Lengo Na.17. Kuimarisha ushiriki wa pamoja katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia, na kwa kuwa Tanzania haiwezi kusimama peke yake na kufanikiwa katika kufikia malengo yake ya maendeleo kama haishirikiani na mataifa mengine, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetekeleza kwa kiwango gani agenda ya Dunia ya 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu?
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa malengo yote 17 ya maendeleo endelevu ya dunia ni muhimu kwa nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa mchanganuo wa kina wa jinsi kila lengo lilivyotekelezwa na kiwango cha utekelezaji (asilimia) kwa kila lengo. Aidha, tunaitaka Serikali kutoa majibu ya ziada na ya kipekee ya namna ilivyotekeleza lengo la 16 la Kuwa na Taasisi imara ili kuwa na Haki na Amani.
Mheshimiwa Spika, Tumeweka msisitizo katika lengo hili kwa kuwa haki inaleta amani na amani ni tunda la Maendeleo. Kwa hali ilivyo sasa hapa nchini, kuna dalili zote kwamba taasisi zetu haziko imara jambo ambalo linafifisha jitihda za kuwa na haki na amani katika nchi yetu. Kama taasisi zetu hasa za kutoa haki zingekuwa imara ni dhahiri Zanzibar kusingekuwa na hitajio la uchaguzi wa marudio. Jambo hilo linatia mashaka kama Tanzania tutaweza kukidhi malengo endelevu ya maendeleo kama Agenda 2030 ya Dunia inavyohitaji.
4. UCHUMI WA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, kwa nchi yoyote Duniani ambayo uchumi wake unaendelea kukua ni dhahiri kuwa sekta ya viwanda inakua kwa kasi inayoridhisha na sekta hiyo ina uhusiano wa moja kwa moja na sekta zinazotoa malighafi kwa sekta ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, Kuwa na uchumi wa kipato cha kati kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda ni lazima kama nchi iwe na malengo ambayo yako wazi kuhusu aina ya sekta zitakazowekezwa ili iwe chachu ya kututoa hapa tulipokwama kwa kipindi chote. Ili malengo yawe wazi ni lazima kuangalia mazingira yetu ya ndani na mazingira ya nje ambayo kwa njia moja au nyingine yana uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji wa viwandani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaposema malengo yaende sambamba na mkakati mzuri wa utekelezaji, ni kwamba utakapo chagua viwanda viwe katika sekta kama: bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, kemikali, misitu na/au huduma; nk. Ni lazima ujenzi wa viwanda kufuatana na sekta tajwa hapo juu uhitaji upembuzi yakinifu wa hali ya juu hadi kufikia maamuzi ya wapi viwanda hivyo vijengwe kwa kulingana na kiwango cha rasilimali zilizopo na kiwanda kitakachojengwa ni kwa muda gani kitaweza kurudisha mtaji na ajira kiasi gani zitazalishwa. Na pia kuangalia nchi za jirani zina kiwanda kama hicho na uwezo wake wa kuzalisha bidhaa na ubora wa bidhaa zake ukoje (uhimili wa ushindani wa bidhaa). Je, aina ya teknolojia itakayotumika kuzalisha bidhaa itaweza kutumiwa na wananchi wetu (rasilimali watu ya hapa hapa ndani ya nchi) au kitakuwa tegemezi kwa wataalamu wa nje?.
Mheshimiwa Spika, Mojawapo ya malengo ni kuhakikisha yanakidhi mahitaji ya ndani kwa bidhaa zinazozalishwa, kuwa soko la malighafi ya bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa kuwa nguzo kuu ya mnyororo wa thamani, kwa kuubadili mfumo wa uchumi ambao ulikuwa tegemezi kwa sekta za kilimo, madini na huduma na kuwa uchumi tegemezi kwa sekta ya viwanda. Pia kuwezesha bidhaa zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la Afrika ya Mashariki na soko la nchi za Kusini mwa Afrika .
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasema ili kuwa kweli nchi yenye uchumi wa viwanda na hivyo kupelekea kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati, tuna hitaji mkakati mzuri na utekelezaji wake wa kutufikisha huko na sio matamanio na mahubiri tu, kama yanavyotolewa na viongozi wetu.Viwanda siyo tu vinakuza uchumi kwa kuongezea bidhaa thamani bali pia vinatengeneza ajira nyingi kwa haraka na kwa sekta nyingine.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 ni mwaka wa kwanza kwa awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa 2025, japokuwa ni mwendelezo wa awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo, hivyo basi ni muhimu kuangalia uwekezaji ambao tayari umefanyika katika sekta nzima ya uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya China wameanzisha kituo cha Biashara kwa ajili ya bidhaa toka China (Kurasini Logistic Center) ambapo hadi sasa Tanzania imekwishatoa shilingi 65,279,464,100/-ambazo ni sawa na Asilimia 72% ya fedha zilizotakiwa kutolewa na Serikali kwa ajili ya fidia kwa wakazi wa kurasini.
Mheshimiwa Spika, dhana nzima ya uwekezaji wa pamoja katika kuanzisha Kituo hiki, kwamba bidhaa mbalimbali toka China zitakuwa zinaletwa hapo na wafanyabiashara wa nchi za Afrika ya mashariki na zile za Kusini mwa Afrika badala ya kwenda China kufuata bidhaa, basi watakuwa wanapata bidhaa zote Dar es Salaam. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kwamba uwekezaji uliokwishafanywa na unaoendelea kufanywa katika kuanzisha kituo hicho ni dhahiri kwamba unapingana na dhana nzima ya awamu ya pili ya Mpango wa maendeleo wa 2025 kuwa ni kuifanya nchi kuwa na uchumi wa viwanda.
4.1. SEKTA YA NYUMBA NA UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mwaka 2011, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe (Mb) akiwasilisha Bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alipendekeza kuwa pamoja na mambo mengine kuna ulazima kama taifa kuwa na mamlaka udhibiti wa sekta ya nyumba (Real Estate Regulatory Authority) itakayokuwa na jukumu la kusimamia sekta ya nyumba nchini hasa majengo makubwa ili kuwa chanzo cha mapato ya serikali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pendekezo hilo kutolewa wakati huo serikali wakati wa bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imependekeza mwaka ujao wa fedha 2016/2017 imeahidi kuleta Bungeni muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya nyumba nchini. Ni msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa pendekezo hili limechelewa sana. Kama serikali ingelitekeleza jambo hili mapema, serikali ingelipata chanzo cha mapato.
Mheshimiwa Spika, majirani zetu wa Kenya ndani ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki, sekta ya nyumba imechangia pato la taifa kwa 10.6% sekta hiyo ikiwa ya nne katika kuchangia katika uchumi wa nchi hiyo. Aidha athari za kuanguka kwa bei ya mafuta duniani haijaathiri uchumi wa Dubai kwa sababu ya kuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya nyumba.
Mheshimiwa Spika, tamwimu zinaonesha kuwa Tanzania kuna uhitaji wa nyumba 200,000 kila mwaka na uhaba wa nyumba milioni 3. Hii ni kutokana na ongezeko la kasi la idadi ya watu nchini pamoja na uhitaji wa nyumba zenye hadhi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa serikali haijawa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha tunatumia fursa ya sekta ya makazi kukuza uchumi wa nchi yetu kama ambavyo mataifa mengine yamepiga hatua kubwa kwa kutumia fursa hiyo.
4.2 KODI YA MAJENGO (PROPERTY TAX)
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi kodi ya majengo ilikuwa ikikusanywa na halmashauri, lakini kwa sasa serikali imeamua kodi hiyo ikusanywe na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kupelekwa Hazina. Agizo hili litaathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri zetu nchini kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri hasa za Miji, Manispaa na Majiji.
Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa kama fedha zitakusanywa na Hazina na kama utaratibu wa kutoa fedha hizo kwenda Halmashauri utaendelea kama ilivyo sasa ambapo fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu zinachelewa kupelekwa kwenye Halmashauri basi tusitegemee kuwa fedha za kodi ya majengo zitanuifaisha tena Halmashauri zetu.
Dhana hii ni kutokana na ukweli halisi ambao upo kwenye kodi ya ardhi ambayo ilikuwa inakusanywa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi ilionyesha wazi kuwa ikishafika wizarani ilikuwa vigumu sana kurejeshwa kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Hii ni kutokana na sababu kuwa serikali mara nyingi imekuwa ikipeleka fedha Halmashuri katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa serikali itafikiria upya uamuzi huu ambao utapunguza sana mapato ya Halmashauri zetu na kuzifanya kushindwa kutoa huduma kwa wananchi wake.
4.3 SEKTA YA UTALII
Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni sekta ambayo inachangia fedha za kigeni katika sekta nzima ya uchumi (foreign exchange earner), kwa kuwa na watalii milioni moja wanaochangia asilimia 17.7 ya pato la Taifa (GDP). Kwa mujibu wa takwimu za nchi nzuri duniani ni kwamba; Tanzania ni namba 8 kati ya mataifa 20 yenye vivutio vizuri na vingi Duniani kwa ajili ya watalii. Lakini kuwa na vivutio vingi sio sababu ya kuwa na watalii wengi, ila sababu kubwa ni jinsi gani unajitangaza na unawavutia vipi watalii? Takwimu zinaonesha kuwa Ufaransa ndiyo nchi inayoongoza kuwa na watalii milioni 83.77 kwa mwaka wakati katika zile nchi 20 haimo. Afrika ya Kusini inapokea watalii 9,616,964 kwa mwaka, lakini katika orodha inachukua namba 1, Kenya ambayo ilikuwa imefikisha watalii milioni 1.7 kabla ya tishio la ugaidi, sasa inatarajia watalii milioni 1.6, Uganda inapokea watalii 1,266,000 kwa mwaka, Zimbabwe inapokea watalii 1,905,000 na Msumbiji 1,661,000
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama tutaweza kuongeza idadi ya watalii hata kufikia milioni 5 kwa mwaka ni dhahiri uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, Ili Tanzania iweze kupata watalii milioni 5 kwa mwaka, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba Serikali iimarishe kwanza usafiri wa anga. Hali ilivyo sasa, watalii wanapata tabu sana kufika Tanzania kutokana na gharama kubwa inayosababishwa na kutokuwepo usafiri wa uhakika wa ndege. Tunashauri kwamba Serikali iweke mkakati mahususi wa kuwashawishi marafiki zetu wa China ili shirika lao la ndege lianzishe safari za kuja Tanzania, na vile vile mashirika ya ndege toka Marekani kuwa na safari za Tanzania kila wiki. Pili, tozo katika viwanja vyetu vya ndege zipunguzwe ili kuvutia watalii. Tatu huduma zinazotolewa kwa watalii huko mbugani ziboreshwe na kuwa na kiwango cha kimataifa ili kuwavutia watalii zaidi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na misimamo ya Serikali isiyokuwa ya kibiashara ni kwamba utalii kuwa na faida sana inategemea na idadi ya watalii wanaoingia, hivyo kama Serikali itakubali kuwa kipindi kisichokuwa cha msimu wa utalii ni vyema bei zikashuka ili idadi ya watalii na siku za kukaa nchini iongezeke. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuja kwa watalii kuna wanufaisha watu wengi sana mbali ya Serikali kupata mgawo wake, ni muda mwafaka sasa Serikali kuwa-“flexible” ili kuwa kibiashara zaidi.
Mheshimiwa Spika, Tunaitaka Serikali kutumia mfano wa jirani zetu Kenya, ambapo Rais Uhuru Kenyatta amefuta tozo za kutua kwa ndege zote za kukodi zitakazokuwa zinaleta watalii nchini Kenya .
5. VITUO VYA KUUZA UTALII WA TANZANIA NJE
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Utalii imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa muda mfupi wakati wa maonyesho mbalimbali ya utalii yanayofanyika nje ya nchi. Ili kuwe na ujio endelevu wa watalii nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali iweke vituo vya utangazaji wa utalii wetu katika balozi zetu katika nchi za Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Uchina, Japani, Canada na nchi za Scandinavia na kuwe na watumishi maalumu watakaoajiriwa katika vituo hivyo kwa kazi maalum ya kuhakikisha kuwa wanatangaza vivutio vyetu na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja hapa nchini. Mkakati huo ukifanikiwa ni dhahiri kwa mwaka mmoja tunaweza kupokea watalii zaidi ya milioni tano.
Mheshimiwa Spika, fursa hii si kila mtu anaweza kuiona, hivyo ni muda muafaka kuwashawishi wachina wawekeze katika hoteli za kitalii, badala ya wawekezaji hao kushindana na watanzania katika maduka ya vifaa vya ujenzi pekee. Kwa njia hii tutaweza kuvuta soko la watalii wengi toka China.
6.0 SERIKALI YA HAPA KAZI TU, IMELETA BAJETI HEWA BUNGENI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni wajibu wa Bunge kupanga na kuidhinisha mapato na matumizi ya serikali kila mwaka wa fedha .Hii ni kwa mujibu wa ibara ya 137(1)’Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya ‘Mapato na Matumizi’ ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata’
Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/17 serikali imewasilisha bajeti hewa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, ninasema kuwa serikali hii imeleta bajeti hewa hapa Bungeni na nitathibitisha maoni yangu haya kama ifuatavyo;
1. Kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka huu wa fedha volume 1 ‘Financial Statements and Revenue estimates’ for the year 1st July ,2016 to 30th June 2017 kilicholetwa hapa Bungeni kinaonyesha kuwa mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi , yasiyokuwa ya kodi ,mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi Trilioni 22.063.
Mheshimiwa Spika, upatikananji wa mapato hayo ni kama ifuatavyo;
i. Mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali ni shilingi Trilioni 17.797
ii. Mapato yasiyokuwa ya kodi ni shilingi Bilioni 665.664
iii. Mikopo na misaada ya kibajeti ni shilingi Trilioni 3.600
Mheshimiwa Spika, ni muhimu Waheshimiwa Wabunge wakatambua kwamba Serikali hii haijaonyesha chanzo kingine kipya cha mapato ambacho hakijathibitishwa na au kupitishwa na Bunge hili kwa mujibu wa katiba na ijulikane pia kuwa Bunge halipitishi kitabu cha hotuba ya waziri bali hupitisha mafungu yaliyopo kwenye vitabu vya bajeti ya serikali.
2. Kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida ,volume II Estimates of Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July ,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha Maendeleo, Volume IV Public Expenditure Estimates Development Votes (part A) kama vilivyowasilishwa Bungeni , tayari bunge limeshaidhinisha matumizi ya jumla ya shilingi Trilioni 23.847
Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:
i. Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) shilingi 13,336,042,030,510
ii. Fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo (Volume IV) shilingi 10,511,945,288,575
3. Ukichukua kitabu cha Mapato ya Serikali (Revenue Book Volume I) utaona kuwa jumla ya mapato yote ya serikali ni shilingi Trilioni 22.063 , ila serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 23.847 ambacho ni kiasi tofauti na Mapato ambayo serikali imepanga kukusanya na tofauti yake ni kuwa kuna nakisi ya shilingi Trilioni 1.783 jambo ambalo linaifanya bajeti hii kukosa uhalali kwani nakisi hii ni kubwa sana.
4. Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa fedha ‘Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwenye mkutano wa wabunge wote katika ukumbi wa JNICC’ mnamo tarehe 06 Aprili, 2016 pamoja na maelezo ya hotuba yake aliyoyatoa hapa Bungeni uk. 91 ameendelea kulidanganya Bunge na Dunia kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali ina bajeti ya kiasi cha shilingi Trilioni 29.539
5. Hotuba ya waziri wa fedha katika ukurasa wa 92 ‘Mfumo wa Bajeti wa Mwaka 2016/17’ inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni 7.475 ni mikopo ya ndani yenye masharti ya kibiashara. Fedha hizi kwenye kitabu cha mapato hazipo na pia hazionekani zitakopwa kutoka Benki gani kama ambavyo mikopo ya nje yote imeonyeshwa kwenye kitabu cha mapato na hata kwenye kitabu cha miradi ya maendeleo hazionekani kwenye kutekeleza mradi wowote ule na hivyo ni sahihi kusema kuwa ni fedha hewa , maana hazina hata kasma yake na Bunge hili tunapitisha kasma .
6. Hotuba ya waziri wa fedha uk.58 anasema kuwa moja ya chanzo chake cha mapato ni pamoja na kurekebisha sheria ya Kodi ya Mapato SURA 332 (i)’kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.’
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu ya kina kuhusu mambo yafuatayo;
i. Bunge linapitisha takwimu zipi hasa? Ni kitabu cha hotuba ya waziri au ni vitabu vya mapato na matumizi pamoja na kile cha Miradi ya maendeleo?
ii. Fedha ambazo waziri kwenye hotuba yake anasema kuwa ni mikopo ya ndani ya masharti ya kibiashara, zinakopwa ili kugharimia miradi ipi? Kwani tayari kitabu cha miradi ya maendeleo VOLUME IV kimeshataja miradi yote na kiasi cha fedha ambazo kila mradi utatumia.Hii miradi inayosemwa kuwa fedha itakopwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni miradi ipi hiyo? Mbona haijapitishwa na bunge au ni miradi hewa?
iii. Waziri wa fedha anaposema kuwa fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi Trilioni 17.719 na hapo hapo anasema kuwa tunakwenda kulipa deni la taifa kiasi cha shilingi trillion 8, mbona hizi fedha hazipo kwenye kitabu ambacho kinapitishwa na Bunge? Kitabu cha matumizi ya kawaida VOLUME IV?
iv. Kwa kuwa CAG anakagua kasma zilizopo kwenye vitabu yaani VOLUME IV na VOLUME II, katika bajeti hii atakagua kasma ipi?maana fedha za kulipia deni la taifa hazipo kwenye kitabu cha VOLUME II na hata mikopo yenye masharti ya kibiashara inayosemwa itakopwa haipo kwenye Revenue Book
v. Huu mkanganyiko wa vitabu vya serikali moja imesababishwa na nini au kuna mikopo na miradi hewa? Ni kwanini kitabu cha mapato (revenue book) kinaonyesha mapato madogo kuliko kiwango cha matumizi?
vi. Kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa fedha 2016/17 hiki si chanzo hewa? Nasema hivi kwa kuwa, kila mwaka tutakuwa tukipitisha bajeti na hiki kilipaswa kuwa chanzo ifikapo mwaka 2020 ambapo ndio kiinua mgongo hiki kinalipwa na ndio kingekuwa chanzo cha mapato au serikali imepanga kulipa kiinua mgongo hicho kila mwaka wa fedha?
Mwisho Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tunaitaka serikali iwasilishe Vitabu vyenye kumbukumbu na takwimu sahihi kabla ya kulitaka Bunge hili kujadili bajeti hii na kuamua kuipitisha au kuikataa, la sivyo Bunge litakuwa halitimizi wajibu wake kikamilifu kwa mujibu wa katiba ya Nchi yetu.
7. WIZARA YA FEDHA NA JUKUMU LA UTEKELEZAJI MPANGO WA KWANZA WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2011/12-2015/16
Mheshimiwa Spika, Mpango huu ni wa kwanza kati ya mipango mitatu ya miaka mitano mitano inayotumika kama chombo katika dhamira ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka ishirini na mitano (Tanzania Development vision(TDV)-2025). Malengo yakiwa ni Tanzania iwe ya kipato cha kati ifikapo 2025 ambayo pamoja na mambo mengine litakuwa taifa lenye:
i) Kiwango cha juu cha mapinduzi ya viwanda
ii) Ushindani na hali nzuri/bora ya maisha kwa wananchi wake
iii) Utawala wa sheria
iv) Jamii ya wasomi waliobobea
Vipaumbele vya msingi (Core Priorities) katika mpango huo ni :
i) Miundombinu / Infrastructure
ii) Viwanda / industry
iii) Maendeleo ya rasilimali watu /human capital development
iv) Nishati
Mheshimiwa Spika, tuangalie mafanikio ya wizara ya fedha katika utekelezaji wa jukumu lake la kusimamia utekelezaji wa mpango wa miaka mitano 2011/12- 2015/16.
1) Reli- mpango ulipanga kukarabati KM 2,707 ya reli ya kati, imefanikiwa kukarabati km 150 tu za Reli
2) Barabara – Kujenga na kukarabati km 5,204 za barabara. Zimejengwa km 2,775
3) Nishati- Ongeza uzalishaji wa umeme kufikia 2,780 MW. Sasa hivi tunazalisha MW 1,461
4) Kilimo - Ukuaji wa mwaka kwa 6%, ukuaji kwa sasa 3.2% (ukuaji huu ni wa kipindi chote toka tupate uhuru….).Kiwango cha umwagiliaji toka 345,690 – 1,000,000. Matarajio yalikuwa ni kuongeza eneo jipya la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekari 645,690. Mafanikio ni nyongeza ya hekari 115,656 tu!
5) Maendeleo ya viwanda na uzalishaji – kukua kwa 11%. Mafanikio ni ukuaji wa 6.6%
6) Elimu - Nyongeza kada ya wasomi wa kiwango cha juu toka 2.7% mpaka 4.3% ifikapo 2015. Idadi imepungua mpaka 2.5%. Halikadhalika kuongeza kada ya wasomi wa kiwango cha kati toka 13.6% mpaka 17.8% ifikapo 2015.Imeongezeka kwa 1% tu kufikia 2015.
Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba tukiwa tunaelekea katika mpango wa pili wa miaka mitano, wizara ya fedha imeshindwa kutekeleza wajibu huu kikamilifu, hali hii inatia mashaka ufanisi wa utekelezaji wa mpango wa pili, wakati mpango wa kwanza umeisha kwa kusuasua!
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu, Ni kwa namna gani serikali imejipanga kuweza kufidia ombwe hili!ili miaka tisa ijayo Tanzania liwe Taifa lenye mapinduzi ya viwanda ya hali ya juu, hali bora ya maisha kwa wananchi wake, utawala bora na Taifa lenye wasomi waliobobea (Rejea taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya jamii)ambayo ilitamka bayana kwamba hali ya elimu nchini ni hatari kwa usalama wa Taifa. Ninukuu maneno ya kamati ‘Taifa letu limejenga mfumo wa elimu ambayo haikidhi DIRA na Mahitaji ya Nchi’.
7.1 UPATIKANAJI FEDHA KUTOKA HAZINA
a) Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi: Hadi kufikia Machi 2016 ,wizara ilikuwa imepokea shilingi 660,333,375,957/- kati ya shilingi 816,080,198,000 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo . Kati ya fedha zote zilizopokelewa kwa ajili ya matumizi ya Wizara, mishahara ilikuwa 52%, matumizi mengineyo ilikuwa 47% na kwa upande wa bajeti ya maendeleo ni 1% tu.
b) Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa: kwa miradi ya maendeleo iliidhinishiwa shilingi bilioni 232.1. Mpaka Februari, 2016 Wizara ilipokea shilingi bilioni 40 tu, sawa na asilimia 17.2 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
c) Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Bajeti ya maendeleo iliyotengwa 2015/16 ni bilioni 440.6, mpaka mwezi machi ikiwa ni robo ya tatu ya mwaka hakuna fungu hata moja ambalo wizara hiyo ilikuwa imepata zilizoidhinishwa na Bunge kwa angalau 50%. Halikadhalika Fungu 52 – Idara kuu Afya hadi kufikia tarehe 31 March 2016 kiasi cha fedha kilichopokelewa ni 31% tu ya Bajeti , halikadhalika fungu 53 kwa Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii jinsia na watoto.
d) Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Katika kipindi cha mwaka 2015/16 wizara ilitengewa jumla ya shilingi 213,079,803,000/- kati ya fedha hizo 32,713,073,000 ilikuwa ni fedha za maendeleo. Hadi kufikia Machi 2016 , fedha za maendeleo zilizokuwa zimepatikana ni bilioni 5.1 ambazo ni sawa na 15.9% tu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, ikubukwe kwamba; Mpango wa kwanza wa miaka mitano (FYDP 1) uliweka malengo ya kibajeti katika sekta ya kilimo (miaka mitatu ya mwanzo) ya shillingi za kitanzania Bilioni 2,710.65 (Trillion 2.7). (ambayo ingewezesha kilimo kukua toka 3.2% ya sasa mpaka 6%). Fedha iliyokuja kutolewa kwa kipindi chote hicho ni shilingi 250.12 billioni sawa na 9.23% ya mahitaji.
e) Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi: Wizara iliidhinishiwa shilingi 511,525,227,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida . Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka, yaani Machi 2016 Wizara ilikuwa imepokea kiasi cha shilingi 316,402,868 ,828.00 sawa na 68%. Kuhusu bajeti ya maendeleo, wizara imepokea jumla ya shilingi 360,922,754,359.61 sawa na 61.9% ya fedha iliyoidhinishwa 582,670,597,884.49. Bodi ya mkopo ambayo ni sehemu muhimu sana ya wizara hii kupitia fungu 46 iliidhinishiwa shilingi 418,300,000,000 kwa ajili ya Mradi Namba PT 4340 uliojulikana kama Higher Education Students Loans ambao ni mradi wa kutoa Mikopo. Hadi kufikia tarehe 15 Machi ,2016 Bodi ilikuwa imepokea jumla ya shilingi bilioni 245 sawa na asilimia 55.9% tu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge . Fedha hizo zingetolewa zote kwa 100% wanafunzi wengi zaidi wangepata mikopo.
f) Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano: Wizara hii ni miongoni mwa wizara (chache sana) zilizopata fedha zilizopangwa katika bajeti na zaidi, hususan katika sekta ya ujenzi (barabara). Katika mwaka wa fedha 2015/16. Sekta hii ilitengewa shilingi 883,832,338,500/- kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo . Kati ya hizo, fedha za ndani kutoka mfuko mkuu wa hazina wa serikali ni shilingi 191,619,568,500 na shilingi 85,572,770,000 zilikuwa fedha za nje. Kwa upande wa fedha za mfuko wa barabara zilitengwa shilingi 606,640,000,000. Hadi Aprili, 2016 fedha zilizotolewa ni shilingi 1.080,804,942,594. Kati ya fedha hizo shilingi 607,350,007,730 ni fedha za ndani kutoka mfuko mkuu wa hazina/serikali (Ongezeko la shilingi 415,730,439,230) ,shilingi 149,502,934,864 ni fedha za nje na shilingi 323,952,000,000 ni fedha za mfuko wa barabara. Sehemu kubwa ya fedha za ndani zilizotolewa imetumika kulipa madeni ya Makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara.
Mheshimiwa Spika, Licha ya mabilioni yanayotumika kujenga barabara na kulipa madeni yenye riba kubwa sana kutokana na serikali kuchelewa kulipa madeni ya barabara, wakati kamati ikikagua miradi mbali mbali ya barabara nchini imebaini kuwepo kwa changamoto ya kuharibika kwa barabara mapema mara baada ya barabara kujengwa! Licha ya visingizio vilivyotolewa vya uharibifu huo, sababu hizo hazina mashiko /msingi wa kuhalalisha upotevu huo wa mabilioni ya fedha. Barabara zote hizi lazima zifanyiwe ukaguzi wa kitaalam ili kujiridhisha na thamani ya fedha na kazi iliyofanywa. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu sana (tokea kipindi ambacho Rais alikuwa waziri wa miundombinu) Wizara hii imekuwa ikihusishwa na uchakachuaji katika ujenzi wa barabara.
g) Wizara ya Nishati na Madini: Wizara hii nayo ilipata fedha kuliko kiasi kilichotengwa kwenye bajeti.Katika mwaka wa fedha 2015/16. Wizara iliidhinishiwa na Bunge Jumla ya Shilingi bilioni 642.12. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 502.30 sawa na 78% ya bajeti yote ilikuwa kwa miradi ya maendeleo na shlingi 139.82 sawa na 22% zikiwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida .Hata hivyo bajeti iliongezeka kutoka bilioni 642.12 mpaka bilioni 762.12 (Nyongeza ya bilioni 120.12)
Mheshimiwa Spika, Licha ya nyongeza hiyo, miradi ya REA inayogharimiwa na fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini ambao vyanzo vyake vya mapato ni pamoja na tozo ya shilingi 100 katika kila lita ya mafuta ya petrol na Dizeli; na shilingi 150 katika kila lita ya mafuta ya taa bado inasua sua. Hii inatokana na fedha ambazo wananchi wanatozwa katika mafuta tajwa hapo juu kwa makusudi ya kupeleka huduma ya UMEME vijijini kutumika kwa matumizi mengine yasiyokusudiwa! Licha ya fedha hizo kuwa zimewekewa wigo kisheria (Ring Fenced). Takwimu zinaonyesha kwamba tangu tozo hizi zilipoanza kukusanywa Julai 2013 mpaka Machi 2016, fedha zilizopatikana toka kwenye tozo ya petrol na Dizeli ni shilingi bilioni 493.8, Mafuta ya taa shilingi bilioni 448.5 na shilingi bilioni 45.4 kutoka kwenye ‘Custom Processing Fee’. Licha ya makusanyo ya shilingi bilioni 987.7 (tozo ya petrol na dizeli) kiasi kilichopelekwa kwenye umeme vijijini mpaka mwezi April 2016 ni shilingi bilioni 366.95 tu sawa na 37.15% ya makusanyo yote. Katika mazingira kama haya, kamwe serikali ya CCM haiwezi kujitapa imetekeleza wajibu wake kikamilifu. Kwa lugha nyepesi imewaibia mamilioni ya wananchi wanaoishi vijijini ambao mfuko huu uliundwa mahususi kwa ajili ya kusogeza huduma za umeme kwao. Ikumbukwe hii fedha sio ya hisani bali ni fedha ya nyongeza iliyoongezwa kwa kila lita inayonunuliwa na wananchi kwenye mafuta ya taa, petrol au dizeli.
h) Wizara ya Maliasili na Utalii: Katika mwaka wa fedha 2015/16 wizara ya maliasili na utalii iliidhinishiwa jumla ya shilingi 66,313,757,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida . Kati ya fedha hizo shilingi 45,235,955,000 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi mishahara na shilingi 21,077,802,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Mpaka Machi 2016, wizara ilipokea 43,487,894,012.34 sawa na 65.5% ya bajeti iliyoidhinishwa ambapo 32,714,043,166.18 ikiwa ni mishahara na 10,773,850,856 ni kwa matumizi mengineyo. Fedha iliyoidhinishwa kwa miradi ya maendeleo ni 7,709,150,000/= . Fedha zilizotolewa ni bilioni 1 na yenyewe ni fedha ya NJE sawa na asilimia 12.9 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kutokana na hali hiyo katika miradi 10 ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa hakuna hata mradi mmoja uliotekelezwa kwa ufanisi.
i) Wizara ya Viwanda na Biashara: Katika mwaka 2015/16 Wizara ilitengewa jumla ya shilingi 87,470,349,000 ambapo 52,082,968,000 zilikuwa ni matumizi ya kawaida (mishahara na matumizi mengineyo) na shilingi 35,387,381,000/- za matumizi ya maendeleo (shilingi 26,588,200,000 ni fedha za ndani na shilingi 8,799,181,000 ni fedha za nje). Mpaka mwezi Machi 2016 Wizara ilipokea 29,752,487,320/- sawa na 34% ya fedha iliyotengwa. Kati ya fedha hiyo fedha za maendeleo zilizotolewa ni 1,602,111,662 tu ambayo ni fedha za nje! Kwa lugha nyingine fedha za ndani za maendeleo zilizotoka ni 0%, na fedha ya nje iliyotoka ni 18% tu!
j) Wizara ya Fedha na Mipango
Mheshimiwa Spika, Wizara hii, licha umuhimu wake mkubwa katika uchumi wa Tanzania katika mwaka wa fedha 2015/16, pamoja na mafungu yake nane (8) iliidhinishwa kutumia jumla ya shilingi 7,326,769,737,771. Kati ya fedha hizo shilingi 72,659,909,000 kwa ajili ya Mishahara (PE) Shilingi 7,218,508,850,128 kwa ajili ya Matumizi mengineyo (kati ya hizo shilingi 6,381,430,000,000 ni kwa ajili ya deni la Taifa). Kwa upande wa fedha za maendeleo fedha zilizoidhinishwa ni shilingi 1,022,924,905,000 ambapo fedha za ndani zilikuwa shilingi 651,541,992,000/- na fedha za nje 371,382,913,000. Mpaka mwezi machi 2016 wizara ilipokea fedha za maendeleo shilingi 25,908,256,142, sawa na 3% tu ya fedha zote zilizoidhinishwa!
8. MWENENDO WA MAPATO YA NDANI NA MKANGANYIKO WA TAARIFA ZA SERIKALI YA HAPA KAZI TU
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka huu wa fedha, na hususan miezi ya karibuni mwenendo wa mapato umekuwa sio wa kuridhisha sana! Kodi ya ushuru wa forodha haikufikia lengo na kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda hali inazidi kuwa mbaya! Idadi ya meli zilizohudumiwa Januari - Aprili 2015 (TPA- Kontena) zilikuwa 41 ukilinganisha na meli 16 tu zilizohudumiwa Januari- Aprili 2016. Pungufu ya meli 25, badiliko la -61%. Halikadhalika kwa Meli ya Mzigo Mchanganyiko ‘General Cargo’ meli zilizohudumiwa Jan- April 2015 zilikuwa 53 ukilinganisha na meli zilizohudumiwa Jan – April 2016 ambazo ni 33 tu. Pungufu ya meli 20 sawa na badiliko la -37%
Mheshimiwa Spika, Maelezo ya waziri wa fedha na Mipango kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16 kwa kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016 na mwelekeo hadi juni 2016 anaeleza sababu za upungufu kuwa ni ;
i) kupungua kwa uingizaji wa mizigo kutoka nje kutokana na hofu ya wafanya biashara katika kipindi cha uchaguzi
ii) Udanganyifu uliokuwa unafanywa na wafanyabiashara kwa kukwepa kodi ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazopitia bandarini
iii) kushuka kwa bei ya bidhaa katika soko la dunia
iv) Na kwa upande wa kodi ya ongezeko la thamani upungufu umetokana na marejesho ya VAT (VAT inputs) kuwa kubwa kutokana na uwekezaji katika viwanda vya sementi pamoja na kupungua kwa mahitaji.
v) Halikadhalika tatizo la kutoa/kuomba risiti za kielekroniki katika huduma mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Wakati wizara ya fedha ikitoa visingizio tajwa hapo juu, Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania katika maelezo yake ya Takwimu za uingizaji mizigo katika Bandari ya Dar es salaam kwa kipindi cha 2013-2015 na kipindi cha Jan- April 2016 inaeleza sababu zilizopelekea kupungua kwa shehena ya mizigo kuwa ni:
i) Kudorora kwa uchumi wa china (Hii imeleta madhara katika bandari nyingi duniani)
ii) Hofu ya wateja kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya VAT katika huduma zinazotolewa na mawakala kwenye mizigo ya nchi jirani (VAT on Transit GOODS) ambayo ni kinyume na sheria za kimataifa
iii) Tatizo la Single customs Territory. Mizigo inayopatikana kwa mfumo wa single customs territory unatozwa kodi kwa asilimia 100%, baadhi ya wafanyabiashara wanaona kupitisha mizigo Tanzania ni gharama kubwa.
iv) Kushuka kwa bei ya shaba duniani kumesababisha migodi mingi nchini Zambia na DRC kufungwa na hata ile inayofanya kazi uzalishaji umepungua.
v) Tozo la barabara (Road tolls) USD 16 kwa KM 100 hapa Tanzania ulikilinganisha na USD 8 kwa kila KM 100 zinazotozwa kwa nchi nyingine kwa magari yenye ekseli zaidi ya mbili.
vi) Muda mfupi (Short grace period) kwa mzigo wa mafuta wa nchi jirani. Tanzania ni siku 30 mzigo unatakiwa uwe umesafirishwa kabla ya kuwa localised tofauti na nchi nyingine ambazo zinawapa siku 60 hadi 70.
vii) Kuongezeka kwa Tozo kutokana na “Government Chemical Agencies” kutoza USD 1.00 kwa Tani badala ya USD 100 kwa “ Bill of Lading” kwa bidhaa ambazo wanazikagua kama vile mbolea hivyo kuongezeka kutoka wastani wa USD 500 hadi USD 20,000 au Zaidi kutokana na ukubwa wa mzigo.
viii) Mfumo wa TANCIS wa TRA kutoruhusu kugawanywa kwa “Bill of Landing” ili kuruhusu kutoa mizigo ambayo haina tatizo panapokuwa na tatizo la mzigo mmoja badala ya mzigo wote kuzuiwa na kusababisha gharama za tozo za hifadhi kwa mteja ambazo sio lazima.
Mheshimiwa spika, Ni aibu kubwa, kwa vyombo viwili vya serikali kuzungumza lugha tofauti katika suala moja! Hiki ni kiashiria kwamba ama serikali hii haifanyi kazi kama timu…ama waziri wa fedha amedhamiria kulipotosha Bunge kwa kutoa sababu nyepesi huku zile za msingi akiziweka kibindoni (sijui kwa manufaa ya nani). Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Serikali ya CCM na Magufuli kutambua kwamba Tanzania sio kisiwa na kwamba Bandari ya Dar es salaam inakabiliwa na ushindani kutoka kwenye bandari za Mombasa (Kenya), Beira,Nacala na Maputo (Msumbiji) , Durban (Afrika ya Kusini ), Walvis Bay (Namibia) na Lobito (Angola) kama kuna vikwazo vyoyote vinavyoikwamisha bandari yetu na nchi kushindana katika soko la ushindani vikwazo husika lazima vishughulikiwe mara moja. Na wizara ya fedha iliyopewa jukumu kubwa la kusimamia uchumi wa Tanzania haiwezi kukwepa jukumu hili.
9. UNUNUZI WA NDEGE ZA ATCL KUNA HARUFU YA UFISADI!
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kitabu cha fedha za Maendeleo Volume IV Part A fungu 62 kasma 4294 zimetengwa jumla ya shilingi Bilioni 500 fedha za ndani kwa ajili ya kununua ndege za abiria kwa ajili ya shirika la Ndege la ATCL.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya waziri wa ujenzi ,uchukuzi na mawasiliano kifungu cha 185 alisema kuwa, nanukuu ‘kazi inayoendelea ni kukamilisha taratibu za ununuzi wa ndege mbili mwaka 2016.Wizara kwa kushirikiana na ATCL na wadau wengine imekwishaainisha ndege zinazofaa kununuliwa baada ya kukutana na wawakilishi wa viwanda vya ndege vya Boeing ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada. Ndege mbili za awali zinazotarajiwa kununuliwa zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja.Ndege ya tatu na ya nne zitakazonunuliwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 155’
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango ni kwamba; serikali imeamua kununua ndege kutoka kiwanda cha Bombadier ya Canada na hii ni kutokana na ushauri ambao wizara ilipokea kutoka kwa wataalam wake .Aidha tuna taarifa kuwa ndege mbili za mwanzo ambazo zitanunuliwa sio mpya bali ni ndege ambazo tayari zilishatumika (kuukuu) kama taarifa hizi ni za kweli , Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa kwa Bunge hili sababu za kina zilizopelekea serikali kwenda kununua ndege chakavu kinyume cha sheria ya manunuzi ya mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wetu kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tuliamua kutafuta taarifa za kina na za uhakika juu ya Bei za ndege mpya kwenye Viwanda ambavyo serikali ilisema kuwa iliwasiliana nao na kufanya nao mazungumzo yaani Viwanda vya ndege vya Boeing ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada na na kukuta bei za ndege mpya kuwa kama ifuatavyo;
Kiwanda cha Bombardier.
Aina ya Ndege Idadi ya Viti Bei (Januari 2015) Mil USD
Q 400 90 31.3
CRJ 700 70 41.0
CRJ 900 76-90 46.0
CRJ 1000 100 49.0
CS 100 100-133 71.8
CS 300 160 82.0
Kiwanda cha Air Bus
Aina ya Ndege Idadi ya Viti Bei (January 2015) Milioni USD
A 320 100-240 97.0
A 318 74.3
A 340 260-400 284.6
A 350 270-350 351.9
Kiwanda Cha Boeing
Aina ya Ndege Idadi ya Viti Bei (January 2015) Milioni USD
737-700 85-215 80.6
747-8 467 379.1
767-300 ER 181-375 197.1
787-8 250-290 224.6
Mheshimiwa Spika, kwa bei hizo hapo juu Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni tunataka kujua ni kwanini Serikali imeamua kununua ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 78 wakati fedha zilizopitishwa na Bunge hili ni Bilioni 500 ambazo zingetosha kununua ndege mpya kubwa na za kubeba abiria wengi zaidi na hivyo kuwa na ufanisi na hata uwezo mkubwa wa kwenda safari za mbali.Au ndio yaleyale ya kutumia Mawakala ambao wanajiwekea asilimia kama ilivyokuwa huko nyuma katika ununuzi wa ndege ya Rais ?
Aidha kwa mujibu wa waziri wa Fedha alipokuwa anawasilisha mpango wa maendeleo hapa Bungeni alisema kuwa serikali imeamua kununua ndege mbili aina ya Q 400 mbili na CS 300 Moja.
Kutokana na uamuzi huo ni kuwa ndege aina ya Q400 mwaka jana ilikuwa dola milioni 31.3 na ndege aina ya CS 300 ilikuwa dola milioni 82.0
Hivyo basi kimahesabu ni kuwa ndege 2 aina ya Q400 na ndege 1 aina ya CS 300 ni jumla yake itakuwa shilingi Bilioni 318.120 (usd1= 2,200) na hivyo kufanya kiasi cha shilingi Bilioni 181.880 kikisalia .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni kwanini tulitenga kiwango hicho cha fedha (500bilioni) wakati bei halisi za ndege zinajulikana? Hizi fedha zinazosalia baada ya manunuzi ya ndege hizo zitatumika kufanya shughuli gani ? Je kuna Wakala katika ununuzi huu wa ndege ambaye atapata Kamisheni, na kama yupo ni kiasi gani ?
9.1 Hakuna fedha za kuendesha ATCL
Mheshimiwa Spika, pamoja na serikali kutenga fedha kwa ajili ya kununua ndege mbili, jambo la kushangaza ni kuwa hakuna fedha za uendeshaji ambazo zimetengwa na serikali kwa ajili ya shirika letu la ndege ATCL .Hata kwenye mashirika ya serikali ambayo yatapata ruzuku kwa mujibu wa kitabu cha Volume II ‘Public Expenditure’ kifungu 62 kasma 2006 kifungu 270846 ATCL zimetengwa shilingi bilioni 3.221 kwa ajili ya mishahara. Fedha kwa ajili ya uendeshaji ‘other charges’ hakuna hata senti moja iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua baada ya serikali kununua ndege hizo mbili shirika litapata wapi fedha kwa ajili ya undeshaji na hasa ikizingatiwa kuwa shirika mpaka sasa ni mufilisi ? Serikali haikuona umuhimu wa kulipatia shirika hili ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shirika, mtaji wa kuanzia utatoka wapi?
9.2 UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MWL.JK NYERERE PHASE II
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere awamu ya pili uko katika hatihati ya kusimama kutokana na Serikali kutokutii makubaliano ya mikataba ambayo waliingia na Kampuni ya Ujenzi ya BAM International ya Uholanzi. Hii ni baada ya wizara ya fedha kuamua kukiuka masharti ya mkataba baina ya TAA na BAM International kuwa fedha za kutekeleza mradi zitatolewa na HSBC kwa awamu zote mbili yaani phase 1&2 na badala yake wizara ya fedha imeamua kwenda kutafuta Mkopo Mpya nje ya makubaliano ya mkataba baina ya BAM na TAA wa Octoba 2015.
Mheshimiwa Spika, jambo hili la wizara ya fedha kuingilia na kuanza kutafuta mkopo sehemu nyingine nje ya makubaliano ya awali linahatarisha ukamilikaji wa ujenzi wa uwanja huu na hata mkandarasi ametishia kusimamisha ujenzi kama fedha za ziada hazitaongezwa kwa ajili ya mradi huu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni sababu gani zimeipelekea wizara ya fedha kwenda kutafuta mkopo mwingine kutoka taasisi nyingine nje ya makubaliano ya awali ya kimkataba? Nani ananufaika na utaratibu huu wa kutafuta mkopo mpya badala ya kukamilisha taratibu zilizokuwepo? Je, Kitendo cha kuanza kutafuta mkopo upya kitachelewesha ukamilikaji wa mradi huu kwa kiwango gani? Nani atalipia hasara itokanayo na kuchelewa kutekelezwa kwa mradi huu?
9.3 UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHATO
Mheshimiwa Spika, ukisoma Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika eneo la usafiri wa Anga moja ya kipaumbele cha mpango katika uk.76 sehemu (x) ni ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Chato. Mradi huu unahusisha ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege Chato kwa ajili ya huduma za usafiri wa anga kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 mpango wa maendeleo umetenga kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuanza kufanyika kwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua kama paliwahi kufanyika kwa utafiti wa kina na majibu ya utafiti huo kuonyesha kuwa ujenzi wa kiwanja cha ndege Chato ndio kipaumbele cha taifa kwa sasa na kuwa mradi huu umelenga malengo mapana ya taifa ya kukuza uchumi wa taifa letu. Kwanini fedha hizi zisingeongezwa kwenye kuimarisha viwanja vilivyopo kwa sasa na hasa ikitiliwa maanani kuwa serikali ndio kwanza inawaza kununua ndege tatu kwa shirika letu la Ndege.
10 .PRESIDENTIAL DELIVERY BUREAU-BRN
Mheshimiwa Spika, kitengo hiki ambacho kilianzishwa kwa mbwembwe nyingi na serikali ya awamu ya nne na hata Bunge hili kushawishiwa kuwa ndio njia pekee ya kuongeza ufanisi serikalini chini ya kauli mbiu ya Matokeo Makubwa Sasa! kimeshindwa kabisa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Itakumbukwa kuwa wakati kitengo hiki kinaanzishwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tulipinga uanzishwaji wa kitengo hiki kwani kilikuwa ni kwa ajili ya ulaji tu.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha wameamua kimya kimya kukivunja kitengo hiki kwa kutotenga hata senti moja kwa ajili ya mishahara na marupurupu mengine kwa ajili ya wafanyakazi wa Kitengo hiki (VOTE 6) na badala yake zimetengwa kiasi cha shilingi 397,278,000 kwa ajili ya kulipia kodi ya pango , (kasma 220700-rental expenses ).
Aidha, ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha 2015/2016 kifungu hiki kilitengewa kiasi cha shilingi 602,800,000 kwa ajili ya kodi hiyo hiyo.
Mheshimiwa Spika, ukisoma katika kitabu cha Maendeleo - Volume IV utaona kuwa fungu 06 President’s Delivery Bureau zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 27,218,829,000 ambazo zote ni fedha kutoka nje (DFID & UNDP) na maelezo yake ni kuwa ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matokeo makubwa sasa ambayo kimsingi haijaainishwa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata maelezo ya kina juu ya mambo yafuatayo;
i. Waliokuwa watumishi wa kitengo hiki wamehamishwa, wamefukuzwa au wamesimamishwa kazi? Mbona hakuna fedha za mishahara na marupurupu mengine kwa kitengo hiki?
ii. Ni sababu zipi zimepelekea kitengo hiki kutokupatiwa fedha za uendeshaji mwaka huu wa fedha?
iii. Ni nani ataenda kusimamia fedha za Maendeleo takribani bilioni 27 ambazo zimetengwa kama kitengo hakina wafanyakazi? Au ndio kusema kwamba DFID &UNDP itakuwa ikisimamia fedha zake moja kwa moja?
iv. Tangu kuanzishwa kwa kitengo hiki kimetumia kiasi gani cha fedha na ufanisi wake umekuwa upi?
v. Fedha za malipo ya pango/kodi ni kwanini mwaka huu imepungua kwa zaidi ya aslimia 48 kulinganisha na ya mwaka jana? Nani watakaa kwenye jengo hilo wakati hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya mishahara yao?
11 . MILLENIUM CHALLENGE CORPORATION (MCC)
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya Wizara ya Fedha na Mipango kifungu 1007 katika mwaka wa fedha 2016/17 idara wameomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 500 kama bajeti yake ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 60 (kasma 210300) zinaombwa kwa ajili ya kuwalipa posho ya majukumu kwa watumishi 12 wa MCA-T Compact II watakaofanya kazi ya uchambuzi wa miradi inayohitaji ufadhili wa MCC. Aidha kiasi cha shilingi milioni 280 (kasma 220700) ni kwa ajili ya kulipia pango la ofisi.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa Bodi ya wakurugenzi ya MCC mnamo tarehe 28,Machi 2016 ilisimamisha kutoa fedha kwa Tanzania katika mradi wa MCA-T Compact II zaidi ya shilingi trilioni moja (USD. 472,824,825) ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya umeme nchini kutokana na serikali hii ya CCM kupitisha sheria mbaya na kandamizi ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crime Act), Sheria ya Taifa ya Takwimu na kuminywa kwa Demokrasia Nchini hasa kufutwa kwa matokeo halali ya Uchaguzi wa Zanzibar ya Octoba 25,2016.
Mheshimiwa Spika, baada ya Marekani kusimamisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huu, bodi ya wakurugenzi ya MCC ilimuandikia rasmi barua Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mhe.John Magufuli tarehe 31 Machi,2016 na kumjulisha rasmi juu ya uamuzi wake .Pamoja na Rais kujulishwa kwa barua Kambi rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa mpaka tarehe 11/05/2016 barua hiyo ya Bodi ya MCC ilikuwa haijapatiwa majibu na Ikulu .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupatiwa majibu ya kina juu ya mambo yafuatayo;
i. Ni kwanini serikali inaomba fedha kwa ajili ya kulipa watumishi ambao watachambua miradi ya MCC ambayo haipo?
ii. Ni lini serikali itaijibu barua ya bodi ya MCC? Kwanini imechukua muda mrefu kiasi hicho kutoa majibu kwa barua yao? Hasa ikizingatiwa kuwa katikati ya mwezi Juni Bodi ya MCC itakaa pamoja na mambo mengine itatoa uamuzi wa mwisho juu ya jambo hili.
iii. Hivi kulipia kiasi cha shilingi milioni 280 cha kodi ya ofisi kwa mwaka ambayo ina watumishi 12 ni kiwango sahihi? Kinaendana na dhana ya kubana matumizi?
12 . WATUMISHI HEWA SERIKALINI
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 01 Mei, 2016 wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mei mosi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Magufuli alilitangazia taifa kuwa jumla ya watumishi hewa walikuwa wamefikia 10,295 na alisema kuwa kati ya watumishi hao hewa 8,373 wanatoka TAMISEMI na watumishi 1,922 wanatoka Serikali Kuu. Aidha, aliendelea kusema kuwa watumishi hao hewa walikuwa wakiligharimu taifa shilingi Bilioni 11.6 kwa mwezi sawa na shilingi Bilioni 139 kwa mwaka na kwa miaka 5 ni shilingi Bilioni 695.
Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi sana kwa nchi maskini kama hii ya kwetu kupotea kwa sababu tu ya uzembe na kukosekana kwa usimamizi ulio makini na dhabiti katika kusimamia rasilimali za taifa letu.Jambo hili halikubaliki hata kidogo katika ulimwengu wa sasa na teknolojia ilikofikia ya watumishi kupokea mishahara kupitia Benki.
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, kupitia hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa umma; ilitoa suluhisho la kuweza kushughulikia ufisadi huu wa watumishi hewa ambao unalelewa na mfumo.
Aidha, leo tunataka kujua hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya Maafisa maduhuli, wakuu wa idara na vitengo pamoja na wahasibu ambao ndio wanaondaa na kupitisha orodha ya watumishi ambao wanastahili kulipwa kila mwezi ‘pay roll’. Hawa ndio wanaoandaa orodha, mbona mpaka leo bado wapo kazini?
13 . WIZARA YA FEDHA, BENKI YA STANBIC NA SAKATA LA MKOPO WA DOLA MILIONI 600-UTAKATISHAJI FEDHA HARAMU
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13 serikali ya Tanzania iliomba mkopo wa dola millioni 600 kwa malengo ya kugharamia mpango wa Taifa wa miaka mitano. Mkopo huu uluzihusisha benki zenye mahusiano ya kibiashara stanbic (Tanzania) na Standard Bank PLC (kwa sasa inafahamika kama ICBC Standard Bank PLC) (Standard Bank) ya Uingereza. Standard Bank ilihusishwa kutokana na ukweli kwamba aina ya mkopo ambao serikali ilikuwa inautaka Benki ya Stanbic Tanzania ilikuwa haitoi hiyo huduma ya aina hiyo.
Mheshimiwa Spika, Inasemekana kwamba mchakato huo ulihusisha udanganyifu wa ada ya mkopo, taarifa zinaonyesha kwamba ada halali iliyotakiwa kulipwa ni 1.4 % ya mkopo wote, hata hivyo ada iliyokuja kulipwa ni 2.4% ya mkopo wote. Kutokana na udanganyifu huo, kuna kesi inayoendelea mahakamani ikiwahusisha aliyekuwa kamishna Mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania, ndugu Harry Kitilya (na mwenyekiti wa bodi ya EGMA, inayohusishwa katika sakata hili), aliyekuwa Mkuu wa idara ya ushirikiano na uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare pamo
ja na aliyekuwa mwanasheria Benki ya Stanbic Tanzania, Bwana Sioi Solomon SUMARI.
Mheshimiwa Spika, Sio dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani kujadili wahusika tajwa hapo juu kwa kuwa tunatambua, kanuni zetu za Bunge zinatuzuia kujadili suala ambalo liko Mahakamani, lakini kwa kuwa leo ni siku ya kujadili Bajeti ya Serikali ni wajibu wetu kama kambi kuhoji nini kilichopelekea udanganyifu huo na kwa kiwango gani Serikali hii ilitekeleza wajibu wake kikamilifu ili kuepusha makosa kama hayo kujirudia hasa ukizingatia kwamba katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/17, serikali inatarajia kukopa mikopo ya kibiashara ya aina hii ili kufidia ombwe la bajeti yenye thamani ya shilingi trillion 7.4. Na wahusika wakuu katika mchakato mzima ndio hao wahusika!
Mheshimiwa Spika, Sio dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani kujadili wahusika tajwa hapo juu kwa kuwa tunatambua, kanuni zetu za Bunge zinatuzuia kujadili suala ambalo liko Mahakamani, lakini kwa kuwa leo ni siku ya kujadili Bajeti ya Serikali ni wajibu wetu kama kambi kuhoji nini kilichopelekea udanganyifu huo na kwa kiwango gani Serikali hii ilitekeleza wajibu wake kikamilifu ili kuepusha makosa kama hayo kujirudia hasa ukizingatia kwamba katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/17, serikali inatarajia kukopa mikopo ya kibiashara ya aina hii ili kufidia ombwe la bajeti yenye thamani ya shilingi trillion 7.4. Na wahusika wakuu katika mchakato mzima ndio hao wahusika!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inazo nyaraka mbali mbali, moja wapo ikiwa ni barua toka TAKUKURU (TAASISI YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA) kwenda kwa mwanasheria mkuu wa serikali, Mhe. George M. Masaju yenye kumbukumbu namba CACE255/362/01/104 ya tarehe 20/01/2016. Barua husika imeambatanishwa na barua kwenda kwa Kitengo cha kimataifa cha makosa ya jinai (International Criminal Unit) kikiomba msaada wa uchunguzi wa wahusika katika sakata husika, huku ikirejea vifungu vya sheria vilivyovunjwa!
Mheshimiwa Spika, Barua husika ina ainisha mambo yafuatayo:
1. Imewataja majina ya watu wanaochunguzwa kwa kukiuka:
a) vifungu 22,23,31,32 na 34(1)sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa (The Prevention and Combating of Corruption Act 2007.
b) Vifungu 333, 335 na 337 vya sheria ya kanuni za adhabu (The Penal Code (Cap 16 R.E 2002).
c) Vifungu 12,13 vya sheria ya kuzuia utakatishani wa fedha haramu ( Anti- Money Laundering 2006 (R.E 2012)
Watuhumiwa wakiwa Stanbic Bank, Harry Msamire Kitilya (Aliyekuwa Kamishna Mkuu TRA), Peter Anandi Nyabuti, Bashir Awale, Shose Sinare, Sioi Solomon Sumari, Dr Servacius Likwelile (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha), Alfred Paul Misana, Bedason Shalanda, Ramadhan Kijjah na Ngosha Said Magonya
2. Mpaka mwezi Februari 2012 makubaliano ya ada ya mkopo kwa benki zote mbili ( Standard na Stanbic ) ilikuwa 1.4% ya Mkopo wote
3. Mchakato ulisuasua sana /ulikwama mpaka mwezi septemba 2012 pale ambapo Stanbic ‘iliongeza’ ada mpaka 2.4% .
4. Nyongeza hiyo ya 1% angelipwa ‘local partner’ na kwamba mgao huo ulikuwa na malengo ya kumshawishi ndugu Harry Kitilya na pengine ‘maafisa wengine wa serikali ya Tanzania’ili wawape upendeleo wa kuchukua mkopo toka benki tajwa hapo juu.
5. Mara tu baada ya nyongeza ya 1%, mchakato ulikwenda kwa kasi ya ajabu. Mwezi Novemba 2012 barua ya ‘mandate and fee’ ilisainiwa kati ya standard bank, Stanbic Bank na Wizara ya fedha .
6. Makubaliano husika hayakuelezea chochote kuhusiana na ‘local patner’ au ‘mtu wa tatu’ zaidi ya kuainisha ada ya ujumla ya 2.4% iliyoogezwa kiaina toka 1.4%
7. Pamoja na yote, utaratibu uliopangwa na pande zote tatu (Stanbic/Standard na wizara ya fedha)uliruhusu fedha ya UMMA (MKOPO wa kibiashara) kuingizwa kwenye akaunti binafsi ya ‘local partner’ badala ya fedha husika kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Serikali ya Tanzania.
8. Pamoja na kwamba kulikuwa na viashiria vyote vya hatari ya rushwa na udanganyifu,hakuna afisa yeyote ya serikali (wizara ya fedha) ,wala timu ya benki ya standard bank aliyeonekana kujali,wala kuhoji chochote na wala hawakutaka kuchunguza au kuhoji uhalali wa huyo ‘third party’ au ‘local partner’ ambaye sio sehemu ya mkataba /makubaliano kuingiziwa 1% ya fedha ya Mkopo
9. Baada ya fedha husika kuingizwa kwenye akaunti ya ‘Local Partner’ mwezi Machi 2013. Kiasi kikubwa cha fedha kilianza kuondolewa haraka haraka na ndugu Fratern Mboya. Ikumbukwe akaunti hii ilifunguliwa mahsusi mwezi mmoja kabla (February 2013)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iliambie Bunge hili tukufu;
i) Ni vigezo gani vilivyotumika kuwachuja watuhumiwa kutoka 11 mpaka 3?
ii) Ni kwa vigezo gani wizara ya fedha iliruhusu fedha za Umma kuingia katika akaunti binafsi huku ikifahamu (kama ilivyoainishwa kwenye barua) anayeingiziwa fedha hajatajwa/hayuko kwenye mkataba baina ya serikali na benki tajwa hapo juu?
iii) Ni kwa kiwango gani wizara ya fedha inadhani, ilitekeleza wajibu wake ipasavyo katika mchakato mzima? Kama ndio kwa nini? Kama sio ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya maafisa wa serikali (Wizara ya Fedha) waliopewa dhamana kusimamia mchakato mzima?
iv) Barua ya TAKUKURU inamtaja bwana Franten Mboya kuhusika na utoaji wa mabulungutu ya fedha kwa kipindi cha siku 10 mfululizo, na kiasi kilichobaki kuhamishiwa kwenye akaunti nyingine ya ‘local partner’. Japokuwa Kambi Rasmi haijui hayo ‘mabulungutu’ yalienda kwa nani?. Kwa nini ndugu huyu sio miongoni mwa washtakiwa? Kwa nini wameshtakiwa watatu tu?
v) Ni kwa nini mpaka sasa Dr. Servacus Likwelile , Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na ndugu Paul Misana kamishna wa wizara ya fedha hawajafunguliwa mashtaka na wanaendelea kuitumikia serikali hii inayojinasibu kwa kutumbua majipu? Mbona hii sheria sio msumeno tena? Inang’ata upande mmoja tu?
13.2 Uwezo Mdogo wa Benki Kuu Kufanya Ujasusi wa Miamala ya Fedha na Kuchukua Hatua Stahiki
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatilia mashaka uwezo na dhamira ya kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) cha Benki Kuu kufanya ujasusi wa Miamala ya fedha katika kuzuia utakatishaji wa fedha haramu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kina mamlaka ya kiutawala pekee na huishia kufanya uchambuzi wa taarifa za miamala ya fedha na kuziwasilisha ama Jeshi la Polisi au PCCB, wakati huo huo PCCB inalazimika kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili atoe ruhusa ya kufungua mashitaka.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kuwa FIU haina uwezo wa kufanya uchunguzi, wala kuendesha mashitaka dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu jambo ambalo ni mwanya unaotumiwa na watu waovu na mafisadi kama ilivyokuwa katika wizi wa Mabilioni ya Rada, wizi wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na wizi wa fedha katika Mkopo wa Serikali dola milioni 600 kutoka Stanbic Bank.
Mheshimiwa Spika, mahakama ya mafisadi inayokusudiwa kuanzishwa na Serikali haitaweza kufanya kazi kwa ufanisi kama mifumo iliyopo yenye mianya ya kifisadi haitazibwa. Mfumo wa FIU ya Tanzania ni “administrative model” wakati mfumo imara zaidi ni ule wa “Judicial Model” ambao unakiongezea nguvu kitengo hicho cha kuzuia miamala ya biashara haramu za kutakatisha fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa “Egmont Group of Financial Intelligence Units” Judicial Model of FIU inamaanisha kuwa
“The Judicial Model is established within the judicial branch of government wherein “disclosures” of suspicious financial activity are received by the investigative agencies of a country from its financial sector such that the judiciary powers can be brought into play e.g. seizing funds, freezing accounts, conducting interrogations, detaining people, conducting searches, etc.”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuimarisha kitengo cha FIU kwa kukiundia Mfumo wa Judicial Model ili kuepuka aibu ambayo Taifa letu limekuwa likiipata kutokana na Serious Fraud Office ya Uingereza kuwana na uwezo wa kurudisha fedha za zilizoibiwa kwa njia ya kifisadi wakati kazi kama hiyo ingeweza kufanywa na vyombo vya hapa nchini endapo vingeimarishwa kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inavyoshauri.
14 MADENI AMBAYO SERIKALI INADAIWA NA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina mifuko sita ya hifadhi ya jamii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa lakini pia maendeleo ya kiuchumi ya wanachama wake. Mifuko hii ni Parastatals Pensions Fund (PPF), Public Service Pension Fund (PSPF), Local Authorities Pension Fund (LAPF) National Social Security Pension Fund (NSSF), National Health Insurance Fund (NHIF) na Government Employees Pension Fund (GEPF).
Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango mkubwa wa mifuko hii ya jamii katika uchumi wa taifa na maendeleo ya kiuchumi ya wananchama wake; mifuko hii imeathiriwa vibaya na mikopo isiyo na tija (non- performing loans) inayotoa kwa Serikali na taasisi zake. Mifuko hii iko katika hatari ya kufilisika kutokana na mikopo hiyo kukosa dhamana (guarantee) au mikataba rasmi na Serikali jambo linalopelekea uwezekano wa fedha hizo zilizokopeshwa kwa Serikali na taasisi zake kupotea au kurejeshwa kwa kasi ndogo sana na hivyo kukosa tija.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 madeni ya Serikali kutoka katika hifadhi za jamii yamekuwa yakiongezeka huku kukiwa na kasi ndogo sana ya urejeshaji wa mikopo hiyo na wakati mwingine hakuna kabisa urejeshaji unaofanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, mpaka kufikia tarehe 30 Juni, 2014, deni la Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia takriban shilingi trilioni 1. 69 ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha takriban shilingi bilioni 975 kilikuwa kimeiva tayari kulipwa katika mifuko hiyo ya hifadhi lakini Serikali haikulipa.
Jedwali Na.1. Mchanganuo wa madeni ya Serikali katika kila mfuko wa hifadhi ya jamii, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2014
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII JUMLA YA DENI (Tshs) KIASI KILICHOIVA TAYARI KULIPWA (Tshs)
LAPF 173,231,417,845.00 94,655,371,891.00
PSPF 460,995,168,878.82 251,942,767,372.27
PPF 221,070,451,951.77 27,252,909,658.32
NHIF 105,792,983,055.76 26,325,247,799.96
NSSF 722,460,946,894.36 575,048,756,582.94
GEPF 14,333,964,512.22 0
JUMLA 1,697,884,933,137.93 975,048,756,582.94
CHANZO: Ripoti ya CAG ya 2013/14
Mheshimiwa Spika, kufuatia malimbikizo ya madeni ya Serikali katika mifuko ya hifadhi za jamii, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliitisha kikao cha baina ya Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii tarehe 24 Oktoba, 2014 ili kupata maelezo ya Serikali kuhusu ulipaji wa madeni hayo. Katika kikao hicho, ilibainika kwamba kulikuwa na tofauti ya kiwango cha deni la mkopo katika taarifa ya Serikali na ile ya mifuko ya hifadhi za jamii. Kutokana na hali hiyo, kiliundwa kikosi kazi cha kilichojumuisha wadau kutoka Serikalini, taasisi za Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii ili kufanya uchunguzi kujua kiwango halisi cha deni ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa Spika, CAG anaeleza kwamba ripoti ya kikosi kazi hicho kilichoundwa ili kubaini deni halisi Serikali inayodaiwa na mifuko ya jamii ilionyesha kwamba hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2014 jumla ya deni halisi ambalo Serikali ilikuwa inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ni takriban shilingi trilioni 1.875, ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 937.865 kilikuwa kimeiva tayari kulipwa lakini Serikali ilikuwa haijalipa fedha hizo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. Hata hivyo, hadi kufikia tarehe 7 Machi, 2015 Serikali ilikuwa haijalipa kiasi hicho kilichoiva kwa mifuko ya hifadhi za jamii.
Jedwali Na. 2 Mchanganuo wa madeni ya Serikali katika kila mfuko wa hifadhi ya jamii yaliyofanyiwa uhakiki na kikosi kazi hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2014.
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII JUMLA YA DENI HALISI KIASI KILICHOIVA TAYARI KULIPWA
LAPF 173,231,417,845.00 94,655,371,891.00
PSPF 478,564,986,495.99 273,422,154,530.03
PPF 275,682,357,071.87 53,269,846,358.40
NHIF 106,576,578,959.00 27,651,457,652.66
NSSF 827,506,941,339.53 488,866,404,953.71
GEPF 14,333,964,512.22 0
JUMLA 1,875,896,246,224.49 937,865,235,385.80
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, deni hili la trilioni 1.875 ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii, halijumuishi deni la shilingi trilioni 7.066 ambalo PSPF inaidai Serikali kutokana na kuwahamishia wananchama waliokuwa chini ya mifuko ya pensheni kwenda PSPF ambao makato yao hayakuwa kwenye mfuko wa PSPF lakini Serikali ikaamuru walipwe penshini jambo ambalo ni kinyume na sheria ya mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa Spika, ikiwa deni hili la shilingi trilioni 7 litajumlishwa na lile la awali, Serikali sasa itakuwa inadaiwa na mifuko ya jamii Jumla ya shilingi 8,942,426,246,224.49 (trilioni 8.942), na hii ni mbali na madeni mengine ambayo Serikali inadaiwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Seirkali kutoa maelezo mbele ya bunge hili, ni kwa nini hailipi madeni (tena yaliyoiva tayari kulipwa) kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
15 KODI KATIKA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI- PAYE
Mheshimiwa Spika, wakati Rais Magufuli akilihutubia Taifa wakati wa sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani alizungumzia suala la makato ya mishahara ya wafanyakazi (PAYE). Na kwa mamlaka aliyonayo kama Mkuu wa Nchi aliasema kuwa amepunguza makato hayo ya PAYE kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9, na kuagiza kuwa suala hilo lianze kufanyiwa kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017 .
Mheshimiwa Spika, kodi hii ya mshahara imekuwa ni kilio kikuu kwa wafanyakazi na ni ukweli ulio wazi kuwa kundi hili la wafanyakazi ndilo linalolipa kodi kubwa kuliko makundi mengine katika jamii yetu. Busara iliyotumiwa na Mhe. Rais Magufuli kupunguza Kodi hii ya PAYE kwa ngazi ya chini iliyokuwa inalipa asilimia 11 na kuwa asilimia 9 kwa wale wote ambao wanapokea mshahara wa kati ya shilingi 170,000 na 360,000/-, na kiwango kitakachokatwa hiyo asilimia 9 ni shilingi 190,000/- ambayo ni tofauti kati ya (360,000-170,000). Kwa wale ambao mshahara wao ni shilingi 540,000/-, PAYE itakuwa 17,100 + 20% ya tofauti kati ya silingi 540,000- na 360,000/- ambayo ni shilingi 36,000/-, hii inafanya mshahara huo kukatwa shilingi 53,100/-. Na kwa wale wanaopokea Mshahara wa shilingi 720,000/- kwa mwezi kodi ya PAYE ni shilingi 53,100 + 25% ya tofauti kati ya shilingi 540,000/- na 720,000/- ambayo ni shilingi 45,000/-, hivyo kufanya PAYE kwa mshahara wa shilingi 720,000/ kuwa shillingi 98,100/-.
Mheshimiwa Spika, na kwa wale wote wanaopokea zaidi ya shilingi 720,000/- kwa mwezi kodi ya Mshahara ni sawa na Tsh 98,100 +30% ya tofauti ya shilingi 720,000/- na kiwango cha juu cha mshahara. Mathalani kwa mtu anayepokea mshahara wa shilingi 2,500,000/- kwa mwezi, PAYE ni sawa na Tshs 98,100+ 30% ya 1,780,000/- (534,000) na hivyo makato ya PAYE kuwa shilingi 632,100/-
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri lengo la Mheshimiwa Rais lilikuwa zuri la kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi wa umma, lakini inawezekana kabisa Mheshimiwa Rais bado hajaelewa utaratibu mzima wa makato, kwani ingekuwa ni bora kama punguzo la asilimia 2 lingekwenda sambamba kwa kila ngazi ya mshahara (yaani punguzo la 2% kwa 20%, 25% na 30%) kwa kulingana na utaratibu wa makato kama ulivyowekwa na TRA.
Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwamba Serikali itoe punguzo la 2% kwa ngazi zote za mshahara kama ambavyo Rais Magufuli alivyokuwa amedhamiria, kinyume na hapo punguzo hilo la PAYE kutoka asilimia 11 hadi 9 itakuwa ni kiini macho kwa wafanyakazi.
Na hii ni kutokana na ukweli kuwa wafanyakazi hawa bado wana mzigo mkubwa sana wa kodi katika kupata huduma mbalimbali ambazo ni mahitaji muhimu katika maisha yao ya kila siku kama vile VAT, na kodi nyinginezo , hivyo kuwapunguzia makato ya kodi katika mishahara yao itawawezesha kuwa na kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku.
16 UPOTEVU MKUBWA WA MAPATO ITOKANAYO NA MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi imekuwa ikilikosesha taifa fedha nyingi. Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikishauri kila mara katika mapendekezo ya hotuba ya bajeti kuwa misamaha ya kodi angalau isizidi asilimia 1ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia (Opening the gate 2012) Tanzania ilikuwa ikipoteza takribani trillioni 2.9 kwa upotevu holela wa kodi bandarini peke yake. Mwaka 2013/2014 misamaha ya kodi iliongezeka kutoka 1.4 trilioni mpaka 1.8 trilioni. Mwaka 2014/2015 serikali ilitoa misamaha ya takribani shilingi bilioni 1,627 sawa na 2% ya GDP.
Mheshimiwa Spika, kwa takribani miaka mitano sasa serikali haijaweza kufikia lengo la kupunguza kudhibiti misamaha ya kodi angalau isiyozidi 1%ya GDP. Hii ni kutokana na uzembe mkubwa wa serikali katika kukusanya kodi, sera mbovu za ukusanyaji wa mapato, udhaifu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya kodi, vitendo vya rushwa kubwa na zile ndogo ndogo zinazotokana na uswahiba wa karibu na baadhi ya viongozi wasio waaminifu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na misamaha ya kodi baadhi ya makampuni ya madini yenye mikataba maalumu yameruhusiwa kuwekeza nje mauzo yake yote kinyume na utaratibu wa kampuni nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo yao. Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la April 29, 2016, makampuni hayo yenye mikataba maalum yameruhusiwa kuwekeza mauzo yake nje ya nchi (illicit financial flows) ambapo jambo hilo limerasimishwa katika sheria ya madini ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika, Jambo hili linaisababisha hasara kubwa serikali, ikiwa ni pamoja na mapato yatokanayo na kodi zinazopotea tu kiholela. Ni wazi sasa serikali iko katika wakati mgumu kifedha na maisha ya wananchi yanazidi kuwa magumu kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali ikiwemo sukari, mafuta ya magari, vyakula n.k Hivyo ni aibu kwa serikali kuendelea kulegeza, au kutojali kabisa hasara kubwa inayotokana na misamaha ya kodi, mianya ya udhibiti wa makusanyo ya kodi, mikataba na sera mbovu ambazo hazinufaishi taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo juu ya maswali yafuatayo:
i. Je, ni kampuni zipi na ngapi zenye ruhusa ya kuwekeza mapato yake yote nje ya nchi?
ii. Je, serikali imefanya tathimini kuwa tunapoteza kiasi gani cha fedha za kigeni yaani (foreign reserves) kutokana na mikataba ya namna hii?
17. MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA-UKUSANYAJI KODI
Mheshimiwa Spika, Ili kuijengea uwezo TRA kutokana na uwezo mdogo wa kukusanya mapato kulingana na vyanzo vilivyopo na uwepo wa mianya mingi ya ukwepaji kodi na kushindwa kusimamia sera za misamaha ya kodi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Serikali iridhie mpango wa kufanya mapitio makubwa ya Mfumo Mzima wa Ukusanyaji wa kodi nchini (Robust and Comprehensive Tax Regime Review) ili kuusuka upya kwa kuondoa na kuziba kabisa mianya yote ya upotevu mkubwa wa mapato uliosababishwa na uzembe wa Serikali kuisimamia TRA katika ukusanyaji wa Mapato.
18. KIZUNGUMKUTI CHA MABILIONI YA JK
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa toka serikali ya awamu ya nne iwepo madarakani uliimbwa wimbo maarufu wa mabilioni ya Kikwete au JK ambayo yalitolewa na serikali wakati huo ikiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia hoja mbalimbali za wabunge na maswali yao hapa Bungeni walizungumzia na kuhoji utaratibu wa mgawanyo wa mabilioni hayo na serikali haikuwahi kuweka wazi utaratibu mgawanyo huo zaidi ya kutoa majibu ya kisiasa kuliko uhalisia wa jambo husika.
Mheshimiwa Spika, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka (Viti Maalum) katika Mkutano huu wa Bajeti Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mheshimiwa Abdalah Possi alieleza Bunge hili kuwa kiasi cha shilingi bilioni 50.6 kilitolewa kama mikopo kwa ajili ya mabilioni ya Kikwete lakini ni kiasi cha bilioni 41.53 ndicho kilichorudishwa na wakopaji. Hii inamaanisha kuwa takribani bilioni 9 hazikuweza kurudishwa na walionufaika na mabilioni hayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuhoja masuala yafuatayo; mosi, ni kwa nini fedha hazikurudishwa zote? Kwa sasa fedha hizo zilizorudishwa zipo wapi na zinafanya kazi gani? Je serikali imechukua hatua gani kwa fedha ambazo hazijarudishwa? Na je ni utaratibu gani uliotumika kugawanywa fedha hizo na kwa vigezo gani?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kuwa pamoja na majibu ya maswali yaliyoulizwa kuhusu mabilioni haya imwagize Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za serikali kufanya uchunguzi maalum juu ya fedha hizi na kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC) na taarifa ya Kamati kujadiliwa katika Bunge hili.
19 MIKATABA MIBOVU SEKTA YA MADINI NA NISHATI INALIKOSESHA TAIFA MAPATO
Mheshimiwa Spika, kutokana na serikali kuendelea kuingia mikataba mibovu na ambayo haina maslahi kwa taifa na kuifanya mikataba kuwa ni siri hata kwa Bunge letu tumeendelea kupata hasara kama taifa kutokana na ukweli kuwa mikataba imekuwa mibovu na ambayo inawanufaisha zaidi wawekezaji kuliko taifa .
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kitabu cha mapato volume I kinaonyesha kuwa Gesi italiingizia taifa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi Bilioni 115.127 (kwa mujibu wa kifungu 140274 - sale of Gas).
Aidha sekta ya Madini inategemewa kuliingizia Taifa kiasi cha shilingi Bilioni 180.803 ambazo ni fedha zitakazotokana na mrabaha wa madini (kifungu cha 140353 --Mineral Royalities) na kiasi cha shilingi Bilioni 29.494 ni kodi mbalimbali kutoka sekta ya Madini (kifungu 140101 –mineral Rent)
Mheshimiwa Spika, serikali mara zote imekuwa ikijitapa hapa Bungeni na huko nje kwa wananchi kuwa sasa uchumi wa gesi unaenda kutuondoa katika umasikini kumbe ni hadaa na hali hii haikubaliki kila mwaka kuendesha serikali kwa fedha za pombe na sigara ambazo ni nyingi kuliko fedha za sekta ya nishati na madini –kwa mfano mapato ya VAT kutokana na sigara na bia ni shilingi bilioni 263.940 mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye bia, sigara na vinywaji vikali ni kiasi cha shilingi Bilioni 544.112 (kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato volume 1)
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , tunaitaka serikali kuiwasilisha mikataba yote ya sekta ya Nishati na Madini hapa Bungeni ili Bunge liweze kuipitia na kuchukua hatua za kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba, na hii ndio itakuwa njia sahihi ya kuliokoa taifa na upotevu huu wa mapato.Aidha tunamtaka waziri aeleze huu uchumi wa gesi ambao unasemwa kila mara uko wapi ?
20. UUZWAJI WA HISA ZA TBL
Mheshimiwa Spika, Msajili mkuu hazina Lawrance Mafulu alinukuliwa wakati serikali ikipitisha bajeti ya mwaka 2015-2016 kuwa moja ya vyanzo vya mapato ni kodi na mapato yasiyo ya kodi ambayo yanapatikana na shughuli za kibiashara ambazo hufanywa na mashirika ya umma ambayo huleta faida katika mfuko wa serikali kwa njia ya gawio.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa inamiliki hisa milioni 11.7 katika Kampuni ya bia ya Tanzania, lakini kwa utaratibu ambao haukueleweka Serikali mwishoni mwa mwaka jana iliuza hisa hizo kwa thamani ya shilingi 15,200/- kwa kila hisa na hivyo kufanya jumla ya mauzo kuwa shilingi bilioni 177.84
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inalazimika kukubali na kutaka maelezo ya mauzo hayo, kutokana na ukweli kuwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 Serikali kutokana na hisa hizo ilipata gawio la jumla ya shilingi 5,700,000,000/- na kwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 kitabu cha mapato VOLUME I Kampuni ya Bia inatoa gawio la shilingi 1,000/- tu. Hoja ni kuwa inawezekanaje gawio liporomoke kutoka shilingi Bilioni 5.7 mwaka jana hadi shilingi 1,000 mwaka huu?
Mheshimiwa Spika, taarifa ya kamati ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara ya Fedha na Mipango uk.21 inaonesha kuwa mauzo ya hisa asilimia 4 za Kampuni ya Bia na asilimia 2.5 za Kampuni ya sigara zingeuzwa kwa shilingi bilioni 200. Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa makusanyo hadi februari, 2016 zilikuwa ni shilingi 344,470,000,000/- Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kupata maelezo ni kwa nini fedha hizi hazikuwa zimeoneshwa kwenye makisio ya makusanyo kwenye kitabu cha JUZUU ya I uk. 10 hadi 13?
21. KUFUTWA KWA MISAMAHA YA KODI KWA MAJESHI YETU
Mheshimiwa Spika , wakati waziri wa Fedha akiwasilisha hotuba ya Bajeti alisema kuwa moja ya hatua ambazo serikali inachukua ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali ni pamoja na kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na badala yake alipendekeza kuwepo kwa Posho maalum kwa ajili ya kuwawezesha wanajeshi wetu kununua mahitaji yao muhimu.
Mheshimiwa Spika, waziri wa Fedha katika hotuba yake uk.88 alisema kuwa tarehe ya kuanza kutumika kwa utaratibu huu ni kuanzia Julai 1,2016 .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupatiwa majibu juu ya masuala yafuatayo;
i. Fedha za kulipa Majeshi yetu ‘posho maalum’ zipo katika fungu lipi la fedha za bajeti na hasa ikizingatiwa kuwa mafungu yote katika wizara husika yalishapitishwa na Bunge hili na posho hiyo haikuwepo?
ii. Je zile bidhaa na vifaa vilivyopo kwenye bohari za majeshi yetu zitapelekwa wapi na zipo kiasi gani kwani utekelezaji wa jambo hili umekuwa wa ghafla sana? yaani chini ya wiki tatu kabla ya utekelezaji wake kuanza
iii. Kwanini serikali isingewachukulia hatua wajanja wachache waliokuwa wanajinufaisha na msamaha huo na badala yake imeamua kuyaadhibu majeshi yetu yote?
22. BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KWA MWAKA WA 2016/2017
Mheshimiwa Spika, bajeti mbadala ya KRUB, ni tulivu na yenye kuleta matumaini yenye heri kwa Watanzania. Katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2015, cha mwezi Juni 2016 kilichotolewa na wizara ya fedha Sura ya I ukurasa wa 1 aya ya 2 kinaonesha takwimu za awali za Pato la Taifa kwa mwaka husika ni shilingi 90,863,681,000,000.
Angalia jedwali la I;
Jedwali I
Maelezo Shilingi Asilimia
Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya Pato la Taifa 18,172,736,200,000 20
Pato la Taifa 90,863,681,000,000 100
Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio wazi kwamba; tukiweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipa kodi, tukipanua wigo wa kodi, tukiwa na sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, ufanisi ukiongezeka TRA kwa asilimia 50, kudhibiti ukwepaji wa kodi, kupunguza misamaha isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi bandari ya Dar-es Salaam, kuweka mazingira mazuri na endelevu sekta ya Utali, kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta za madini, uvuvi, maliasili, nyumba,ardhi n.k. Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia aslimia 20.
Mheshimwa Spika, inawezekana kutekeleza kwa mambo hayo hapo juu. Hivyo, KRUB inapendekeza kukusanya shilingi 18,990,509,329,000/- ambapo mapato ya kodi na yasiyo ya kodi shilingi 18,172,736,200,000/- sawa na asilimia 20 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato ya Halmashauri ni asilimia 0.9 ya pato la Taifa sawa na shilingi 817,773,129,000/-
SURA YA MBADALA YA BAJETI 2016/17
MAELEZO MAPATO KATIKA SHILINGI (TZ)
A Mapato ya ndani ya Kodi na yasiyo ya kodi 18,172,736,200,000/-
B Mapatoya Halmashauri 817,773,129,000/-
JUMLA MAPATO YA NDANI 18,990,509,329,000/-
C Mikopo na misaada ya mashart nafuu 383,002,000,000
D Misaada na Mikopo ya miradi 2,745,659,000,000
E Misaada na mikopo ya Kisekta 372,147,000,000
JUMLA YA MIKOPO NA MISAADA YA NJE 3,500,808,000,000/-
JUMLA YA MAPATO YOTE 22,491,317,329,000/-
MATUMIZI
E Matumizi ya Kawaida 15,410,000,000,000/-
(i).Deni miradi ya maendeleo 8,000,000,000,000/-
(ii).Mishahara 6,600,000,000,000/-
(iii) Matumizi mengineyo
a. Wizara 360,000,000,000/-
b. Halmashauri 450,000,000,000/-
H Matumizi ya Maendeleo 7,081,317,329,000/-
1. Kukuza Uchumi Vijijini (35%) 2,478,461,065,150/-
2. Huduma za Jamii (28%) 1,982,768,852,120/-
3. Miundombinu (17%) 1,203,823,945,930/-
4. Usimamizi wa Ardhi (12%) 849,758,079,480/-
5. Utalii (8%) 566,505,386,320/-
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 22,491,317,329,000/-
Mheshimiwa Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani inategemea misaada toka kwa nchi wa hisani na kwa mashirika ya kimataifa (utegemezi) kwa 16% tu na tunaamini kwa mazingira mazuri yakiendelea kuwekwa bila ya kuwa kero kwa wadau wa sekta mbalimbali, na pia kuondoa mchwa wanaokula fedha za miradi katika halmashauri, ni dhahiri kwa miaka miwili ijayo tungeweza kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa inatilia mkazo juu ya ukuzaji uchumi vijijini (Rural Growth) na hivyo kuwa ni kipaumbele cha kwanza katika Bajeti zake Mbadala. Vivyo hivyo kwa mwaka huu imetenga 35%. Tunaamini kabisa kuwa ili Tanzania tuwe na uchumi wa viwanda ni lazima miundombinu ya barabara kutoka pembezoni mwa wilaya zetu, maji na nishati viwe ni vya uhakika, kwa njia hiyo hata uhamiaji wa vijana kutoka vijijini kuja mijini utapungua kabisa kwani wawekezaji watafungua viwanda vya uzalishaji na hata kilimo cha uhakika kitafanyika kwani masoko yatakuwa na uhakika vile vile.
Mheshimiwa Spika, Kipaumbele cha pili ni kwenye huduma za jamii ambazo kwa muktadha wetu ni elimu, afya na maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, ambapo Bajeti Mbadala imetenga 28% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kipaumbele cha tatu ni Miundombinu kwa maana ya Barabara za kuunganisha wilaya na wilaya, usafiri wa reli, usafiri wa ziwani n.k na imetengewa 17% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kipaumbele cha nne ni kwenye usimamizi wa ardhi, kwani tumeshindwa kutumia fursa ya ardhi yetu kukuza uchumi, na kwakuwa tulipendekeza uwepo wa chombo cha kusimamia na kuratibu sekta nzima ya majengo (Real estate regularatory authority-Rera) na pia kuhakikisha kuwa kodi za ardhi zinalipwa kwa utaratibu unaoeleweka, hivyo basi, imetengwa 12% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha tano na cha mwisho ni kuwekeza katika sekta ya utalii, kwani sekta hii ndiyo itakayoleta fedha za kigeni na kwa muda mfupi kama tutapunguza vikwazo vinavyopunguza idadi ya watalii wanaoingia na kukaa nchini kwa muda mfupi. Hivyo basi,bajeti mbadala imetenga 8% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani haikopi mikopo ya kibiashara kwani mikopo ya kibiashara hasa kwa mabenki ya ndani ndio chanzo kikuu cha kuua sekta binafsi hapa nchini. Hivyo basi kwa kuliona hilo bajeti mbadala ni bajeti ya kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiliamali wa ndani na nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa sekta zote za uchumi.
24. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kusema kwamba, Serikali hii ya awamu ya tano imeanza vibaya muhula wake wa uongozi kwa kulidanganya bunge kwa kuleta bajeti yenye takwimu zinazokinzana. Serikali imeeleza katika bajeti yake kwamba inakusudia kukusanya na kutumia shilingi trilioni 29.539 lakini cha ajabu ni kwamba vitabu vya mapato vinaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 22.063 na cha ajabu zaidi vitabu vya matumizi vinaonyesha kwamba Serikali itatumia shilingi trilioni 23.847 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 1.784 nje ya makusanyo.
Mheshimiwa Spika, Ukichukua jumla ya bajeti yote iliyotajwa na Serikali ya shilingi trilioni 29.539 ukatoa jumla ya makusanyo halisi ya shilingi trilioni 22.063 utapata tofauti ya shilingi trilioni 5.476 ambazo haziko kwenye makusanyo wala haziko kwenye matumizi. Ukichukua tofauti hiyo ya shilingi trilioni 5.476 ukajumlisha na shilingi trilioi 1.784 ambazo ziliingizwa kwenye matumizi nje ya makusanyo utapata jumla ya shilingi trilioni 7.26 ambazo hazimo katika makusanyo halisi ya Mapato.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imetafakari kina jambo hili na kufikia uamuzi kwamba; Serikali imelihadaa bunge na wananchi kwa kuliaminisha Bunge na wananchi kwamba ina bajeti ya shilingi trilioni 29.539 wakati ki-uhalisia Serikali hii ya awamu ya tano ina bajeti ya shilingi trilioni 22.063 tu ikiwa ni pungufu ya shilingi bilioni 432 ukilinganisha na shilingi trillioni 22.495 za bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
David Ernest Silinde (Mb)
NAIBU WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YAUPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA
YA FEDHA NA MIPANGO
10 Juni, 2016
Comments
Post a Comment