Mhasibu TANESCO ahukumiwa kifungo jela miaka 425 na faini shilingi bilioni moja

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kifungo cha miaka 425, aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lilian Chengula (42) baada ya kupatikana na hatia ya makosa 85 likiwemo la kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.3.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi alisema mshtakiwa amepatikana na hatia ya makosa 85 kati 167 yaliyokuwa yanamkabili na katika kila kosa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

Hata hivyo alisema, Chengula atatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja ambayo itakuwa ni sawa na kifungo cha miaka mitano jela. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shahidi alisema mshtakiwa akimaliza kutumikia kifungo chake, atatakiwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni moja.

Aidha aliwaachia huru washtakiwa wenzake watatu, ambao ni mfanyabiashara Salha Salim Saad (57), Salum Saad Ally (65) na Bakary Kinyogoli (65). Alisema anawaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa hawajatiwa hatiani katika makosa 82 yaliyokuwa yakiwakabili wote wanne.

Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 13 pamoja na vielelezi ili kuthibitisha mashtaka hayo. Mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka akiwa mtumishi katika Shirika la TANESCO, na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 1.3.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Chengula kupitia kwa Wakili wake Alex Mshumbusi, aliomba Mahakama imsamehe kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, kesi hiyo ni ya muda mrefu pia ana watoto wanaomtegemea, na muda mrefu hakuwepo kazini.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Aidha waliiomba Mahakama itoe amri kwa mshtakiwa huyo kulipa kiasi hicho cha fedha alichosababisha hasara ili kulifidia shirika hilo.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA