Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yawashukia Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU)
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kuhusu ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, iliyowasilishwa na Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU).
NEC imesisitiza kwamba ripoti hiyo imebainisha mapungufu ambayo hayapo kwenye sheria na taratibu, zinazoiongoza tume hiyo.
Miongoni
mwa mapungufu waliyoyatoa waangalizi hao ni Suala la Uchaguzi wa
Zanzibar, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na haki ya wagombea
binafsi kugombea nafasi katika uchaguzi wowote wa Tanzania Bara na
Zanzibar, mgawanyo wa majimbo na uwazi wa kuhesabu kura.
Akitoa
ufafanuzi huo, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema kuwa kwa
mujibu wa sheria, waliwapa nafasi hiyo waangalizi wa ndani na nje
kuangalia uchaguzi wa Tanzania Bara , kama unaenda kulingana na Katiba,
sheria na taratibu za uchaguzi huo.
Alisema
kuwa katika ripoti hiyo, waangalizi hao wamezungumzia uchaguzi wa
Zanzibar, ambao NEC hawahusiki nao na kwamba wamefanya makosa, kwa kuwa
wao walikuwa waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania Bara na sio Zanzibar.
‘’Waangalizi
wowote wa uchaguzi wanapoomba kibali kuangalia uchaguzi, wanatakiwa
kufuata taratibu kwa kutambua kwamba kuna NEC na Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC). Sisi tulitoa kibali kwa waangalizi hawa kuangalia
uchaguzi wetu na sio wa Zanzibar,’’ alisema.
Aliongeza kuwa, ‘’hawakupaswa
kuingiza katika ripoti yao masuala ya uchaguzi wa Zanzibar ulivyokuwa,
badala yake wangeeleza kama NEC hatukufuata sheria na taratibu kwenye
uchaguzi huu wa Tanzania Bara.”
Alisema pia kuwa waangalizi walitakiwa kuangalia uchaguzi huo na sio kupendekeza kwamba uchaguzi ulitakiwa kuwa vipi.
Kuhusu
suala la mgombea binafsi, alisema Katiba iliyopo sasa haijaruhusu,
hivyo wasingeweza kuweka wagombea hao, kwani Katiba ingewabana.
Kailima
alisema kuwa endapo Katiba Inayopendekezwa ingepitishwa, waangalizi hao
wangeweza kuhoji kwa nini hakukuwepo na mgombea binafsi, kwani ndiyo
inaeleza kuhusu mambo hayo.
Akizungumzia
mgawanyo wa majimbo, Kailima alisema kuwa kila halmashauri ya mji na
wilaya ni jimbo na kwamba hawapaswi kulinganisha kati ya Halmashauri ya
Temeke yenye watu 419,612 na jimbo la Madaba lenye watu 27,502, kuwa
mgawanyo wake haukufuata uwiano.
Alisema
kuwa mgawanyo wa majimbo, huzingatia mambo mengi, ikiwemo jiografia ya
eneo lenyewe. Alieleza pia kuwa NEC haijawanyima haki Wazanzibari kwa
kutoongeza idadi ya majimbo, kwa kuwa Bunge ambalo lilitakiwa kujadili,
lilikuwa limekamilisha kazi yake.
Alisema kwamba ZEC yenyewe ilichelewa kutangaza mabadiliko hayo ya majimbo kutoka 50 hadi 54.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania matokeo ya uchaguzi wa
Madiwani na Wabunge yalikuwa yanabandikwa kwenye vituo vya kupigia kura
pamoja na matokeo ya awali ya Rais.
Alisisitiza kuwa matokeo yote, yalikuwa yanasainiwa na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya siasa na kutangazwa kwa wananchi.
Aidha,
alisema kuwa hawakuweza kutangaza wabunge wa viti maalumu kabla ya
uchaguzi, kwani kisheria wanachagua wagombea hao baada ya kujua idadi ya
kura ya asilimia tano zilizopata chama, hivyo wasingeweza kutangaza
kabla ya uchaguzi.
Hata
hivyo, alisema kuwa Tume hiyo imepokea mapendekezo yao na itayafanyia
kazi ikiwemo kuwa na watumishi kwa ngazi zote. Kailima alisema kuwa hali
hiyo, itawasaidia kujua namna ya kuwaadhibu watumishi ambao watakiuka
utaratibu wa NEC.
‘’Pia
tutaongeza muda wa daftari la kupiga kura kuhakikisha kwamba kwa mwaka
linakuwepo mara mbili ili wapiga kura wote waangalie. Lakini suala la
Sheria ya Makosa ya Mtandao wanatakiwa kulipeleka kwa wahusika na
mengine kwa serikali kwani sisi kama NEC hatuhusiki nayo,’’ alisema.
Comments
Post a Comment