#BungeLive: "...matangazo yatarushwa moja kwa moja na redio zote" - Waziri Nape

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuviruhusu vituo vya redio nchini, kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja.

Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kupokea maoni ya wadau mbalimbali ikiwemo wanahabari waliokwenda Dodoma, kuonana na Uongozi wa Bunge kujadili suala hilo la matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa studio ya kuzalishia vipindi ya Mtandao wa Redio za Jamii nchini (COMNETA) iliyopo Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
“Jambo moja ni kwamba kupitia studio za Bunge matangazo yatarushwa moja kwa moja na redio zote zinaweza kupokea matangazo hayo na zenyewe zikarusha. Hii itasaidia hata kupunguza gharama kwa sababu zamani ilikuwa ni lazima utume wa waandishi upeleke vifaa, sasa hii redio nyingi hasa hizi za kijamii haziwezi kumudu,” alisema Nape.
Alisema jambo hilo ni jipya na kwa sababu ni jipya, litakuwa na mapungufu mengi na kadri siku zinavyoenda lazima kuna wadau watakaojitokeza kwa ajili ya kuelezea mapungufu hayo, ambayo serikali itakuwa ikiyafanyia kazi.

Nape alisema serikali iko tayari kukaa katikati ya Bunge, wananchi na wadau wengine kwa ajili ya kuhakikisha wanapata haki yao ya kupata taarifa.

Hata hivyo, Nape aliwataka waandishi wa habari kuongeza uzalendo kwa nchi, kwani wanatakiwa kutambua kuwa mambo wanayoyaandika mwisho yanakuwa na matokeo chanya au hasi.

Akizungumzia studio hiyo, Nape alisema redio za jamii, zina mchango mkubwa hasa katika kukuza demokrsaia nchini na kuongeza uelewa kwa wananchi katika masuala mbalimbali.

Aliongeza kuwa uwekaji wa studio hiyo, utawasaidia hata wanafunzi wanaosomea fani ya uandishi wa habari katika chuo hicho, kuitumia katika kujitolea ili kuongeza uelewa wao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sanyasi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodriguez alisema, shirika hilo linafurahishwa na maendeleo ya redio hizo nchini.

Alisema, wamefurahishwa na jinsi serikali ilivyorudisha heshima kwa kuzitumia redio hizo katika kutoa taarifa mbalimbali bkwa wananchi na hata katika kipindi cha uchaguzi hilo lilionekana.
“…tunapongeza hilo lakini tunaiomba serikali iendelee kuzitumia redio hizi za kijamii ili kuifikia idadi kubwa ya wananchi hasa wale walioko pembezoni, sisi UNESCO tunaunga mkono redio hizi,” alisema Rodriguez.
via Frank Leonard.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA