Ajali ya lori yaua watano mkoani Rukwa

Watu watano wamekufa papo hapo na wengine kujeruhiwa baada ya lori walilokuwa wakisafiria kushindwa kupanda mlima Lukangao na kupinduka. Ajali hiyo ilitokea juzi saa kumi na moja jioni katika kijiji cha Ntendo, Sumbawanga mkoani Rukwa.

Gari hilo ni lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 347 ATX ambalo ni mali ya mfanyabiashara Khalid Salum Abdallah, lililokuwa likiendeshwa na Abeid Said (32), mkazi wa Mazwi. Wakati likipata ajali, lori hilo lilikuwa limebeba zaidi ya magunia ya mpunga 80 pamoja na watu 10 waliokuwa wamekaa juu wakitokea kijiji cha Majimoto wilayani Mpanda. “Wakati likipanda mlima, lilipata pancha na hivyo kupoteza mwelekeo na kupinduka na watu kupoteza maisha,” alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage.

Kamanda Mantage aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni mwanafunzi wa Sekondari ya Karema, Lucy Andrew (24), Fumbuka Elias (28), Mayunga Mathias (30), na wengine wawili ambao bado hawajatambuliwa.

Majeruhi waliotajwa ni Athanas Choka (26), Ngaya Mihayo, Martin Paul (21), Geofrey Mwang'amba (20) na Cecilia Dominick (31). Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa na wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao ni nzuri. Dereva wa lori hilo alitoweka baada ya tukio hilo.

habari hii ni kwa hisani ya hisani ya gazeti la Uhuru

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA