Mpendazoe agombea ubunge kwa Chadema
Viongozi wa CCJ wakikabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa Chadema
CHAMA Cha Jamii (CCJ) kimeondokwa na vigogo wake na waanzilishi kadhaa wake akiwamo msemaji wake mkuu, Fred Mpendazoe aliyetangaza kugombea ubunge kwa tiketi ya Chadema.
Mwenyekiti wa chama hicho Richard Kiyabo, naibu Katibu Mkuu Nickson Ng'ihily na Msemaji wa Chama, Fred Mpendazoe jana walikabidhiwa kadi za Chadema jijini Dar es Salaam na mwenyekiti Freeman Mbowe.
Muda mfupi baada ya kupokea kadi hizo, viongozi hao walitangaza nia ya kugombea ubunge katika majimbo tofauti nchini kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Fred Mpendazoe ambaye mwanzoni mwa mwaka huu aliacha ubunge, kuihama CCM na kujiunga na CCJ, ametangaza kuwania ubunge wa Jimbo la Segerea, Richard Kiyabo anaenda Bukene na Ng'ihily anagombea Jimbo la Temeke. Jimbo la Segerea pia linawaniwa na Dk Makongoro Mahanga wa CCM.
Kabla ya kujiunga na CCJ, Mpendazoe alikuwa mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga kupitia CCM.
Akizungumza jana katika hafla hiyo kwa niaba ya wenzake hao, Mpendazoe alisema wameamua kujiunga na Chadema kwa kuwa sera na itikadi zake, vinafanana na zile za CCJ.
Pia alidai kuwa uamuzi wao wa kujiunga Chadema umetokana na hujuma zilizofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini dhidi ya CCJ.
"Kwa kuwa CCJ tunaamini kuwa umoja ni nguvu ya pekee ya wananchi katika kujenga usawa, uhuru na kuondoa umaskini, ujinga, maradhi na kupambana na ufisadi na Chadema kinaamini katika falsafa ya nguvu ya mamlaka ya umma,...hivyo basi tunatangaza rasmi kuwa Ng'ihily, Kiyabo na Mpendazoe tutagombea uongozi kwa tiketi ya Chadema," alisema.
Akizungumzia kuhusu Jimbo lake jipya la Segerea, Mpendazoe alisema anakwenda huko kugombea ubunge baadaya kuitwa na kushawishiwa na wakazi wa eneo hilo.
Aliwataka Watanzania wajitokeza kwa wingi kuwachagua wapinzani katika uchaguzi ujao ili wapate maendeleo ya kweli kwa kuwa CCM haiwezi kuleta mabadiliko.
Kwa mujibu wa Mpendazoe, Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali uliwekwa na Mungu na kwamba wananchi wake ni masikini wa kutupwa kutokana na uongozi mbovu usio na uzalendo wa CCM.
“Ndugu zangu, nyote ni mashahidi na mnaelewa juu ya utajiri mkubwa ambao Mwenyezi Mungu ameuweka ndani ya mipaka ya Tanzania, hata hivyo, ni jambo la kusiskitisha kwa kuwa wananchi wake ni masikini wakutupwa, umasikini unaotokana na uongozi usiojali wanyonge na usio na uzalendo wa CCM,” alisema Mpendazoe.
Alisema njia pekee ya kupambana na hali hiyo ni kwa wananchi kuunganisha nguvu zao na kudai mabadiliko kwa kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura siku ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyka Oktoba 31 mwaka huu.
“Naomba Watanzania waelewa kuwa huu si wakati wa kupigishwa porojo na kupewa kanga na fulana, ni wakati wa kusimama pamoja wanaume, wanawake, vijana na watoto kudai mabadiliko na hilo litawekana katika sanduku la kupigia kura,” alisema Mpendazoe na kuongeza “Tanzania yenye neeme bila CCM inawezekana”
Mpendazo alitumia nafasi hiyo kuwashawishi wanachama wa CCJ aliosema wamefika 9,500 kujiunga na Chadema huku akitaka wale wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kufanya hivyo.
Alisema Watanzania wa sasa wamechoshwa na mambo yalivyo sasa na wanahitaji mabadiliko ya kweli katika uongozi na uendeshaji wa nchi huku akisitiza kuwa CCM na serikali yake haviwezi kufanya hivyo.
Mbowe aliwakabidhi wanachama hao wapya kadi na vitabu vinne vinavyoelezea taratibu za chama hicho huku akitanabisha kuwa Chadema inaongozwa kwa taratibu, kanuni, sheria na mifumo.
“Sisi Chadema tunaongozwa kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria zilizopo. Hapa hakuna uongozi wa kufuata kauli ya mwenyekiti wa chama wala katibu au kiongozi yeyote,"alisema Mbowe.
Aliwapongeza wanachama hao kuchukua uamuzi huo na kueleza kuwa katiba ya Chadema iko wazi na kila mwanachama anayejiunga nacho anapata haki sawa na wanachama wote waliojiunga kabla yake.
“Chadema ni kama timu ya Real Madrid, inapokea wanachama kutoka kila kona. Hapa tunao wanachama kutoka vyama vyote vya saisa hii ni kutokana na kuwa chama makini kilichojengeka katika kuleta mabadiliko ya kweli,”alisema Mbowe.
Mbowe aliwataka Watanzania kutumia muda mfupi uliobaki kutafakari na kuchagua viongozi kutoka upinzani ili kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa hili.
habari hii ni kwa hisaniya gazeti la mwananchi
Comments
Post a Comment