Kanisa Katoliki latoa tamko kuhusu Dkt. Slaa

KANISA Katoliki limekuja juu na kukanusha tuhuma zinazoelekezwa kwa kanisa hilo kuwa limemtuma Dkt. Willibrod Slaa kuwania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Vile vile kanisa hilo limesema kuwa Kanisa Katoliki si taasisi inayojihusisha na harakati za kisiasa wala si chama cha kisiasa kinachohusika kwa namna yoyote ile na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Jude Ruwa'ichi alisema kuwa habari za kanisa hilo kuhusishwa na Dkt. Slaa katika harakati zake za siasa zimelenga kulichafua kanisa na kulipunguzia heshima ndani ya jamii.

"Tunapenda Watanzania wenzetu waelewe kuwa Kanisa Katoliki halijamtuma wala halitamtuma mtu yeyote kugombea nafasi ya uongozi kwa jina la kanisa, kwani si jukumu lake...kanisa litaendelea kuhubiri upendo, haki, amani, mapatano na mshikamano na litaendelea kutoa mchango wake na kushirikiana na raia wote wanaoitakia mema nchi," alisema na kuongeza:

"Kanisa litafanya hivyo ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki na unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu ili nchi ipate viongozi waadilifu, wanaojali maslahi ya wote ili wasaidie nchi ya Tanzania na watu wake kupata maendeleo ya kweli."

Askofu Ruwa'ichi ambaye pia anaongoza Jimbo la Dodoma, alisema kuwa Kanisa Katoliki lina mamlaka ambayo halikupewa na binadamu yeyote na wala hakuna binadamu anayeweza kupokonya mamlaka hayo, hivyo haliwezi kujihusisha na siasa.

"...Kulihusisha Kanisa Katoliki na harakati hizo za kisiasa ni upotoshaji na udhalilishaji ambao hauwezi kukubaliwa," alisisitiza.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa wao kama kanisa wataendelea kuwaomba wadau wote wa Uchaguzi Mkuu washiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa kuwajibika na kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani, kama matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Alisema kuwa Kanisa halitakubali kuhusishwa na chama chochote cha siasa wala mgombea yeyote, na linaamini kuwa serikali kwa upande wake na kwa kutumia vyombo vyake vitakuwa macho kuzuia vitendo hivyo.

Hatua ya kutoa ufafanuzi huo umetokana na gazeti moja la kila siku, kulihusisha kanisa hilo na mchakato wa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Slaa.

Gazeti hilo liliripoti kuwa baada ya Dkt. Slaa kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais, anategemea 'udini wa wakatoliki kushinda' na kwamba, 'aliingia makubalino yasiyo rasmi na baadhi ya maaskofu katoliki' kukamilisha mpango wake.

HABARI KUTOKA GAZETI LA MAJIRA

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA