na huu ndio mpango mzima wa fiesta 2010.

Tamasha la kumi la burudani na michezo na sanaa nchini Tanzania,
linalojulikana zaidi kwa jina la Fiesta limewadia, msimu unaanza tarehe 7
mwezi Julai ambapo utakuwa ni msisimko wa burudani kwa mwezi mzima, huku
wasanii wakitembelea baadhi ya mikoa ya Tanzania yenye msisimko wa sanaa
kujumuika na mashabiki wa sanaa, na kuonesha kazi zao.

Kwa mwaka huu wa 2010, Fiesta imepewa msemo wa Jipanguse, ikiwa na mlengo wa
kuhamasisha vijana, kuachana na tabia ya kulalamika kuhusiana na matatizo
wanayokutana nayo katika maisha yao ya kila siku, na badala yake wachukulie
matatizo hayo kama ni sawa na kuanguka, wajipanguse na kuendelea na safari
ya maisha..

Kauli mbiu hii inamsisitiza kijana wa kitanzania kuachana na habari za
kuhubiri matatizo yake huku akiomba msaada wa kuyatatua wakati akitumainiwa
kama mjenzi wa Taifa, kupitia burudani kijana anaelimishwa kuhubiri jinsi ya
kuutumia ujana wake kukabiliana na ugumu wa Taifa akiwa kama nguzo ya Taifa.


Mikoa nane ya Tanzania itajipangusa kiburudani na tamasha hili ambalo
hufanyika mara moja tu kila mwaka huku mwaka huu mikoa ya Arusha na Moshi
ikitarajia kupata ugenni kutoka Burundi ambapo mwanamuziki anayesifika kwa
tungo za mahaba mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya,
anayejulikana kwa jina la Kidumu, anatarajiwa kufanya maonesho mawili
makali na kulipa tamasha hili mtazamo mtofauti mwaka huu.

Katika kuanzia, tarehe 7.07.2010 katika viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro,
kuanzia saa nne asubuhi patakuwa na mambo, yakiwemo yale ya mbio za
mikokoteni, kukimbia na magunia, mbio za baiskeli za walemavu na za kawaida
na baada ya hapo, wanamuziki mahiri wanaoiendesha fani ya muziki wa kizazi
kipya nchini watatarajiwa kupanda jukwaani kuonesha sanaa yao kwa mashabiki
wa muziki wa mkoa huo.

Hii itakuwa ni kabla ya kuelekea katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha
ambapo matamasha ya mikoa hii yatafanyika tarehe 9 na 10.

Tamasha hilo litazunguka katika mikoa 8 ambayo ni Morogoro, Arusha, Moshi,
Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Zanzibar, Musoma na Mwanza.

Ratiba kamili inasema, baada ya Morogoro tarehe 7, tarehe 9 ni Matongee Club
Arusha na tarehe 10, kazi itakuwa mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Moshi katika
ukumbi wa La Liga.

Baada ya hapo Ijumaa ya tarehe 16 Julai, kazi itakuwa Royal Village ambapo
wasanii hawa watafanya onesho kali la usiku na kisha kesho yake, yaani
mchana wa tarehe 17 Julai, uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma tamasha
litafanyika kwa ajili ya familia.

Tarehe 24 Julai, safari ya kuelekea mkoani Tanga uwanja wa mkwakwani na
kama ilivyokuwa katika ufunguzi, mashindano mbali mbali, na kisha burudani
kwa wakazi wa mkoa wa Tanga.

Mwisho wa mwezi sasa, ndipo tamasha kubwa kwa ajili ya mji mkubwa, huku
msanii wa kimataifa na uwakilishi wa kutosha wa Afrika Mashariki utaonekana.
Jiji la Dar es Salaam na vitogoji vywake litajipangusa na kuwa safi na kisha
litajitupa katika ama Viwanja vya Leaders au vya Posta Kijitonyama,
mtafahamishwa zaidi kuhusiana na hili kadri tunavyoendelea.

Baada ya hapo safari ya kuelekea visiwani Zanzibar itaanza na huko burudani
itaangushwa pembezoni mwa bustani ya Forodhani, ndani ya ukumbi wa Ngome
Kongwe. Wakazi wa Zanzibar wataipata burudani hii kwa masaa yasiyozidi saba,
na kisha wasanii watarudi Dar es Salaam kujiandaa na safari ya Musoma.

Huko Tamasha litafanyika Musoma Hotel siku ya Ijumaa ya tarehe 6, na msanii
mwenyeji wa huko atakuwa ni Beatrice Moses, mwana Hip Hop ambaye ni zao la
shindano la Bongo Star Search 2009.

Tamasha litafungwa mkoani Mwanza, ambapo tarehe 7 mwezi wa nane, ndani ya
ukumbi wa Yatch, kutakuwa na patashika nguo kuchanika, na kisha kujipangusa
na burudani hii ya muziki, na siiku inayofuata, kazi itamalizikia CCM
kirumba ambapo mashindano ya michezo na burudani ya muziki vitaunguruma.

Tamasha la mwaka huu linakuja likiwa na wasanii wapatao 30 ambao ni Diamond,
Belle 9, Hussein Machozi, Baby J, Offside Trick, Chege& Temba, Shaa, Juma
Nature, Dully Sykes, Barnaba, Amini, Linah, Godzilla, Joh Makini, Roma, Kiki
Wa Pili, Young Dee, Fid Q, Mwana Fa, Mataaluma, JCB, Tip Top, Mwasiti, Pina
na Beatrice.

Fiesta Jipanguse ya 2010, inakujia kwa hisani kubwa ya Serengeti Breweries
Limited, Precision Air, Prime Time Promotions, Kitangoma Magazine, Mradi wa
kuzuia Malaria wa Zinduka, na Clouds FM.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA