Utata ujenzi barabara ya Serengeti

NDOTO ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia mradi wa ujenzi wa barabara ya kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara inayopita katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama mtaji wa kuombea kura kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu iko katika hatari ya “kuyeyuka” kutokana na jumuiya za kimataifa kupinga ujenzi huo.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita takribani 421 inatarajiwa kuanza kujengwa mwaka 2012 na tayari watalaamu wa upembuzi yakinifu wameanza kazi wakitarajiwa kuikamilisha mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa kwamba ujenzi wa barabara hiyo kuwa “ulimbo” wa kura kwa wapiga kura wa Kanda ya Ziwa zinathibitishwa na kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga. Waziri huyo amekaririwa na vyombo vya habari akisema ujenzi wa barabara hiyo kupitia Hifadhi ya Serengeti uko palepale kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Barabara hiyo ni ahadi iliyoko kwenye Ilani ya CCM kwa wapiga kura wa Kanda ya Ziwa kwa hiyo ujenzi wake ni lazima utekelezwe,” anasema Waziri Mwangunga. Aliwatoa wasiwasi wanaharakati wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi kuwa ujenzi huo utazingatia ushauri wa kitaalamu utakaotolewa kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo. “Tuko makini sana na suala la uhifadhi kwa hiyo ningependa kuwatoa hofu wanaharakati wa uhifadhi kwamba mradi wa barabara hautakuwa na madhara kwa wanyama na Hifadhi yenyewe ya Serengeti,” alisema.

Pamoja na kauli hiyo ya Mwangunga habari kuwa barabara hiyo ingerahisisha zaidi kampeni za CCM katika mikoa hiyo katika uchaguzi wa mwaka huu zilithibitishwa na moja wa watendaji wa CCM mkoani Mara ambaye alizungumza kwa simu na Raia Mwema mwishoni mwa wiki. "Ni kweli suala la ujenzi wa barabara hiyo ni moja ya ajenda za kampeni ya mikoa ya Kanda yetu.....unajua kabla ya kubuniwa kwa barabara hiyo na hadi sasa wananchi wengi wanataka kusafiri kwenda mikoa ya Kanda ya Kaskazini au hata Dar es Salaam wanapitia nchi jirani ya Kenya," alisema. Aliongeza: "Na safari hiyo ya kupita nchi jirani inakuwa na gharama kubwa lakini pia ni mbali na inachosha, hivyo kujengwa kwa barabara hiyo kungewapunguzia adha hiyo wananchi wetu na hilo tulipanga kuliweka wazi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu."”

Hata hivyo, kauli hizo za Waziri Mwangunga zinapingana na ripoti ya utafiti uliofanywa na jopo la wataalamu watatu waliobobea katika masuala ya uhifadhi na mazingira unaoonyesha kuwa barabara hiyo italeta madhara makubwa kwa Hifadhi ya Serengeti na misafara ya wanyama. Ripoti hiyo yenye kursa zaidi ya 30 imeandaliwa na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Gerald Bigurube, Profesa Anthony Sinclair wa Chuo Kikuu cha British-Columbia cha Canada na Marcus Bonner wa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS).

Ripoti hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuona nakala yake tayari imetumwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mwangunga ikiainisha athari kadhaa ambazo zitatokea endapo barabara hiyo itajengwa. Miongoni mwa madhara makubwa yaliyoainishwa ni pamoja na kuingilia mapito ya misafara ya wanyama hasa nyumbu kutoka Hifadhi ya Serengeti na Maasai Mara nchini Kenya.

Uhamaji wa nyumbu wanaokadiriwa kufikia milioni mbili kutoka katika hifadhi moja kwenda nyinigine mwaka jana iliingizwa katika kundi la maajabu saba ya dunia na tukio hilo limewavuta watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia pamoja na vyombo vya habari vya kimataifa. Wataalamu hao wanasema kuwa barabara hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na magari mengi kutokana na shughuli za kiuchumi kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na ile ya Kanda ya Kaskazini itayaweka rehani maisha ya viumbe adimu wanaopatikana katika Hifadhi ya Serengeti. “Barabara hiyo pia itaongeza shughuli za kibinadamu ambazo haziendani na matakwa ya uhifadhi, uharibifu wa mazingira na pia itavuruga matembezi huru ya wanyama pori katika hifadhi hizo kubwa,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo. Wataalamu hao wameonya kuwa iwapo Serikali itang’ang’ania mradi wake huo wa ‘barabara-kwa-kura’ ipo hatari Tanzania kupoteza heshima yake mbele ya macho ya jamii za kimataifa kwa kuupuza uhifadhi.

Si hivyo tu, Tanzania pia itapoteza mapato makubwa yatokanayo na sekta ya utalii yanayokadiriwa kufika dola milioni moja zinazoingizwa na Hifadhi ya Serengeti pekee na ajira rasmi na zisizo rasmi zipatazo 600,000 zitakuwa shakani. “Barabara hiyo itahatarisha nafasi na sifa ya Hifadhi ya Serengeti ya kuwa moja ya vivutio vilivyoko katika urithi wa dunia iliyopewa na UNESCO,” inasema ripoti hiyo.

Wataalamu hao katika ripoti yao wanaeleza bayana kuwa Serengeti ndiyo eneo pekee duniani linaloonyesha sura halisi ya dunia ilivyokuwa miaka milioni moja iliyopita. Wataalamu hao wamekwenda mbali zaidi na kushauri maeneo mbadala ambayo Serikali inaweza kupitisha barabara hiyo ili kuinusuru Hifadhi ya Serengeti. Wanasema kuwa barabara hiyo inaweza kujengwa kusini mwa Hifadhi hiyo ikianzia wilayani Karatu hadi wilayani Meatu mkoani Shinyanga hadi Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara na urefu wake utakuwa kilomita 383 ambazo ni pungufu ya zile za kupitia hifadhini.

Iwapo barabara hiyo itajengwa ndani ya Hifadhi ya Serengeti itakuwa na urefu wa kilomita 421 ambazo ni nyingi na gharama itakuwa kubwa zaidi kuliko kupita nje ya Hifadhi. Akizungumza katika mahojiano ya simu na Raia Mwema kutoka nchini Uingereza, Bigurube alithibitisha kuwa ni kweli waliaandaa taarifa hiyo ya kitaalamu ili kuisadia Serikali kupata njia sahihi ya kutekeleza mradi huo bila kuleta madhara yaliyotajwa. “Ni kweli tumeaandaa ripoti lakini mimi niko nchini Uingereza kwa likizo hivyo wasiliana na wenzangu walioko Soronera ili upate ufafanuzi zaidi….lakini kwa kifupi tumetoa ripoti hiyo kwa mwongozo kwa Serikali,” alisema Bigurube.

Mbali na wataalamu hao, bado Tanzania inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati mbalimbali nje na ndani ya nchi kuhusu mradi huo barabara wakitaka usitishwe mara moja kuinusuru Hifadhi ya Serengeti ambayo ni urithi wa dunia. Moja ya taasisi hizo ni Wildlife Society of Tanzania (WCST) ambayo ilikuwa katika harakati za kuungwa mkono na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ili kuishawishi Serikali kutafuta njia mbadala na kuachana na wazo la kutekeleza mradi huo. “WCST inafanya juhudi za kukusanya maoni kutoka kwa wadau wengine ili kupinga mpango huo wa Serikali, na lengo letu ni kuinusuru Serengeti kwa manufaa ya Taifa letu na vizazi vijavyo,” inasomeka sehemu ya waraka pepe uliosambazwa na na taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Arusha, Deusdedit Kakoko, jumla ya dola za Marekani milioni 480 (makadirio ya shilingi bilioni 500) zitatumika kujenga barabara ya Arusha-Musoma ambapo kati ya hizo dola milioni 260 zitatumika kujenga kipande cha Arusha-Serengeti na nyingine dola milioni 220 zitatumika kujenga sehemu iliyobakia ya Serengeti-Musoma. Kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa, Kakoko alisema kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo utaanza mapema mwaka 2012 baada ya upembuzi yakinifu kukamilika mwishoni mwa mwaka huu. Barabara hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na magari mengi, itaanzia eneo la Mto-wa-Mbu wilayani Monduli, na itapita Engaruka-Engaresero , Ziwa Natron, Loliondo, kona ya Serengeti Kleins hadi Mugumu na Musoma mjini.

habari hii ni kutoka gazeti la raia mwema website ni www.raiamwema.co.tz

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA