viwango vipya vya soka.... Brazil yashuka

*Hispania yashika ukanda, Tanzania yazidi kuzama
ZURICH, Uswisi
BRAZIL imeporomoka kwa nafasi mbili kwenye ubora wa viwango vilivyotolewa jana na Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA, huku Hispania ikishika ukanda ikifuatiwa na Uholanzi.

Mabingwa hao wa dunia mara tano, walikuwa wakishika namba moja kwenye chati hizo za FIFA tangu April 2010 imeporomoka ikiwa ni baada ya matokeo mabaya ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini.

Brazil iliondoshwa na Uholanzi katika mechi ya robo fainali kwa kufungwa mabao 2-1 ambayo ilikuwa ikishika nafasi ya nne kabla ya kupanda nafasi ya pili kwenye viwango hivi vipya vya Fifa. Uholanzi ilifungwa bao 1-0 na Hispania kwenye fainali.

Kwa mujibu wa viwango hivyo vipya vya Fifa, Tanzania imeshuka kwa nafasi nne kutoka nafasi ya 108 ambayo ilikuwa ikiishikilia mwezi Aprili mpaka nafasi ya 112.

Januari mwaka huu, Tanzania ilikuwa nafasi ya 108 sawa na Februari kabla ya kushuka kwa nafasi moja hadi 109 mwezi Machi. Ilipanda tena kwa nafasi moja mwezi Aprili hadi ilipoporomoka.

Viwango hivyo vipya vya Fifa vinaonyesha Uruguay imepanda kwa nafasi 10 hadi nafasi ya sita wakati Ghana imepanda kwa nafasi tisa na inashika nafasi ya 23 wakati Paraguay imepanda kwa nafasi 15 na inashika nafasi ya 16.

Timu ya Cameroon imeshuka kwa nafasi 21 na hivi sasa inashika nafasi ya 40 katika viwango vipya vya Fifa, Ivory Coast imepanda kwa nafasi moja inashika nafasi ya 26, wakati Nigeria imeshuka kwa nafasi tisa hadi nafasi ya 30.

Algeria imeshuka kwa nafasi tatu inashika nafasi ya 30 na Afrika Kusini imepanda kwa nafasi 17 inashika nafasi ya 66.

Ukiacha Tanzania ambayo inashika nafasi ya 112 kwenye viwango vya FIFA, viwango vya timu nyingine za Ukanda huu wa Afrika Mashariki ni kama ifuatavyo; Uganda imepanda kwa nafasi tatu hivi sasa inashika nafasi ya 70, Rwanda imeshuka kwa nafasi sita hadi nafasi ya 113.

Kenya imeshuka kwa nafasi mbili na sasa inashika nafasi ya 115 na Burundi imepanda kwa nafasi tatu hadi nafasi ya 141.

Katika upande wa Afrika, Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 26 hadi ya 28 ikiwa juu ya Rwanda ambayo ipo nafasi ya 29, wakati Uganda ipo nafasi ya 13, Kenya nafasi ya 30 na Burundi nafasi ya 37.

Kwa mujibu wa viwango vya CAF, Misri ndiyo inaongoza ikifuatiwa na Ghana kwenye nafasi ya pili na Ivory Coast kwenye nafasi ya tatu.

Februari 1995, Tanzania ilishika nafasi ya 65 katika viwango vya Fifa, hicho ndiyo kiwango cha juu Tanzania kuwahi kushika katika viwango vya FIFA , na kiwango cha chini kabisa Tanzania ilishika nafasi ya 175 mwezi Oktoba 2005.

habari hii ni kwa hisani ya tovuti ya www.mwananchi.co.tz

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA