MIKAKATI YA KUWEKA MANISPAA YA MUSOMA SAFI YAZIDI KUBOREKA

Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara imejiwekea malengo ya kufanya usafi wa mazingira kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi ili kuweka mji huo katika hali ya usafi.

Akisoma Risala siku ya uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya usafi wa mazingira, Afisa Afya wa Manispaa hiyo, Peter Mtaki alisema kuwa uzinduzi huo utakuwa chachu uya uendeshaji wa usafi wa mazingira kwa kila mtu, kaya, nyumba, mtaa na kata.

“Pia kampeni hii itafanya watu wabadili tabia na kuona kuwa suala la usafi si la watumishi wa Idara ya Afya pekee ni suala la mtambuka kila mtu kwenye eneo lake analoishi na anakofanyia kazi mazingira yake yawe safi,” alisema Mtaki.

Alisema kuwa halmashauri hiyo lishatunga sheria ndogo ya usafi wa mazingira ambayo mpaka sasa ndiyo inayotumika ambapo sheria hii inamtaka kila mkazi kuweka eneo lake safi kuanzia majumban, eneo lake la kazi na maeneo ya biashara pamoja na kuchangia kiasi cha shilingi 500kama ada ya usafi.

Vile vile halmashauri ilianza kuunda vikundi vya usafi katika kata tano ambazo ni Kitaji, Nyasho, Mkendo, Mwigobero na Nyakato. Pia wale ambao wanakuwa wagumu wa kutojali usafi na kuchafua mazingira watabanwa na sheria ndogo ambayo ni faini ya shilingi laki tano au kifungo cha miezi mitatu au adhabu zote.

“Kampeni hii inamtaka kila mtu awe ni askari kwa yeyote Yule atakayeonekana anachafua mazingira achukuliwe hatua papo hapo na kufikishwa kwa wahusika mitaani, katani au Manispaa kwa hatua zaidi,”alisema Mtaki.

Naye Mkuu wa Mkoa John Tupa alitoa wito kwa mabwana afya watekeleze wajibu na majukumu yao kama zamani na kusimamia sheria vizuri ipasavyo zinazohusu mazingira.

“Watendaji kufanya kazi kwa maagizo ya viongozi wa Mkoa siyo kanuni na taratibu za utawala bora badala yake wafanye kazi kwa kusimamia sheria zilizopo na kwamba kwa kufanya hivyo ni kujiaibisha,”alisema Tupa.

Manispaa hiyo imeahidi kumuenzi makamu wa Rais wa Dkt. Mohamed Bilal wakati alipofanya uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira Februari 12 mwaka jana na kuwa itafanya zoezi hilo kuwa endelevu.

Halmashauri hiyo inazalisha kiasi cha tani 90 kwa siku na taka ambazo zinakusanywa na kutupwa ni tani 62 kwa siku zinazozalishwa toka kwenye nyumba za makazi, maeneo ya biashara , viwandani na kiasi kidogo toka kwenye bustani.

 
Na Thomas Dominick kutoka Musoma.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA