WAZIRI AZINDUA AKAUNTI YA TWIGA STARS TIGO PESA

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara leo (Machi 10 mwaka huu) amechangia sh. milioni moja kwenye uzinduzi wa akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC).
 
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Dk. Mukangara alisema ni jukumu la kila Mtanzania kuichangia Twiga badala ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuachiwa pekee mzigo huo wa kuendesha timu hiyo.
 
Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Kwa Waziri Dk. Mukangara kuchangia sh. milioni moja alifanya mihamala miwili.
 
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani alisema Twiga Stars kwa sasa haina mdhamini na Shirikisho limekuwa likibeba mzigo wa kuhakikisha inashiriki katika mechi za kirafiki na mashindano mbalimbali kwa vile imekuwa ikifanya vizuri.
 
Twiga Stars inayofundishwa na kocha Charles Boniface Mkwasa iko kwenye raundi ya pili ya mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa.
 
Katika raundi ya kwanza, Twiga Stars iliitoa Namibia kwa jumla ya mabao 7-2. Ilishinda ugenini 2-0 na kuibuka na ushindi mnono nyumbani wa mabao 5-2. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA