TIDO MHANDO MKURUGENZI MTENDAJI MPYA WA MWANANCHI COMMUNICATION LIMITED




MKURUGENZI Mtendaji mpya wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando, amewataka wafanyakazi wa kampuni hiyo, kuchapa kazi kwa bidii, ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa.Tido alitoa wito huo jana katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wafanyakazi, muda mfupi baada ya kutambulishwa rasmi.

Mkurugenzi huyo anayechukua nafasi ya Sam Shollei, aliyemaliza muda wake wa kufanyakazi nchini, alianza kutumikia nafasi hiyo juzi.Alisema kampuni hiyo imepiga hatua kubwa kwa  mafanikio, lakini vema wafakanyakazi wakazidisha  juhudi ili kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Mhando alisema ili azma hiyo iweze kufikiwa, kuna haja kwa wafanyakazi wa MCL kupendana, kuheshimiana na kufanya kama timu.“ Binafsi najiona kuwa nina changamoto kubwa ya kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa, hilo litafanikiwa ikiwa tutaheshimiana, tutapendana na kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema.

“Napenda kufanya kazi kwa ufanisi, tukishirikiana kufanya hivyo tukiwa kama familia moja tutafanya mambo makubwa ya kuiendeleza kampuni yetu,”alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Alimpongeza na kumshukuru kwa dhati, Mkurugenzi Mtendaji aliyemaliza muda wake, (Shollei) kwa kuiwezesha kampuni kupata faida katika kipindi cha mwaka uliopita.Kampuni MCL inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumapili, The Citizen on Sunday na Mwanaspoti, mwaka jana 2011 ilipata faida ya Dola 1 milioni za Marekani (Sh 1.6 bilioni).

Kwa mujibu wa Shollei, mwaka huu kampuni inatarajia kupata faida ya Dola 3 milioni (Sh 4.8 bilioni).“Mafanikio hayo yananivutia kufanya kazi katika kampuni hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika kuiendeleza,” alisema Mhando ambaye uteuzi wake umekuja baada ya kuwashinda wenzake 15 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.

Kwa upande wake Shollei,  aliwashukuru viongozi na wafanyakazi wa MCL kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha kuendesha kampuni na kuiwezesha kufikia mafanikio hayo.

“Nawashukuru viongozi na wafanyakazi kwa sababu ushirikiano mlionipa ulinifanya nitekeleze majukumu yangu kwa urahisi na kufikia mafanikio tunayojivunia,” alisema.

 “Nashukuru kwamba namkabidhi kampuni Tido Mhando mwanahabari shujaa ambaye amefanya makubwa katika tasnia hii ya habari, mpeni ushirikiano atafanya makubwa,”alinena Shollei.

 
Mhariri Mtendaji wa MCL, Theophil Makunga, ambaye amekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji tangu Novemba mwaka jana, alimpongeza Mhando kwa kujiunga na kampuni hiyo na kuelezea matumaini yake kuwa mafanikio yaliyopatikana yataendelezwa.

Pia alimpongeza Shollei kwa mafanikio yaliyofikiwa na kwamba anaondoka nchini akiwa shujaa wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd.“Alijiunga na kampuni hii miaka mitano iliyopita na kampuni ilikuwa haitengenezi faida lakini kuanzia mwaka jana tumepata faida tumeweza kufikia malengo tuliyojiwekea hivyo kwetu sisi huyu ni shujaa,” alisema Makunga.

Shollei amepangiwa kazi nyingine katika makao makuu ya Kampuni mama ya Nation Media Group (NMG) jijini Nairobi,Kenya.  Mhando amefanya kazi ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 30.

Amewahi kufanya kazi katika iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kisha kwenda nje ya na kufanikiwa kupata heshima ya kuwa Mwafrika wa kwanza  kuwa  Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza  (BBC).

Pia amewahi kufanyakazi katika mashirika mengine ya habari ya nje ambayo ni pamoja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na Redio Deutche Welle (DW), ya Ujerumani.
Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kabla hajamaliza mkataba wake mwaka jana.

SOURCE  www.mwananchi.co.tz

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA