Andrew Nyerere; Mwalimu angekuwepo angepinga ufisadi!


Andrew Julius Nyerere
Kuna maswala kadha wa kadha yanayoikabili Tanzania kwa hivi sasa, miongoni mwa mambo haya ni sakata la akaunti ya Tegeta/Escrow, mchakato wa katiba mpya na mengine mengi. Mwandishi Nova Kambota amefanya mahojiano na Andrew Julius Nyerere ambaye ni mtoto wa kwanza wa baba wa taifa hayati Mwalimu Nyerere, fuatana naye katika mahojiano haya………………
SWALI; Kuna mambo kadhaa yaliyojitokeza siku za karibuni ambayo watu wanataka kufahamu manufaa yake kwa taifa, moja ya matukio hayo ni ziara ya Jafar Mermo  Idd Amin mtoto wa rais wa zamani wa Uganda marehemu Idd Amin mwaka 2008, je ziara hiyo ambayo ilimkutanisha na Madaraka Nyerere walipozuru Butiama ilikuwa na manufaa gani kwa taifa?
JIBU; Kwa familia ya Mwalimu Nyerere na familia ya marehemu Idd Amin nadhani ilikuwa jambo zuri kuleta upatanishi, kuhusu kama taifa lilipata faida sijui. Aliongea Jafari kuhusu kuanzisha mfuko wa hela kuwasaidia wanajeshi walioathirika na vita vya Kagera(wa Uganda na Tanzania), pia nchi hizi mbili zilihitaji kupatanishwa , Jenerali Musuguri alikuwa anaongea katika redio miezi michache iliyopita, kwamba wanajeshi wetu walikuwa na hasira sana, kabla ya kufika Kyaka walikuwa wameshawaua watu 10,000(elfu kumi), Jenerali Musuguri yupo hapa Butiama, natamani kwenda kumuuliza kama hao wote waliouwawa walikuwa ni maadui kwasababu hii ilikuwa ni vita yetu ya kwanza, inawezekana makosa yalifanyika.
SWALI; Una maoni gani kuhusiana na mwenendo wa CCM iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere ambayo sasa baadhi ya viongozi wake wanatuhumiwa vikali kujihusisha na ufisadi? Hudhani ni sababu tosha kwa watanzania kuikataa CCM ikiwa inakiuka misingi ya kuundwa kwake?
JIBU; CCM iliamua kujiita Chama Cha Mapinduzi kwa maana ya mapinduzi yaliyofanyika Urusi au Uchina, kwa maana kwamba watu walio wengi wakiwa na njaa wataleta fujo za kuiangusha serikali kama wamechochewa au hata kama hawajachochewa. Iwapo CCM itaendeleza hayo mapinduzi wananchi wataendelea kuichagua, inategemea tu watu wangapi bado wanaamini inaendeleza mapinduzi, maoni yangu mimi siyo muhimu, watu waamue, na nadhani wanaweza kugawanyika katika maamuzi.
SWALI; Miaka ya karibuni kumekuwa na watu wanaohoji namna baba wa taifa Julius Nyerere alivyoaga dunia, baadhi ya wanasiasa wametilia shaka mara kadhaa kifo chake mpaka ikampelekea Madaraka Nyerere kutoa kauli, vipi mtazamo wako kuhusu hili? Kuhoji kifo cha Nyerere kuna maslahi yoyote kwa taifa?
JIBU; Magige , mtoto wa Mwalimu anasema kuna chanjo moja ilikuwa wapewe watanzania ambayo Mwalimu alikuwa ana mashaka nayo. Mwalimu alimwambia Dr Mwakyusa kwamba yeye apewe, aijaribu halafu akiridhika ataiidhinisha wapewe Watanzania, lakini alipopewa hiyo chanjo, Mwalimu hali yake ilibadilika ghafla, amefariki. Niliposikia hiyo stori nilimweleza Magige kuhusu Global 2000 Report ya Warren Christopher, inasemekana katika miaka ya sabini viongozi wa Afrika walishauriwa na IMF wakubali wananchi wao wachanjwe chanjo za magonjwa ili watu wapungue ili iwe rahisi kuwasaidia; kwamba tatizo la kuwasaidia ni tatizo la logistics tu. Inasemekana ushauri huo ulikubaliwa na viongozi wetu. Global 2000 Report ni Top Secret ipo United Nations na hata ukiwa kule huwezi kuipata mpaka uwe na Special Clearence. No, nilimwambia Magige hatutapata faida yoyote tukianza kuuliza maswali kuhusu kifo cha Mwalimu, kama kuna mtu anabisha kwamba World Health Organization inaweza kufanya ufisadi, mtu huyo huwa anashauriwa kufanya utafiti jinsi W.H.O ilivyoanzishwa.
SWALI; Unazungumziaje mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya nchini, kutokana na matukio yanayoendelea kujitokeza kama Mzee Warioba kupigwa na hali ya kutoelewana miongoni mwa watanzania, Je unaona wapi tumekosea? Nini kifanyike kunusuru mchakato huu ili tupate katiba itakayolivusha taifa letu kutoka hapa tulipo?
JIBU;  Hakuna matatizo kuhusu katiba , isipokuwa kama kuna maoni yanayoweza kuiboresha katiba , maoni mapya ambayo siyo ya UKAWA , sasa ndiyo wakati wa kuyatoa.
SWALI; Unazungumziaje uongozi wa baba wa taifa hayati Mwalimu Nyerere? Una lipi la kusema kwa kumlinganisha na viongozi wa zama hizi?
JIBU; Sioni sababu ya kuwalinganisha viongozi wa awamu tofauti, zama tofauti zinahitaji viongozi, kumlinganisha Nyerere na Kikwete hiyo itakuwa sawa kumlinganisha Bismark na Angela Markel.
SWALI;  Unazungumziaje harakati za vyama vya upinzani nchini kupambana na ufisadi kama wa hivi karibuni wa Tegeta/Escrow? Unadhani vyama hivi vya upinzani vina dhamira ya dhati kupambana na madudu?Je vitafanikiwa?
JIBU;  Vyama vya upinzani vina nia njema , hii kashfa inayojadiliwa sasa hivi Bungeni imeletwa na upinzani. Hii vita ya sasa hivi ya Bungeni wanaweza kushinda, lakini kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa ni jambo lingine.
SWALI; Kadri ulivyomwelewa hayati Nyerere, unazungumziaje kutokuwepo kwake? Je unadhani angekuwepo angesaidia vipi kunusuru taifa kwenye kupambana na ufisadi na kunusuru mchakato wa katiba mpya?
JIBU; Mwalimu angekuwepo angepinga ufisadi, kuhusu katiba hakuna tatizo kubwa au naweza kusema hakuna tatizo lolote zaidi ya fujo inayoletwa na UKAWA.
 SWALI;  Ukipewa nafasi ya kuwashauri vijana wa sasa wa Tanzania, ungependa wafanye nini kulisaidia taifa lao?
JIBU; Vijana wa Tanzania wafikiri sana kabla ya kuwachagua viongozi.
SWALI; Unapata tafsiri gani unapoona taasisi za kidini kama kanisa katoliki likianzisha, kusimamia na kuratibu mchakato wa kumtangaza hayati Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu?
JIBU; Kanisa katoliki ndiyo linataka Mwalimu aitwe lay saint, Mwalimu aliishi maisha ya uadilifu lakini kama alikuwa mtakatifu hiyo ni kwa Vatican kuamua.
SWALI; Unaweza kueleza nini kuhusu siku za mwisho za uhai wa Mwalimu na namna alivyokuwa akilalamikia ubinafsishaji/uuzwaji wa mashirika ya umma kama benki ya taifa ya biashara NBC, ukizingatia hali ya ugonjwa wake na uzalendo wake kwa nchi, alikuwa mtu wa namna gani? Alionekanaje nyakati zile?
JIBU; Uuzaji wa mashirika ya umma au ubinafsishaji siyo jambo baya wakati wote.
 Swali; una lolote la kumalizia?
Jibu; Kwa kumalizia, nataka kusema viongozi wachaguliwe kwa uadilifu, kwasababu ukiwachagua mafisadi, Mungu ataheshimu uteuzi wako, hatabadili kitu chochote!
Andrew Nyerere anaweza kupatikana kwa namba 0718- 536281, ikiwa unataka kuwasiliana na Nova Kambota mwandishi aliyefanya mahojiano haya piga simu namba 0712-544237, barua pepe; novakambota@gmail.com au tembelea http://novakambota.wordpress.com

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA