MASWALI 10 KWA MBUNGE WA MUSOMA MJINI VINCENT NYERERE NA MAJIBU YAKE

1. Fazel Janja

Tunaelekea uchaguzi mkuuunafikiri nini haujawafanyia wananchi wako na ni kwa nini hujakifanya, unafikiri ukipewa nafasi utawatekelezea?

Jibu. Tuliahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha sita kwa ngazi ya jimbo, hatukufanya hivyo zaidi ya kupunguza ada kwa kuwa tulitegema kuunda Serikali na kupata mawaziri ila haikuwa hivyo.

2. David Katikiro

Ulitoa ahadi 11 wakati wa kampeni je, umetekeleza kwa kiwango gani?

Jibu. Ahadi nilizotoa kwa sasa zimetimia kwa asilimia 89. Yapo tunayotekeleza nje ya ahadi kulingana na umuhimu na dharura.

3. Swalehe Juma

Wewe ni Mbunge wa Musoma Mjini lakini umekuwa ukijitangaza kuwa ni mbunge wa Mkoa wa Mara. Kwa mfano, uliwahi kutangaza hivyo katika mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya na katika Kijiji cha Wegero wilayani Butiama je, mamlaka hayo uliyatoa wapi?

Jibu: Mimi peke yake ambaye ni mbunge wa jimbo kutoka chama cha upinzani, Chadema katika Mkoa wa Mara na mamlaka hayo nilipewa na wananchi.

4. Felix Kalisa

Uliahidi kukomesha michango shuleni hasa katika shule za misingi lakini michango hiyo bado inaendelea mpaka sasa, mfano Shule ya Msingi Bweri kila mwanafunzi anatakiwa kuchangia Sh2,000 kwa ajili ya kuchapisha mitihani kila wafanyapo mitihani je, ni nini tatizo?

Jibu. Mitihani iliyopo katika muhula haina michango, ila baadhi ya shule kwa makubaliano na wazazi ili kuinua kiwango cha ufaulu, ipo mitihani ya majaribio na ziada ambayo wazazi husaidiana kufanikisha.

5. Abida Mafuru

Uliahidi kupeleka kompyuta katika shule zote za sekondari za kata, lakini hadi sasa umegawa kompyuta sita tu katika shule sita. Je, vipi kuhusu shule zilizobaki?

Jibu. Tayari nimepeleka kompyuta 15 na ‘projector’ sita kwa shule tatu, kwa mwaka juzi wa fedha, mwaka jana wa fedha pia tumenunua nyingine 15 na projector tatu, mwaka huu wa fedha tunamaliza kwa shule zote.

6. Sophia George

Ukiwa mbunge una lipi la kujivunia katika kuboresha sekta ya miondombinu jimboni kwako?

Jibu. Bado sijaridhika kiasi cha kujivunia japo hakuna njia isiyopitika tofauti na nilipokabidhiwa jimbo, kiwango cha uboreshajishaji hakijafikia mwisho.

7. Anna Wansame

Muda mwingi umekuwa nje ya jimbo huku ukishughulika na masuala ya chama zaidi. Je, majukumu yako ukiwa mbunge unayatekeleza vipi?

Jibu. Kazi za bunge pia hutekelezwa bungeni Dodoma, kwenye kamati na ninapokuwa jimboni nafanya utekelezaji hasa kipindi hiki kwa kushirikiana na madiwani.

8. Bigambo Jeje

Una nia ya kugombea tena? Kwa nini?

Jibu. Kwa kuwa bado imani yangu na Wanamusoma wenzangu imeongezeka, sitawaangusha nitagombea tena maana wao ndiyo waamuzi.

9. Mwita Mahende

Una mpango gani na Uwanja wa Ndege wa Musoma? Kwa vile unachangia kuporomoka kwa uchumi wa mkoa kutokana na kusitisha shughuli zake hali inayowalazimu wasafari wa anga kutoka Mkoa wa Mara kutumia Uwanja wa ndege wa Mwanza?

Jibu. Katika mpango wa viwanja 10 vinavyotakiwa kuwekwa lami pia Kiwanja cha Musoma kiliwekwa katika orodha na hii itategemea na upatikanaji wa fedha serikalini. Tayari naibu waziri akijibu swali langu bungeni aliahidi kutekeleza.

10. David Katikiro

Kuna taarifa kuwa Bandari ya Musoma inatakiwa kuhamishwa katika eneo la Kigera Etuma wilayani Butiama je, ni kwa nini?

Jibu. Bandari haitahama ila kuna ujenzi wa bandari mpya maeneo ya Musoma Mjini au Butiama ila bado hatujafanya uamuzi. Hata ikijengwa mpya maeneo ya Butiama, hii ya zamani bado itakuwapo. Ila kwa maoni yangu ni bora kupanua iliyopo kwa sababu wananchi wapo tayari kupokea fidia kupisha upanuzi.


Chanzo: Mwananchi | 19 Novemba, 2014

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA