INTERPOL KUDHIBITI UTOROSHAJI WA MADINI YA TANZANITE

Serikali imesema itatumia Polisi wa Kimataifa (Interpol), kukabiliana na utoroshaji madini ya vito ya Tanzanite nje ya nchi.
Hatua hiyo inakuja huku Kenya na India zikiongoza kwa kuuza Tanzanite kwenye soko la dunia mwaka jana na kuizidi Tanzania, ambako ndiko madini hayo hupatikana pekee duniani.
Akifunga maonyesho ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyomalizika jana jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Madini, Richard Kasesela alisema Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kuchunguza na kubaini njia na mbinu zote zinazotumika kutorosha madini hayo nje ya nchi.

“Kuanzia sasa, yeyote atakayekutwa akiuza Tanzanite nje ya nchi bila cheti cha uhalisia kinachothibitishwa yametoka Tanzania kupitia njia halali, atakamatwa na kurejeshwa nchini na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi,” alisema Kasesela
Alisema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia madini na rasilimali zinazopatikana nchini kuendelee kunufaisha watu na mataifa mengine.
“Tanzanite lazima iuzwe kutoka Tanzania na inufaishe wananchi na Taifa la Tanzania,” alisisitiza Kasesela
Wakizungumza muda mfupi mara baada ya hafla ya ufunguzi wa maonyesho hayo Jumanne iliyopita, Naibu Katibu Mkuu, Ngosi Mwihava na Kamishina wa Madini nchini, Paul Masanja walisema Tanzania inauza asilimia 20 pekee ya madini ya Tanzanite, huku asilimia 80 iliyosalia ikiuzwa na Kenya na India.
Wakati Kenya iliuza Tanzanite yenye thamani ya zaidi ya Sh173 bilioni, India Sh509 bilioni, Tanzania iliuza Sh48.5 bilioni pekee.
Tanzanite huchimbwa eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.
Nchi za Afrika  Mashariki na DRC zimekubaliana kutumia Interpol kudhibiti biashara haramu ya dhahabu kutoka nchi hiyo.
chanzo:mwananchi.co.tz

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA