KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, UMAKINI UNAHITAJIKA KATIKA KUCHAGUA KIONGOZI BORA

MAANDALIZI ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu ni ya kipekee kutokana na kupambwa na mbwembwe nyingi ikiwamo misafara na maandamano makubwa ya wagombea urais. Ni jambo la kujivunia kuona kwamba wananchi wengi wameonyesha mwamko mkubwa wa ushabiki wa kisiasa.

Hadi sasa dalili za awali zinaonyesha kwamba ushindani mkubwa wa kinyang’anyiro cha urais utakuwa kati ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Misafara na maandamano makubwa ya wagombea urais hao vinazidi kuteka akili za wananchi wengi waliogawanyika katika makundi mawili yanayoelekea kulingana; kundi linalomshabikia Lowassa na jingine linalomuunga mkono Dk. Magufuli.

Kutokana na misukumo mikubwa ya hisia za kisiasa, kuna wananchi ambao ukiwambia kuwa Dk. Magufuli ndiye rais ajaye wanaweza kukutoa roho! Vivyo hivyo, wapo wengine ambao wakikusikia unasema njia ya Lowassa kuelekea Ikulu ni nyeupe wanaweza kukutenga katika jamii.

Ukiuliza sababu za wanaoamini kwamba Lowassa atashinda urais watakwambia ni misafara na maandamano makubwa ya watu wanaoonekana kumshabikia. Hata kwa upande wa Dk. Magufuli jibu ni hilo hilo!

Lakini kwa upande mwingine, wapambe wa Lowassa wanamuelezea kwamba ni mwajibikaji na mwenye uamuzi mgumu katika masuala ya umma, hivyo anafaa kukabidhiwa uongozi wa nchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania kiuchumi na kijamii.

Wengine wanaamini kwamba Dk. Magufuli ndiye anafaa kukabidhiwa mikoba ya Ikulu ya Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete. Kwamba mgombea huyo ni msafi asiye na kashfa za ufisadi, lakini pia hayumbishwi katika kusimamia misingi ya uwajibikaji kwa umma na kutetea maslahi ya Taifa.

Kimsingi hakuna wa kuwalaumu mashabiki wa pande hizo mbili maana wanatekeleza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ilmradi hawavunji sheria za nchi.

Lakini pamoja na haki hiyo, mashabiki hawa wanapaswa kutafakari vizuri juu ya misimamo yao ya kuamini kwamba misafara ya kifahari na maandamano makubwa ya watu ni kielelezo tosha cha ushindi kwa mgombea urais.

Si sahihi kutumia takwimu za idadi kubwa ya watu katika misafara na maandamano kuwa ndiyo kigezo cha ushindi kwa mgombea, maana mbwembwe za aina hiyo hazimchagui rais. Kinachomchagua rais ni kura zinazopigwa kwa utaratibu uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), si vinginevyo.

Tukumbuke kwamba mtu yeyote ana uhuru wa kushiriki maandamano ya wagombea urais, ubunge na udiwani bila kuulizwa kitambulisho. Lakini haruhusiwi kupiga kura za kuchagua viongozi wa nafasi hizo kama hana kitambulisho husika na iwapo atakiuka maelekezo ya NEC.

Hii ni sawa na kusema kwamba katika Tanzania hii, kila mtu, yaani mwenye kitambulisho cha kupiga kura, asiye nacho, mtoto na hata mgonjwa wa akili, wote wana uhuru wa kushiriki maandamano ya wagombea, jambo ambalo ni tofauti na utaratibu wa kupiga kura za kuchagua viongozi wa kisiasa.

Ikumbukwe hata wakati wa ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani hapa Tanzania Julai 2013 maelfu ya watu walijitokeza kumlaki, kumwona na kusikia anachosema, ingawa si kweli kwamba wote walikuwa wanampenda wala kumkubali na kumfurahia. Miongoni mwao walikuwapo wanafiki waliochukizwa na ziara hiyo wakiamini kimakosa kwamba alikuja kusaini mikataba ya kuuziwa nchi yetu!

Misafara na maandamano ya wagombea ni sawa na kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe wasiohitajika. Kuna watu wanashiriki misafara na maandamano ya aina hiyo wakiwa na dhmira ya kweli ya kuwaunga mkono wagombea, lakini wengine wanakwenda kufanya kazi zisizo za kisiasa kama vile kulinda usalama, kupiga picha, kurekodi video na sauti.

Kwa hiyo, kuamini au kujitumainisha kwamba idadi kubwa ya watu kwenye misafara na maandamano ya wagombea ndiyo kigezo cha ushindi, ni sawa na ndoto za mchana kweupe ambazo daima hazitimii.

Itakuwa jambo la maana kama mashabiki na wapambe wa kisiasa watazingatia umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kuza za kuwachagua wagombea wanaowataka kuliko kujiridhisha na wingi wa watu katika maandamano ambayo hayana nafasi ya kuchagua viongozi.

Kuamini kwamba idadi kubwa ya watu kwenye misafara na maandamano ya wagombea ndiyo kigezo cha ushindi ni dhana potofu na matokeo yake mwisho wa siku upande unaoshindwa katika uchaguzi hudhani umeibiwa kura, na wakati mwingine hugeuka kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani usiyo wa lazima.

Jambo la msingi zaidi kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ni kuongeza juhudi za kuhamasishana (kwa wenye vitambulisho waliojiandikisha kwenye dafrari la kudumu la wapigakura) kujitokeza kwa wingi kupiga kura za kuchagua viongozi tunaowataka siku ya Jumapili Oktoba 25, mwaka huu.

Sambamba na hilo, wananchi wote tunapaswa kushiriki mikutano ya kampeni za wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa ili kuwachuja na kubaini wanaofaa kutuongoza baada kusikia sera na ilani za vyama vyao.

Ingawa baadhi ya wananchi imani zao zimejikita kwenye vyama, lakini ni vizuri zaidi kuchagua mtu kwanza, chama baadaye kwa sababu maendeleo na mabadiliko tunayoyataka yataletwa na viongozi watu, siyo vyama ambavyo daima haviwezi kufanya chochote.

Lakini pia, tushirikiane kuuombea Uchaguzi Mkuu ujao baraka za Mungu ili ufanyike kwa uhuru na haki. Tuombe tukitambua kwamba mshindi wa uchaguzi huo atakuwa ni yule aliyepigiwa kura nyingi kwa utaratibu halali, si vinginevyo. Mungu ubariki Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015.

Imeandikwa na CHRISTOPHER GAMAINA

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA