RAIS ATEUA BALOZI, ABADILISHA WAWILI

RAIS amefanya uteuzi wa balozi mmoja na kubadilishia wengine wawili vituo vya kazi; mmoja akiwa ni Wilson Masilingi anayekwenda nchini Marekani.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Dar es Salaam jana, imetaja aliyeuteuliwa kuwa ni Charles Makakala anayekwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Kabla ya uteuzi huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makakala alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi.
Kwa upande wa Masilingi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, amehamishiwa Marekani kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Liberata Mulamula aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa.
Balozi Masilingi pia atakuwa anaiwakilisha Tanzania nchini Mexico.
Aidha, Balozi Irene Kasyanju aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi kushika nafasi inayoachwa wazi na Masilingi.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete amemteua rasmi Joseph Masikitiko kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Kabla ya uteuzi huo Masikitiko alikuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA