TAYARI 3 WAMEFARIKI KWA KIPINDUPINDU DAR, 34 WAMELAZWA

Watu watatu (wanawake 2, mwanaume 1) wamefariki dunia na wengine 34 wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na hospitali ya Mburahati jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kipindupindu.
Hospitali ya Sinza Palestina imeripotiwa kuwa na wagonjwa walio na dalili za ugonjwa huo zaidi ya 50.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Bw. Paul Makonda amezitaja Kata zilizoathirika na ugonjwa huo kuwa ni Kijitonyama, Kimara, Manzese, Tandale, Saranga, Makumbusho na Mwananyamala.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesema kuna ripoti ya wagonjwa waliolazwa 71 hadi sasa, na kwamba Wilaya ya Ilala na Temeke bado hazijakumbwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Minispaa hiyo, Dk. Aziz Msuya, amesema kuwa mgonjwa wa kwanza aligunduliwa katika maeneo ya Kijitonyama kwa Ally Maua na kufia nyumbani kwake katika eneo hilo na kuambukiza ndugu zake wawili ambao walikufa wakati wanapelekwa Hospitali
Dk. Msuya amesema kumetayarishwa kambi za muda katika Hospitali za Kijitonyama, Mwananyamala na Sinza Palestina pamoja na kambi kuu iliyopo katika Hositali ya Mburahati. Amewataka wananchi wa Jiji hilo kuchukua tahadhari kwa kuweka mazingira safi kunywa maji yaliyochemshwa na kujiepusha kula vyakula vilivyopikwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
“Ukipata huu ugonjwa tutakupa dawa lakini kwa sasa tumetoa dawa katika maeneo yale ambayo tumeona yameathirika zaidi ambayo ni Manzese na Kijitonyama. Tumeshazipa dawa kaya zile ambazo tunazitilia mashaka kwamba zinawezikawa zimepata maambukizi, na wale waliopo katika maeneo mengine ambayo sio maeneo hayo niliyokutajia hapo awali, wanapoona hizo dalili za kutapika na kuhara basi wafanye haraka kukimbia Hospitali.”
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini, Dk. Rufaro Chatora, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amethibitisha kupokea taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiijulisha WHO kuwepo kwa ugonjwa huo, na kwamba ugonjwa huo uliibuka tangu Agosti, 15, 2015.
Hata hivyo, ametaja maeneo yaliyobainika kuwa na wagonjwa hadi sasa kuwa ni Tandale, Kijitonyama, Saranga, Kimara, Manzese, Makumbusho na Mwananyamala.
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inafanya uchunguzi wa kina katika Wilaya ya Kinondoni ambayo ndiyo imeshambuliwa kwa sasa na ugonjwa huo kwa kasi ambapo pia timu hiyo itaendelea kutoa njia za kujikinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Musa Nati, amesema watu wengine ambao hadi sasa idadi yao haijathibitishwa wamethibitika kuugua kipindupindu na wamelazwa katika hospitali hizo za manispaa hiyo. Ameeleza kuwa wodi mbili zimetengwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya wagonjwa wenye dalili hizo.
Mathalani, amesema wameanza kuchukua tahadhari kwa kupuliza dawa katika maeneo yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Historia ya kipindupindu Dar es Salaam
Ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukiutesa mara kwa mara mkoa wa Dar es Salaam kila mwaka licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali licha ya kila mwaka ugonjwa huo ambao umekuwa ukilipuka na kuwaathiri watu wengi na wakati mwingine kupoteza maisha.
Mamlaka za serikali zimekuwa zimekaririwa mara kadhaa na vyombo vya haabri kuwa zinachukua hatua kwa kuweka tahadhari mbalimbali kwa lengo la kudhibiti kipindupindu. Miongoni mwa hatua hizo ni kuzuia mikusanyiko ya watu kama sherehe, misiba na unywaji wa pombe za kienyeji.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo na nyingine nyingi kumekuwepo na hatua ya upigaji marufuku uuzaji wa vyakula katika maeneo yasiyoruhusiwa hali ambayo inatajwa kusababisha ugonjwa huo wa kipindupindu kuendelea kuutesa mkoa huo kila mwaka.
Kufuatia hali hiyo, Halmashauri ya Jiji hilo, imelazimika kufungua kambi maalumu za kuhudumia walioathirika na ugonjwa huo, katika Manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala ili wanaporipotiwa wagonjwa wapatiwe tiba kwa haraka.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA