Utapeli wa nyumba za kupanga waibuka
Dar es Salaam. Umeibuka mtandao
wa matapeli jijini hapa wanaojifanya madalali wa nyumba na viwanja,
ambao wanatumia matangazo na namba za simu wanazoziweka magazetini
kuwanasa watu kwa urahisi.
Mtandao huo wa matapeli
unaoongozwa na mtu anayejifanya kuwa ni daktari katika Hospitali ya
Amana na mmiliki wa nyumba moja inayopangishwa iliyopo Mtoni Kijichi.
Polisi inamsaka mtu huyo baada ya kumtapeli mkazi mmoja wa Temeke.
Akisimulia
juzi namna alivyoangukia mikononi mwa mtandao huo na kutapeliwa Sh1.4
milioni za kodi ya nyumba, mfanyakazi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania
(Tea), Tito Mganwa alisema alikuwa akitafuta nyumba ya kupanga, ndipo
alipopiga simu za madalali alizoziona kwenye gazeti moja la kila siku
(siyo Mwananchi).
Mganwa alisema baada ya kupiga namba
hizo, aliambiwa kuwa daktari mmoja anayefanya kazi katika Hospitali ya
Amana anatafuta mpangaji kwenye nyumba yake iliyopo Mtoni.
Alisema
kwa kuwa alikuwa akihitaji kupata nyumba haraka, alikutana na madalali
hao na kwenda kuonyeshwa nyumba hiyo na kumkuta mlinzi aliyewatembeza
ndani ya nyumba.
Baada ya kuvutiwa na mazingira ya
nyumba yalivyo, Mganwa alimwambia mwenye nyumba kwa njia ya simu kuwa
atalipa kodi ya miezi sita kwa awamu mbili; awamu ya kwanza Sh1.4
milioni.
“Tulikubalina tukutane pale Hospitali ya
Amana, ambako anafanya kazi, nilikwenda na kumkabidhi fedha mkononi.
Nikiwa palepale alijifanya anampigia simu mlinzi na kumwambia afanye
usafi nyumba kwa vile tayari nilishalipa kodi,” alisema Mganwa.
Mganwa
alisema baada ya kulipa alikwenda kwenye nyumba ile ili kuifanyia
usafi, ndipo aliposhangazwa kusikia kuwa mlinzi hakuwa amepigiwa simu
kama mwenye nyumba alivyoagiza.
Alisema alikwenda kituo
cha polisi kuandikisha maelezo na kupewa RB ya kuwakamata matapeli hao,
kisha aliambatana na polisi hadi kwenye nyumba hiyo, lakini hawakumkuta
mlinzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta
alimtaka Mganwa kwenda ofisini kwake ili msako wa kumtafuta mwenye
nyumba hiyo ufanyike na pia kujua kama kuna matukio mengine yamehusisha
nyumba hiyo.
Comments
Post a Comment