Shamsa, Nay, siamini kama nyie ni wa kutafuta kiki! ...suala la mapenzi, si wa muziki wala filamu

 
WAANDISHI wa habari na mastaa wa fani mbalimbali duniani ni watu wa familia moja. Wanakutana, wanaongea na baadhi yao wanajenga urafiki mkubwa au hata kuoana. Kuna msururu mrefu wa mastaa walioingia katika uhusiano wa kimapenzi na waandishi au kujenga urafiki wa kindugu.

Ni rahisi kwangu kwa mfano, kukutana na staa yeyote mkubwa katika nchi hii kuliko inavyoweza kuwa hivyo kwa mtu mwingine. Hata kama sijawahi kukutana naye, ni kiasi cha kujitambulisha na kuomba miadi naye. Inaweza isiwe muda ule nitakao mimi, lakini mwishowe tutakutana na kufahamiana.

Inakuwa rahisi kwa sababu ni watu tunaotegemeana kikazi. Mimi nitahitaji kujua habari zake ili niihabarishe jamii kama ambavyo yeye atanihitaji mimi ili nipeleke ujumbe kwa mashabiki wake. Zipo baadhi ya nyakati unakutana na msanii kwa mfano, hajui namna gani atapromoti kazi yake, iwe nyimbo au filamu, hivyo kutokana na uzoefu unaweza kumpa mwongozo wa suala hilo.

Kifupi ni watu tunaoishi nao, tunajuana vizuri kiasi kwamba baadhi ya maandishi tunayosoma magazetini yakiwahusu, tunafahamu kama yako sawa au la.

Mkali wa kibao cha Muziki Gani, Nay wa Mitego na muigizaji nyota Shamsa Ford ni wapenzi kwa muda mrefu sasa. Mara kadhaa, wamekutwa pamoja nyumbani kwa Nay wakiwa katika hali isiyotia shaka kwamba wanapika na kupakua. Bahati nzuri, magazeti ya Global Publishers yameshawahi kuripoti mara kadhaa kuhusu jambo hili.

Lakini katika hali ya kushangaza kidogo, kwa nyakati tofauti, wawili hawa wamekuwa wakiripotiwa na vyombo vingine vya habari wakikana kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi, wakidai wao ni washkaji tu, wanaofanya ‘project’ moja kwa sasa.

Majuzi, waliibuka katika chumba chetu cha habari katika mahojiano maalum, wakatoa kioja baada ya kudai kuwa awali ni kweli walikuwa wakitoka pamoja, lakini kwa sasa kila mtu kivyake. Wakati wakitoa kauli hiyo, walipozi kwa namna ambayo wapenzi, hasa vijana wa umri wao, hupenda kupozi!

Sijaelewa kwa nini wanafanya hila hizi za kitoto.

Kuna msemo maarufu kwa wasanii wanaotumia kuwa kutafuta kiki, yaani kurejea midomoni mwa watu baada ya kuona hazungumzwi, hasa na media.

Sidhani kama Nay wa Mitego anahitaji kiki kwa kiwango alichofikia na wala simuoni Shamsa kama mtu wa kutegemea ‘kelele’ za vyombo vya habari. Ninafahamu uwezo wao kazini, ni wasanii wa daraja la juu kwa viwango vya wasanii wa Bongo!

Kukana kuhusu uhusiano wao, licha ya kusema ni kiki, lakini pia kunamaanisha aliyeandika habari hizo ni mwongo. Sasa kumuita mtu ambaye anafahamu nyendo zako za kila siku kuwa ni mwongo ni kumdhalilisha.

Wote wanajua, wasanii wetu hawajatulia linapokuja suala la mapenzi, si wa muziki wala filamu. Kama kukataa kwao kunataka kupanua wigo ili waendelee kuwapata wenza zaidi, hilo tunalikataa. Hatuwezi kukaa kimya mtu anapokanusha kitu anachojua ni cha kweli na bahati mbaya tukawa tumeandika kwenye magazeti.

Watu kujua kuwa Nay na Shamsa ni wapenzi, hakuwezi kuzuia wawili hao ‘kuchepuka’ kwa sababu tunao ushahidi wa wasanii walio katika ndoa wakizisaliti bila kificho. Na wala siyo jambo la ajabu kuwa na msururu wa mabwana au wanawake kama Kim Kardarshan alivyo.

Niwashauri Nay na Shamsa watafute kiki kwa kufanya kazi ambazo zitawafanya wasikauke kwenye vyombo vya habari.
CHANZO:GPL

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA