MADAI YA KUIBA: RASTAMAN ANASWA, ANYOLEWA!

Stori: Mwaandishi Wetu/Risasi Mchanganyiko
MWANAUME mwenye imani ya Kirasta ambaye jina lake halikuweza kunaswa mara moja, mwishoni mwa wiki iliyopita alijikuta akinyolewa rasta zake bila ridhaa yake kufuatia kudakwa akidaiwa kutaka kuiba kwenye duka moja.
Nywele za rasi zikiwa hatarini kuchezea wembe wa 'NACET' kama si 'GILLETE'
Tukio hilo lililokusanya watu kibao, lilijiri maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam chini ya jengo jipya la Wanyama.
Kwa mujibu wa mashuhuda, rastaman huyo alipofika kwenye duka hilo alijifanya kutaka kununua bidhaa mbalimbali kwa kuulizia bei zake lakini mtu mmoja dukani humo aliyekuwa akimlia ‘rada’ kwa mbali aligundua kuwa jamaa hakuwa mteja bali mkwapuzi.
“Ilikuwa kufumba na kufumbua, jamaa akiwa katika hatua ya mwisho kukwapua, akaitiwa mwizi na kudakwa hapohapo huku kipondo kikianza kumshukia mwilini.
“Alitolewa nje ya duka, watu wakajaa wakisema apigwe mawe hadi kufa, wengine apelekwe Kituo cha Polisi Msimbazi, lakini kuna mtu akasema hakuna haja ya adhabu zote hizo, kwa kuwa ana nywele za kirasta dawa ni kumnyoa.
'Rasi' akijaribu kujitetea ili wembe usiguse nywele zake.
“Huwezi amini, jamaa alijitetea kuwa yeye si mwizi lakini wembe wa Gillete ulinunuliwa, watu wakaanza kumnyoa nywele kwa kukata yale mabutu ya kirasta,” alisema shuhuda mmoja.
Mwisho wa tukio hilo, rasta huyo aliachiwa kwa vile iliaminika kuwa, adhabu aliyopewa ilimtosheleza kama si kumtia adabu.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wamiliki wa maduka Kariakoo alisema changamoto kubwa ya biashara maeneo hayo ni wizi wa mara kwa mara.
“Hapa tunaibiwa kila siku. Kuna siku tunawakamata siku nyingine wanafanikiwa bila kukamatwa. Wanatupa hasara sana hawa watu.



“Mfano akikuibia suruali ya shilingi elfu thelathini maana yake amekata faida ya suruali kama tano. Sasa hapo huo umeme wa Tanesco tutalipaje na vibarua tutalipaje?” alihoji mfanyabiashara huyo bila kutaja jina lake.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA