WATANO WAJERUHIWA KWA KURUSHIWA BOMU TANGA


Wakazi watano wa kitongoji cha Mafuriko Amboni kilichopo jijini Tanga wamejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili baada ya kurushiwa bomu la kutupwa kwa mkono na mtu asiyejulikana wakati walipokuwa wakitazama mpira kwenye banda la wazi.

Majeruhi hao ni Hassani Abdallah (72) ambaye amevunjika mguu wa kulia na kupata madhara makubwa kifuani na sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa ya Bombo. Wengine ni Rashid Ally (45), Mrisho Abdi (29), Juma Mtoo (15) na Abdul Ismail (19) ambao waliumia sehemu mbalimbali za mwili lakini baada ya kufikishwa Bombo wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha tukio hilo na kusema limetokea Januari 15 mwaka huu saa 3:00 usiku huko Mafuriko wakati waathirika hao walipokuwa ndani ya banda moja la kuonesha video.

“Ni kweli jana usiku huko Amboni Mafuriko katika kata ya Chumbageni kulitokea mlipuko wa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu,” “Bomu hilo lilirushwa majira ya saa 3:00 usiku kwenye banda la wazi la kuonyesha video ambalo ni mali ya Evarist Kingazi (82) na kusababisha majeruhi watano,” 
alisema.

Alisema uchunguzi wao wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni la kutengenezwa kienyeji kwa sababu askari waliofika eneo la tukio walifanikiwa kuokota mabaki yake ambayo yamejumuisha vipande kadhaa vya nondo na vibati vidogo vidogo. Kamanda Kashai alisema mkazi mmoja wa eneo hilo, Ally Rashid (25) anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano maalumu kuhusiana na tukio hilo.

  • HabariLeo

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA