BURUDANI MGANGA WA DIAMOND JELA MIAKA 7, HAKIMU ASOMA HUKUMU KIJASHO KIKIMTOKA!

Yule mganga aliyejitapa kumtengenezea nyota ya mvuto staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ustadh Yahya amehukumiwa kifungo cha miaka saba (7) jela baada ya kukutwa na hatia katika kisa cha kuchanganya akihusishwa na wizi wa gari.

Ustadh Yahya akiwa chini ya ulinzi.
TUJIUNGE MAHAKAMA YA WILAYA YA ILALA
Habari za uhakika zilieleza kwamba aliyehitimisha kesi hiyo ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar, Hassan Kisailo mapema Jumatatu wiki hii wakati jua la asubuhi likiwaka.
HAKIMU ASHUSHA MIWANI
Huku kijasho chembamba kikimtiririka huku akishusha miwani kidogo kuona wahudhuriaji wa kesi hiyo, Hakimu Kisailo alitoa hukumu hiyo kwa maelezo kwamba, mnamo Januari 20, mwaka jana, maeneo ya Kariakoo jijini Dar, Yahya alidaiwa kuiba gari aina ya Toyota RAV4 lenye namba za usajili T 139 BSJ likiwa na thamani ya Sh. milioni 12, mali ya Edrick Elieza.

Wakati Hakimu Kisailo akisoma hukumu hiyo, mshtakiwa na wadhamini wake hawakuwepo mahakamani hapo hivyo alisema mara tu baada ya hukumu wahusika hao watakamatwa ili wakatumikie adhabu inayowakabili.
MAPITIO MTIRIRIKO WA KESI
Huku akiangalia kulia na kushoto, Hakimu Kisailo alisema kuwa, baada ya kuupitia mtiririko wa kesi hiyo, alibaini kwamba ni kweli mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo hivyo alimhukumu kwenda jela miaka 7.
...Ustadh Yahya akilaumu yambo.
BOFYA HAPA KUMSIKIA HAKIMU
Kama ilivyo desturi ya Magazeti ya Global kutaka kujua vitu kwa undani, mwanahabari wetu alizungumza hakimu huyo kuhusiana na hukumu hiyo ambapo alishusha tena miwani kidogo kisha kumwangalia kwa juu na kusema:
“Ni kweli huyo mnayemuita sijui Mganga wa Diamond nimemhukumu kwenda jela miaka 7, ingawa hakuwepo hapa mahakamani.
“Nasikia alitoroka tangu alipowekewa dhamana lakini kifungo hicho kitaanza muda wowote atakapokamatwa.”
WADHAMINI NAO WANALO
Hakimu Kisailo alisema kwamba, Ustadh Yahya aliwekewa dhamana na watu wawili, Moses Msangi na Seme Kisusandi ambao wanatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja kila mmoja au kwenda jela miezi sita wakati sangoma huyo akisakwa.
Hakimu Kisailo alisema licha ya jamaa huyo kuingia mitini, wadhamini wake nao hawakuwepo mahakamani hapo na kusema kuwa mkono wa sheria ni mrefu utawafikia popote pale walipo.
MANENO KUNTU
Mmoja wa mashuhuda wa kike aliyekuwa kwenye chumba cha hakimu huyo alisikika akisema: “Huyo mganga wa Diamond hana lolote, iweje ashindwe kuzima kesi yake na kufikia hatua ya kuhukumiwa kifungo hicho wakati huwa anajidai ni mkali kwenye mambo ya kuwatengenezea watu nyota?
“Unaweza kukuta huko mitaani anajifanya kuwaambia wateja wake ana uwezo wa kuzima ‘makesi’ makubwa-makubwa kumbe hata kesi yake mwenyewe inamshinda.”
Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
DIAMOND ATUPIWA LAWAMA
Shuhuda huyo alikwenda mbele zaidi na kumtupia lawama Diamond kwamba alishindwaje kumsaidia mtu aliyempaisha hadi sasa hivi anawiki kimataifa?
DIAMOND ANASEMAJE
Amani lilimsaka Diamond ili kumfikishia ‘ubuyu’ kuwa mganga wake amehukumiwa miaka sasa jela lakini simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na hata alipofuatwa nyumbani kwake, Sinza-Mori, Dar, hakuwepo.
TUMEFIKAJE HAPA?
Ustadh huyo alidaiwa kukamatwa na gari hilo alilodai kufika mikononi mwake kutoka kwa mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Mwanahamis. Ustadh alikamatwa  akikatiza nalo Tabora mjini ndipo akawekwa nyuma ya nondo za mahabusu kabla ya kusafirishwa jijini Dar kwa hatua zaidi za kisheria ambazo zimemhukumu kifungo hicho. TUJIKUMBUSHE HUKO NYUMA

Stori: Richard Bukos/Amani/Global Publishers

EXCLUSIVE: MGANGA WA DIAMOND YAMEMKUTA


Stori: CHANDE ABDALLAH NA DENIS MTIMA/GPL
KIBAO kimegeuka! Yule mganga anayejitapa kumtengenezea nyota ya mvuto staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ustadh Yahya yamemkuta mazito.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa jamaa huyo anahenyeshwa na polisi akiwa mahabusu kufuatia madai ya wizi wa gari aina Toyota Rav 4 ‘milango mitatu’.
Kwa mujibu wa chanzo makini, gari hilo liliibwa wiki kadhaa maeneo ya Msimbazi-Kariakoo jijini Dar.
HABARI ZA AWALI
Habari za awali zilidai kuwa gari hilo lilifika mikononi mwa Ustadh kutoka kwa mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Mwanahamis ambaye ilisemekana kwamba alikuwa akichukua dawa kwa mganga huyo.
Ilidaiwa kuwa mwanamke huyo naye alihongwa gari hilo na mume wa mtu huku akiwa hajui kuendesha hivyo aliliweka poni kwa Ustadh ambaye alimpa dawa ambayo aliipeleka Kigoma kuwauzia watu wake.
Hata hivyo, ilizidi kudaiwa kwamba mwanamke huyo alichukua dawa za shilingi milioni 3 lakini akashindwa kurudisha fedha hizo na riba waliyokubaliana na mganga huyo.
Ikazidi kudaiwa kuwa, Ustadh alimuongezea dawa nyingine mwanamke huyo hadi kufikia deni la shilingi milioni 6 ndipo akaamua kulichukua gari hilo.

NI UZEMBE?
Ukiacha stori hizo za awali ambazo zilikosa ‘balansi’, kuna habari nyingine kuwa gari hilo mali ya Edric Magayane liliibwa baada ya kuachwa eneo la tukio likiwa ‘sailensi’ bila mtu ndani.
Ilielezwa kwamba aliyekuwa na gari hilo aliingia dukani kununua vitu na alipotoka alichanganyikiwa akidhani gari hilo lilikuwa limevutwa na watu wa ‘breki dauni’ waliokuwa wakivuta magari yaliyoegeshwa hovyo katikati ya jiji.
Habari zinasema kuwa mhusika alikwenda kulitafuta katika ‘yadi’ zinakopelekwa magari yaliyovutwa lakini hakuliona.


POLISI
“Alichokifanya ni kwenda kuripoti polisi ambao walianza kulisaka Dar bila mafanikio.
“Wakati polisi wakiendelea kulisaka kuna mtu akasema amemuona Ustadh akitanua nalo.
“Yule mwenye gari (Magayane) alimtafuta Ustadh hakumpata. Akaelekezwa nyumbani kwake, Kigogo Luhanga, Dar au Urambo, Tabora.
“Jamaa alipatafuta nyumbani kwa Ustadh, Kigogo hadi akafika akiwa na polisi waliovalia kiraia lakini hawakumkuta.

ALITAKA KULIRUDISHA?
“Waliambiwa amesafiri Tabora. Pia walihakikishiwa kwamba kweli Ustadh alikuwa na gari hilo. Jamaa akaambulia namba za simu.
“Alipompigia simu Ustadh alimwambia kama gari limeibwa ana uwezo wa kutumia uganga wake kulirejesha kwa kuwa ni mtaalam wa mambo hayo.
“Ustadh aliomba apewe fedha ili afanye mambo yake gari lirudi. Kweli alitumiwa fedha, lakini akawa anazungusha huku akijiita majina lukuki kama Maimuna na mengine,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

MKOKO WATAFUTIWA MTEJA
Baadaye polisi walifanya uchunguzi na kubaini kuwa, gari hilo lilikuwa likitafutiwa mteja mkoani Tabora lakini ilishindikana kutokana na kukosa ‘dokyumenti’ muhimu.

GARI LAKAMATWA
Habari zilizidi kutiririka kwamba, wakati Ustadh akikatiza na gari hilo Tabora mjini ndipo alipokamatwa na polisi kisha kuwekwa nyuma ya nondo za mahabusu kabla ya kusafirishwa jijini Dar kwa hatua zaidi za kisheria.

MASHITAKA MAWILI
Habari za uhakika zilieleza kuwa, Ustadh alipofikishwa Kituo cha Polisi cha Kati (Central), Dar alifunguliwa mashitaka mawili; wizi wa gari na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali.
Baada ya kujikusanyia habari hizo, juzi gazeti hili lilishuhudia polisi wakipekuwa nyumbani kwa Ustadh kisha kumrejesha kituoni kwa ‘difenda’ huku amepigwa pingu mikononi.

MMILIKI ANENA
Akizungumza na gazeti hili juzi, mmiliki wa gari hilo, Magayane alikiri maelezo yote juu ya habari hiyo.
Alipoombwa namba ya jalada la kesi aliitaja kuwa ni MS/RB/827/ 2014-WIZI WA GARI NA KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA ISIYO HALALI.
Jitihada za gazeti hili kuzungumza na Ustadh juu ya msala huo mzito ziligonga mwamba kwa kuwa simu yake ilikuwa haipatikani na bado alikuwa mahabusu huku ikelezwa kwamba soo limemkalia vibaya.

DIAMOND KAINGIA MITINI?
Kwa mujibu wa chanzo kingine, Diamond amekuwa akiombwa kumsaidia jamaa lakini akaingia mitini kwa madai kuwa hapendi kuhusishwa na Ustadh ambaye aliahidi msanii huyo kupata majanga makubwa baada ya kumkimbia na kwenda kwa waganga wengine.
Diamond alipotafutwa juzi kwa njia ya simu hakupatikana huku mmoja wa watu wa timu yake akisema yupo Afrika Kusini ‘Sauzi’ kwa ajili ya kufanya kolabo na D’Banj wa Nigeria.

CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA