JINSI YA KUTAMBUA MAGONJWA YANAYOATHIRI AFYA YA UZAZI
KUNA dalili nyingi za kugundua kama una magonjwa ambayo yanaathiri viungo vya uzazi kwa upande wa wanawake na wanaume.
Kwa upande wa wanawake, wanaweza kutambua kwamba wana ugonjwa ambao utaathiri afya ya uzazi kwa kutokwa na majimaji au ute kwenye uke. Wanawake wanapaswa kutafuta msaada wa kimatibabu wakigundua lolote kati ya haya yafuatayo:-
Majimaji ya ukeni ambayo yana harufu isiyo ya kawaida na yenye rangi tofauti na wingi kuliko ilivyo kawaida au kuhisi maumivu au kusikia kama unaungua au mwasho wakati wa kwenda haja ndogo.
Dalili nyingine ya kupata maradhi haya ni kusikia maumivu na muwasho katika maeneo ya uke au maumivu ukeni wakati wa kukutana faragha.
Wanawake wengine watatambua kuwa wana magonjwa hatari kwa kutokwa na vidonda na malengelenge katika eneo la uke. Kumbuka, baadhi ya maambukizi huenda yasiwe na dalili, hivyo kama una wasiwasi au umetokewa na dalili hizi ni vyema kuchunguzwa na daktari haraka iwezekanavyo, ama kwenda katika kliniki.
DALILI KWA WANAUME
Mwanaume anaweza kupata magonjwa yanayoweza kuathiri viungo vyake vya uzazi na dalili zake ni hizi zifuatazo.
Majimaji kutoka uumeni ambayo yana harufu isiyo ya kawaida, au yakiwa mengi, kuhisi mwasho ndani ya uume, wakati na baada tu ya kwenda haja ndogo au kutokwa na vijidonda au malengelenge juu au katika sehemu za kiume.
Wengine wanatokwa na vipele au uvimbe katika sehemu za siri.
Kila mtu awe mwanaume au mwanamke ambaye ataona dalili zilizotajwa hapo juu ili kugundua ugonjwa ni lazima aende kuonana na daktari na kufanyiwa vipimo.
USHAURI
Hata hivyo, kila mtu akumbuke kuwa maambukizo mengine kama ya Virusi Vya Ukimwi yanaweza kuwemo mwilini kimyakimya kwa muda mrefu bila dalili zozote kujitokeza. Unaweza usione dalili yoyote kwanza, lakini haimaanishi kwamba huwezi kuwaambukiza wengine.
Kama umefanya mapenzi bila kutumia kinga na una wasi wasi huenda umeambukizwa, nenda ukafanyiwe uchunguzi na daktari lakini pia kama umefanya mapenzi wakati una dalili hizi nenda wewe na mpenzi wako ukapimwe na ikigundulika una ugonjwa unaohusiana na magonjwa ya zinaa, utatibiwa kwani maradhi haya huathiri sana viungo vya uzazi ikiwa hujapata tiba mapema na magonjwa hayo mengine yanaweza kusababisha usipate mtoto.
Comments
Post a Comment