WAZIRI SITTA AMSIMAMISHA MKURUGENZI TPA, ATEUA MWINGINE AUNDA TIMU YA UCHUNGUZI

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uendeshaji mbovu wa utoaji wa zabuni.

Aidha, amemteua Awadhi Massawe kushika wadhifa huo. Kabla ya uteuzi huo, Massawe alikuwa Meneja wa Bandari.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sitta alisema uamuzi huo umetokana na kuwapo malalamiko ya kutofuatwa kwa taratibu za zabuni na ucheleweshaji wa barua kwa wanaoshinda.

“Ni muhimu sana taratibu zetu za ununuzi katika bandari ziwe wazi na ziheshimike duniani kote, maana miradi hii ni mikubwa sana inayopitishwa na bodi ya zabuni ya TPA,” alisema.

Sitta alisema, aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dk Harrison Mwakyembe alianza kushughulikia masuala hayo, lakini hayajakaa vizuri. Alisema hakuna uwazi na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, ikiwemo kubadilika majina ya kamati za kutathmini zabuni.

Wakati huo huo Sitta ameunda timu ya watu sita itakayochunguza tuhuma za Kipande. Imepewa wiki mbili iwe imefanya kazi hiyo.

Timu hiyo itaongozwa na Jaji mstaafu, Augusta Bubeshi na Katibu wake, Deogratius Kasinda ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi.

Wajumbe wengine wa timu hiyo ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ( PPRA) Dk Ramadhani Mlinga, Samson Lugigo , Happiness Senkoro na Flavian Kinunda ambao walishawahi kushika nyadhifa za juu ndani ya TPA.

“Nimejitahidi kuchukua hawa wastaafu kwa sasa hivi hawatafuti cheo chochote, naamini watatenda haki, watachunguza tu bila kufanya uonevu,” alisema Sitta.

Waziri Sitta alisema bandari ni eneo muhimu, kwani takwimu zinaonesha kwamba asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yanatokana na kodi ya ushuru wa forodha. Kati ya makusanyo hayo, asilimia 87 yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa Kipande, alisema hawezi kupinga hatua iliyochukuliwa na Waziri .

Hata hivyo, alisema anaamini kipindi chote cha uongozi wake, alifanya ambayo yalikuwa sahihi na hana wasiwasi na uamuzi huo.

"Mimi sina wasiwasi na hilo sababu huo ni uamuzi wake; lakini nina imani kuwa katika bandari hii, nimefanya kile ambacho nilikuwa natakiwa kufanya, hivyo sina shaka na hilo," alisema Kipande.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto ametaka serikali kujenga matangi ya kuhifadhia mafuta na kujenga bomba la mafuta kwenda mikoani.
Aidha, kamati hiyo imetaka TPA kuangalia uwezekano wa kununua hisa 50 za Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (Tiper) imilikiwe kwa asilimia 100 na Serikali.

Kuhusu ujenzi wa matangi, Zitto alisema hatua ya Serikali kujenga matangi yake ya kuhifadhi mafuta, itasaidia kujua kiasi cha mafuta yanayoingia na kuweza kukadiria kodi kwa uhakika.

Akitoa mfano wa Kenya, alisema Serikali inamiliki matangi ya kuhifadhia mafuta, wanayapima kujua kiasi cha mafuta kilichoingia na kukitoza kodi kabla ya kupelekwa kwenye matangi ya waagizaji.

“ Walichofanya, wamemtaka kila muagizaji kuwa na flow meter yake na yakitoka kwenye meli yanaingia kwenye matangi ya Serikali na baada ya kujua kiasi na kutozwa kodi hupelekwa kwa walionunua,” alisema.
Zitto alisema wakati umefika sasa kwa serikali kujenga mabomba ya kusafirishia mafuta na kwa kuanzia yakawa matatu, ambayo yatasaidia kuondoa mfumo wa sasa wa kusafirisha kwa magari.

“Linaweza kujengwa bomba moja kwenda Mbeya, likawa na matoleo kwa ajili ya mikoa ya Morogoro, Iringa na mikoa iliyo jirani, kwa kufanya hivyo tutaondoka na hali ya sasa ya kusafirisha mafuta kwa magari,” alisema.

Alisema katika kuimarisha reli, ni vyema ukaanzishwa mfumo wa kutoza kodi asilimia 1.5 kwa kila bidhaa inayoingia nchini na fedha hizo ziimarishe usafiri wa reli.

“Kwa sasa asilimia 99 ya mizigo inasafirishwa kwa barabara, hili si jambo jema kwa uchumi, najua nikisema hivyo wenye malori watalalamika, lakini wanaweza kufanya biashara nyingine,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe alisema asilimia 60 ya mafuta yanayoingia nchini hupitia kwenye boya la Single Buoy Mooring (SBM).

Alisema wamejipanga kujenga mita ya kisasa ya kupimia mafuta maeneo ya Kigamboni huku ile ambayo haitumiki, wamepanga kuiboresha na kuwa ya kisasa.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 ambazo zabuni yake iliingia utata, Massawe alisema ripoti ya maandishi wataipeleka kwa Kamati hiyo ya Bunge ifikapo Machi Mosi mwaka huu.

Pia, Massawe alisema hatua ya kitengo cha kupakua kontena kupewa mtu binafsi, inawapunguzia mapato na kuwa hiyo ndio sekta ambayo inaingiza fedha nyingi.

Alisema ili kupambana na hali hiyo, wamejipanga kuimarisha gati namba 1 hadi 7 na kuongeza kina cha bahari ili kuweza kupakua makasha na kuwa kwa mwaka jana waliweza kupakua makasha laki mbili.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta akizungumza na wanahabari leo bandarini) amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eng Madeni Shamte Kipande kwa tuhuma za utendaji mbovu, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa uwazi kwenye mamlaka hiyo hususani katika michakato ya zabuni mbalimbali zinazotangazwa na mamlaka hiyo.
(picha: Francis Dande)

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA