USHINDI WA CHADEMA SUMBAWANGA, VIGOGO CCM TUMBO JOTO


Kufuatia ushindi wa kishindo walioupata Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema) katika uchaguzi wa marudio wa serikali za mitaa uliofanyika wiki hii katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mkoa na taifa, wanadaiwa kuhaha huku na kule ili kujua chanzo cha kushindwa huko.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, ushindi huo umewavuruga mno viongozi wa CCM kwani wako tumbo joto na hawakutegemea kuanguka vibaya kama ilivyotokea na vikao mbalimbali vya chama vinaendelea mjini Sumbawanga, kujaribu kutafuta sababu na kurekebisha makosa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, Oktoba 2015.

“Wameanguka vibaya mno, yaani katika mitaa 43, CCM wameambulia viti vitano tu wakati Chadema wamechukua 37 na mtaa mmoja uchaguzi utarudiwa tena, hii haijawahi kutokea. Hivi sasa hapa Sumbawanga hapakaliki, vikao vya CCM kila dakika, wamechanganyikiwa kwa kweli,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina.

Baada ya kupata habari hizo, mwandishi wetu alimtafuta katibu mwenezi wa CCM wa wilaya hiyo, Clement Bakuli ambaye alisema wameyapokea matokeo hayo kwa masikitiko makubwa, lakini katika mpambano wowote lazima mshindi apatikane, hivyo chama kinafanya tathmini kuona wamekosea eneo gani ili waweze kujirekebisha kwenye uchaguzi ujao.

CHADEMA WACHEKELEA
Wakati CCM wakihuzunishwa na matokeo hayo, hali ni tofauti kwa Chadema ambao wameupokea ushindi huo kwa shangwe kubwa na kujigamba kwamba hiyo ni dalili ya anguko la CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumzia matokeo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema: “Ushindi huu mkubwa ni mwendelezo wa anguko la CCM na ni motisha kuelekea hatua ya Ukawa ya kutoshiriki kura ya maoni na badala yake kuelekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka huu.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Mabere Marando alisema: “Watu wameelewa ubaya wa CCM, sishangazwi bali nawapongeza watu wa Rukwa kwa kujua kuwa CCM imewanyima maendeleo kwa miaka 53 tangu kupata uhuru.
“Naamini sehemu nyingine nchini watu watafanya hivyo kwenye uchaguzi mkuu ujao. Huu ni wakati wa kufanya mabadiliko kwa kuiondoa CCM kwa nguvu ya umma.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Taifa wa CCM, Nape Nnauye alipopigiwa simu na mwandishi wetu, alisema kwa wakati huo hakuwa na nafasi ya kuzungumzia hilo, akaahidi kuwasiliana na mwandishi wetu baadaye lakini hakufanya hivyo mpaka tunakwenda mitamboni.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA