MAKALA: HAWA WENYE TAALUMA YA KUTEGEMEA SAUTI KUTANGAZA HAWANISUMBUI: MMLIKI

Makala hii imetoka gazeti la kiongozi....soma...soma...tuwakomboe waandishi....
Title, "Hawa wenye taaluma ya kutegemea sauti kutangaza hawanisumbui: Mmiliki". 

Denis Mpagaze
“Hawa watu wenye taaluma ya sauti nzuri wako wengi, wala hawanisumbui kichwa. Unafukuza mmoja asubuhi, jioni umeshapata wengine wengi tu” ni maneno yenye dharau, kiburi na majivuno kutoka kwa mmiliki mmoja wa vyombo vya habari hapa nchini akijidai kutowalipa waandishi wake kwa madai ya kwamba hata wakiacha kazi atapata wengine. Mwandishi wa habari anakaa mpaka miaka mitatu hajui pesa ya mwajili wake, pamoja na kufanya kazi kila siku na kwa bidii.Lakini hata wale waliobahatika kulipwa hawalipwi kwa wakati.


Huu ni ukatiri!Wakati wenzetu katika nchi zilizoendelea wanapima uandishi wa habari kwa uwezo wa mwandishi, huku kwetu wamiliki wanajua mwandishi wa habari ni kuwa na sauti nzuri na sura ya kuvutia (beuty). Ni upumbavu uliboreshwa kufikiri uandishi wa habari ni sauti na sura nzuri.

Upumbavu huu ndiyo pengine unampa kiburi mmiliki huyu kusema hana muda wa kupoteza na wanataaluma wanao tegemea sauti. Sasa kunaredio pia sitoitaja, mmiliki wake alitia fora. Yeye alidiriki kuwaambia waandishi wake anayeona ameshindwa kufanya kazi hapa aondoke kwani hawamtishi kitu kwa sababu ana wanakwaya wa kutosha wanaweza kutangaza. Na kweli waandishi wale walipoondoka, jioni wanakwaya walianza kutangaza. Huu ni ubakaji wa taaluma ya habari!


Wakati nchi zilizoendelea wanafanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari kwa maendeleo ya jamii,huku kwetu wamiliki wanawatumikisha waandishi kwa ujira wa hovyohovyo zaidi ya ule waliokuwa wanapewa manamba kwenye mashamba ya mkonge huko Tanga. Yaani mwandishi pamoja na kusaga soli ya kiatu na kupigwa jua kali anaishia kulipwa shilingi 5000 kwa kila habari inayotoka? Huu ni ujambazi na uuaji!
Wakati katika nchi zilizoendelea waandishi ndiyo msingi wa demokrasia ya kweli kwani kupitia vyombo vya habari jamii inaweza kupaza sauti dhidi ya maovu, huku kwetu wamili wamewafanya waandishi kuwa waoga kujisemea na kuisemea jamii yao. Wakijaribu kufungua midomo na kudai haki zao, wanakumbana na vitisho lukuki ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kwa ‘message’ za simu, pasipo kujieleza (Natural Justice). Sijui kama Umoja wa Klabu za Habari Tanzania (UTPC) na Baraza la Habri Tanzania (MCT) waliojipa dhamana ya kutetea tasnia ya habari wanaliona hili au ndiyo njia nyingine ya kujinufaisha kwa jina la waandishi. Huu ni ukoloni!
Wakati nchi zilizoendelea wanawawezesha waandishi wa habari kuifuata habari popote pale ilipo,na kwa gharama yoyote, huku kwetu wamiliki wameruhusu waandishi wa habari kuwa kama kuku wa kienyeji. Anashinda jalalani kutwa nzima akijitafutia chakula lakini mwisho wa siku kila mtu anataka kufurahia mayai yake. Mwandishi mmoja anasema alipojaribu kuomba malipo yake, mmiliki alimjibu hivi, “Yaani wewe kuonekana kwenye Luninga ukitangaza habari masaa mawili tu kwa siku ni mshahara tosha. Tumia nafasi yako vizuri”. Hii inamaana gani kama siyo kumfanya mwandishi awe anawinda semina na warsha ili apate mshiko? Aibu gani hii kwa wanataaluma wa habari jamani?
Wakati nchi zilizoendelea mwandishi wa habari akimfuata ‘source’ , source anawaza atamjibu nini mwandishi, huku kwetu source anajiuliza atamlipa shilingi ngapi. Nakama wahenga walivyosema “anayemlipa mpiga zumari ndiye huchagua wimbo” kadhalka ‘source’ ataamua ni aina gani ya habari iandikwe. Hali inakuwa hivi kwa sababu wamiliki wa vyombo vya habari wameshindwa kutambua thamani ya mwandishi wa habari. 


Wakati nchi zilizoendelea huwapatia waandishi vitendea kazi vizuri na vya kisasa ili kufanya kazi iliyobora na kuonesha umahiri katika taaluma yao kama afanyavyo Salim Kikeke wa BBC, huku kwetu wamili huwapatia waandishi vitendea kazi duni na kuwataka wafanye kazi nzuri. 


Mwandishi anaposhindwa kufanya kazi vizuri, anasimamishwa kazi na kutakiwa ajieleze na wakati sababu inajulikana. Huu ni udhalilishaji wa taaluma ya habari!
Wakati nchi zilizoendelea waandishi wa habari hufanya kazi kwa kushirikiana na serikali zao kwa maendeleo ya wananchi, huku kwetu waandishi wa habari na serikali yao ni kama paka na panya. Yaani mpaka leo bado kunamasheria kandamizi ya toka enzi za ukoloni bado yanatumika kuminya uhuru wa habari na wanahabari. 


Pengine ni mkakati nchi iwe na vyombo vya habari dhaifu kwa sababu waandishi makini huwa ni mwiba kwa utawala wenye mashaka. 

Wakati vyombo vya habari katika nchi zilizoendelea hufanya kazi kama mhimili wa nne wa dola, huku kwetu waandishi wamefanya vyombo vya habari kama biashara. Wanathamini sana watoa matangazo zaidi ya waandishi wa habari.


Siku moja mwandishi mmoja anakuja na habari ya uchunguzi kuhusu uozo wa kampuni moja jijini Mwanza. Alichokuja kujibiwa na mmiliki wake alibaki mdomo wazi “ hivi nikikosa hela ya matangazo utaendesha kituo changu?”
Wakati nchi zilizoendelea wanafanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari kwa maendeleo ya jamii, hapa kwetu waandishi wanaonekana kama watu wababaishaji wasio na mchango wowote.


Wanafanyishwa kazi zaidi ya punda na mwisho wa siku wanaishia kutukanwa na kunyimwa ujira wao kiduchu. Nasema ujira wao kiduchu kwa sababu wengi hawalipwi mishahara. 

Mwandishi mmoja juzi kipindi natoa paper pale Mwanza kuhusu mchango wa waandishi wa habari katika kupambana na dawa za kulevya, alijitambulisha kama kibarua wa Daily News. Nilijiskia vibaya. Yaani mwandishi msomi na mfanyakazi wa muda mrefu kujiita kibarua? Inafedhehesha. 

Kwa sababu ya roho mbaya, ukatiri na ushenzi wa wamiliki wa vyombo vya habari Tanzania, taaluma ya habari imebaki kuwa kimbilio la wasio na taaluma bora. Naskia jamaa mmoja katika kituo kimoja hapa nchini baada ya kuwa mtuma salam bora sasa amekuwa mtangazaji.


Kwa sababu ya ubabe wa wamiliki, waandishi wa habari wengi wamekuwa ‘majambazi’, matapeli na wala rushwa kwa kutumia mbinu ya “blackmail”. Kunawaandishi leo hii hawafanyi kazi katika chombo chochote kile lakini wanazunguka mjini na kunusa ni wapi kunaskandali ili watishie kulipua. Hapo sasa mhusika kinachofuata ni kutoa dau, na dau linatoka. ‘Ndo habari ya mujini’. 


Ndugu zangu waandishi wa habari, mstakabali wa taaluma yetu uko mikononi mwetu, bila kuungana na kuwa kitu kimoja, tutaishia kuwa mamluki na kushindwa kuitumikia jamii ipasavyo. Hebu tuamke, jamii bado inatuhitaji. 


Mwandishi ni Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari SAUT-Songea. Anapatikana kwa denis_mpagaze@yahoo.com, 0753665484

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA