RAIS KENYATTA ATAKIWA KUFIKA ICC
Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC, inamtaka
Rais Uhuru Kenyatta kufika Hague tarehe 8 mwezi Oktoba. Hii ni licha ya
majaji wanaotarajiwa kusikiliza kesi dhidi yake kuiahirisha.
Kesi dhidi ya Kenyatta ilitarajiwa kuanza Oktoba tarehe 7.
Katika
taarifa ya mahakama hiyo, kutakuwepo na mikutano miwili ya hadhara
kujadili hali ya ushirikiano kati ya kiongozi wa mashitaka na serikali
ya Kenya kuhusiana na kesi hiyo.
Swala hilo liliibuka katika taarifa ya
kiongozi wa mashitaka iliyotolewa Septemba tarehe 5.
Katika
taarifa yake, mahakama imesema kuwa mwakilishi wa Rais Kenyatta
atahitajika kuhudhuria mkutano wa kwanza huku Rais Kenyatta akitakiwa
kuhudhuria mkutano wa pili utakaojadili hali ya kesi yake.
Vikao
hivyo viwili, vitashirikisha kiongozi wa mashitaka, upande wa utetezi na
mawakili wanaowawakilisha waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi
mkuu mwaka 2007/08.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mahakama iliamua
kuahirisha kesi dhidi ya Kenyatta ili kujipatia muda zaidi kutafakari
maombi yaliyotolewa na pande zote kwenye kesi hiyo bila ya kuonea au
kupendelea upande wowote.
Rais Kenyatta ameshitakiwa kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mnamo mwaka 2007/08.
Anakabiliwa
na makosa matano ya kutenda uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji,
kuwalazimisha watu kuhama makwao , ubakaji na vitendo vingine
vinavyokwenda kinyume na haki za binadamu.
Inadaiwa yote hayo aliyafanya wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007-2008.
Comments
Post a Comment