PAKA AFUNGIWA HIRIZI MTINI

Tukio hilo lililokusanya umati mkubwa wakiwemo waumini wa msikiti huo lilitokea alfajiri ya Alhamisi iliyopita ambapo…
Stori: Dustan Shekidele, MOROGORO
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida, paka mwenye hirizi kubwa shingoni akiwa hai alikutwa amepigiliwa misumari juu ya mti uliopo jirani na Msikiti wa kwa Mtawara uliopo Kata ya Mwembesongo mkoani hapa.
Paka mwenye hirizi kubwa shingoni akiwa amepigiliwa misumari juu ya mti uliopo jirani na Msikiti wa kwa Mtawara uliopo Kata ya Mwembesongo, Morogoro.
Tukio hilo lililokusanya umati mkubwa wakiwemo waumini wa msikiti huo lilitokea alfajiri ya Alhamisi iliyopita ambapo baadhi ya waumini wa msikiti huo walikuwa wamefika msikitini kwa Swala ya Alfajiri.
Baadhi ya waumini wa msikiti huo walipohojiwa na mwandishi wetu walisema alfajiri hiyo walisikia sauti ya paka akilia kutoka kwenye mti huo uliopo kandokando ya Barabara ya Mtawara inayoelekea Kichangani na Mji Mpya.
Watoto wakishudia tukio hilo la kushangaza.
“Tulifika hapa msikitini kwa lengo la kuswali Swala ya Alfajiri kwa kuwa bado kulikuwa na giza hatukuweza kumwona, lakini tulisikia akilia kwa kupiga kelele mfululizo.
“Tuliposogelea tulimwona akiwa juu ya mti huku amevishwa hirizi kubwa ya rangi nyeusi. Haya ni mambo ya kishirikina, tena tuna wasiwasi hata wa maisha yetu.
“Unajua eneo hili lina miti mingi lakini wahusika wamekuja kumpigilia misumari paka huyu hapa. Mimi nasema wasakwe hawa watu tuwajue,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Said.
Umati wa watu wakishudia tukio hilo linalohusishwa na ushirkina.
Naye mjumbe wa kamati ya utendaji ya msikiti huo, Haji Said Dihole alipohojiwa na mwanahabari wetu alisema:
”Kama kuna mtu alitaka kutujaribu angemuweka paka huyo kwenye eneo letu la msikiti angeipata habari yake, pia nasikia tukio kama hili liko kwa majirani wetu pale Kanisa la T.A.G Mwembesongo, nenda kashuhudie.”
Paka huyo baada ya kutolewa mtini.
Baaada ya kupata taarifa hizo, mwandishi wetu alifunga safari hadi kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of  God ‘T.A.G’ linalofahamika kwa jina la Bethel Revival Temple lililopo Mwembesongo.
Mwandishi wetu hakumkuta paka lakini wananchi wa eneo hilo walipoulizwa walikiri kuwepo kwa paka huyo kwenye mtaa huo lililopo kanisa hilo lakini aliondolewa.
Baadhi ya wananchi wakimwangalia paka huyo kwa karibu zaidi.

Haikufahamika mara moja mtu aliyeamua kuweka paka hao kwenye maeneo ya jirani na nyumba za ibada alikuwa na malengo gani.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA