VIDONDA VYA TUMBO VINAVYOWATESA WATU WENGI BILA KUFAHAMU


Vidonda vya tumbo ni ugonjwa unaowasumbua watu wengi,  wanaume na wanawake na hata watoto wadogo. Tatizo hili husumbua sana na kumfanya mgonjwa asiweze kumudu shughuli zake za kila siku.

Ugonjwa huu huathiri kwa ujumla katika suala zima la afya.
Tatizo hili huanza taratibu na dalili za awali huwa hazionyeshi kama mtu ana ugonjwa huu.

Chanzo cha ugonjwa
Ugonjwa huu hutokana zaidi na maambukizi ya bakteria waitwao ‘Herictobacter Pylori’ au maarufu kama H. Pylori  hushambulia tabaka la ndani la tumbo.
Aina hii ya bakteria ni wagumu kufa kwa kuwa wana uwezo wa kuishi kwenye  mazingira ya tindikali tumboni. Tumboni kuna tindikali ya Hydrochloric Acid ambayo husaidia katika mmeng’enyo wa chakula.
Bakteria hawa wanaposhambulia tabaka la ndani la kizazi, hutegemea vishimo vishimo ambavyo ni vidonda hivyo tindikali inapotoka huchoma kwenye hivyo vidonda na kumfanya mgonjwa ahisi maumivu makali.

Aina za vidonda vya tumbo
Vidonda vya tumbo vipo vya aina mbili, kwanza ni vile vilivyopo mwanzoni mwa tumbo la chakula, Gastric Ulcers na ya pili ni Duodenal Ulcers katika sehemu ya pili ya tumbo. Maumivu na dalili za aina hizi mbili hufanana sana.
Ili kutofautisha aina hizi za vidonda, vipimo maalum hufanyika kama vile ‘OGD” na “Barium Meal’, vipimo ambavyo hufanyika katika hospitali za rufaa.

Dalili za ugonjwa
Hapa tutazungumzia dalili kuu za vidonda vya tumbo kwa ujumla. Mgonjwa wa vidonda vya tumbo katika hatua za awali huwa hajigundui kama ana tatizo.

Mgonjwa hulalamika kuhisi homa za mara kwa mara na kujihisi kama ana malaria au homa ya tumbo ‘Taifoidi’, wengine hulalamika kutumia sana dawa za taifoidi lakini hakuna nafuu.
Mwili unanyong’onyea, maumivu ya viungo, kuhisi baridi kuumwa kichwa na tumbo kujaa gesi.

Mgonjwa pia hulalamika maumivu ya tumbo eneo la chembe ya moyo ambapo ni chini ya kifua na juu ya kitovu.
Maumivu ya muda mrefu husambaa tumbo lote na tumbo huunguruma mara kwa mara .

Maumivu ya chembe ya moyo yaani chini ya kifua na juu ya kitovu husambaa hadi kifuani na kuzunguka mpaka mgongoni.

Mgonjwa hulalamika kuhisi moto kifuani na maumivu yaani kiungulia. Akilala usiku hali ya moto huongezeka na mgonjwa akicheua hutoa majimaji ya moto na machungu.

Mgonjwa hupata choo kigumu na vipande vipande kama cha mbuzi na wakati mwingine huwa cheusi.
Mgonjwa hupoteza hamu ya kula na wakati mwingine hutapika damu. 

Macho hupoteza nguvu ya kuona kwa kuwa muda wote anakuwa na maumivu, mwili unachoka na anakosa raha kutokana na kuwaza sana juu ya maumivu anayopata kiasi cha kumfanya mgonjwa akonde.
Mkojo unakuwa wa njano sana, hufunga kupata choo kikubwa na kusababisha maumivu ya kiuno kwa ndani ambayo husambaa hadi miguuni. Hamu ya tendo la ndoa pia hupotea.

Uchunguzi wa ugonjwa
Uchunguzi wa awali hufanyika katika vituo vya afya na hospitali za wilaya, mikoa na rufaa. Ni ugonjwa unaotibika hospitali na  vipimo ni kama Ultrasound, OGD, Barium Meal na vipimo vya damu ili kuangalia maambukizi ya H. Pylori na wingi wa damu.
Choo kikubwa pia kitapimwa. Ni muhimu pia kuangalia matatizo mengine kwa undani. Kipimo cha OGD ambacho kitapitishwa katika mfumo wa chakula kitasaidia kutoa majimaji yatakayopimwa maabara.
Ushauri
Ni vema mgonjwa azingatie kuhudhuria hospitali kwani ugonjwa wa vidonda vya tumbo huchunguzwa na kutibiwa hospitali ingawa tiba huchukua muda mrefu.

Ugonjwa huu dalili zake zinafanana sana na saratani au kansa ya tumbo hivyo ni vizuri uwahi hospitali ili ugundulike mapema.Unaweza ukawa unatumia dawa nyingine pasipo uchunguzi wa kidaktari mwishowe ukajikuta tayari hali inakuwa mbaya na kusababisha utumbo kutoboka au kansa.
 
CHANZO: GLOBALPUBLISHERS

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA