‘Kampuni za simu nchini zinawaibia wateja wao’
Makamba alikiri hilo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji.
Haji alisema wizi huo si mkubwa kama uliofanyika
kwenye Escrow, bali ni wizi mdogo ambao wateja wanaibiwa Sh2,000 au
3,000 katika simu zao.
“Mpemba wa Konde akiibiwa Sh3,000, Mnyamwezi
aliopo Tabora akiibiwa 2,000 ukizijumlisha ni mamilioni wanaibiwa
Watanzania,” alisema.
Alihoji Serikali inafikiriaje kuhusu gharama za kwenda kutoa malalamiko yao katika Mamalaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA).
Pia alitaka kufahamu ni nani aliopo nyuma ya pazia hilo au CCM ina fungu katika wizi huo?
Akijibu, Makamba alisema CCM haihusiki na wizi huo
unaotokana na kampuni za simu na kwamba chama hicho ni kizuri, makini
na kimekuwa kikiaminiwa na wananchi.
“Napenda nikiri dhahiri tatizo la wizi na dhuluma
lipo na ni kubwa na ndio zilisababisha tukaweka kanuni na hatua za
kuchukua katika kudhibiti wizi huo,” alisema.
Pia alisema wateja wa vijijini hawawezi kufuatilia
madai yao hadi Dar es Salaam, hali ambayo imeifanya Serikali kuanzisha
kituo cha kushughulikia malalamiko hayo.
“Sheria inazitaka kampuni kuweka huduma kwa
wateja, lakini wakati mwingine utaratibu huo una matatizo, unaweza
kupiga simu hazipokewi, unaweza ukaambiwa usubiri lakini wakati
ukisubiri unakatwa,” alisema.
Alisema katika kituo walichokianzisha, kutakuwa na
namba ya bure ya kupiga simu, hali itakayomrahisishia mteja kusafiri
hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kulalamika.
Alisema kituo hicho kitakuwa wazi saa 24, mteja atapewa namba atakapotoa lalamiko lake ili lishughulikiwe
- Mwananchi
Comments
Post a Comment