AJIRA MPYA ZA WALIMU MEI

jumanne-saaginii_300_179_75b90.jpg
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini
SERIKALI imesema ajira za walimu wapya zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku ikiweka wazi kuwa walimu hao wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea kupangiwa katika maeneo hayo kutokana na idadi ya walimu waliopo ni kubwa na inakidhi mahitaji, huku maeneo yaliyopewa kipaumbele ni vijijini na halmashauri ambazo zina mahitaji na upungufu mkubwa wa walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira zao mwezi ujao ni 31,056 ambapo kwa walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795, Stashahada (Diploma) 6,596 na wenye Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo zimechelewa kutokana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi ya shule ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmahauri na shule.
“Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa halmashauri na shule hasa za mjini zenye walimu wa ziada na zingine hasa za vijijini zina upungufu mkubwa wa walimu,” alisema Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia kuwapanga walimu wapya kwa usawa ili kuondoa uwiano usioridhisha kwenye maeneo mengi ya vijijini. Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu za kupata kibali kwa ajili ya ajira za walimu na fedha za kuwalipa stahili zao ili waanze ajira zao rasmi mwezi ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo watakavyopangiwa vitawekwa katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ambayo ni www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu www.moe. go.tz ifikapo Aprili 24, mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba alisema, pia ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na taarifa sahihi za walimu wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi kuajiriwa ili kuepuka usumbufu kwa walimu ambao hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao wameshaajiriwa wanapoenda kusoma, hupangiwa upya vituo na hawatoi taarifa hivyo kuleta usumbufu wa kuchelewa kutopata mishahara yao.
“Kuna baadhi ya walimu wameshaajiriwa kwa hiyo jina linapoingizwa katika taratibu za malipo, linagoma kuingia ndipo ukifuatilia unajua alikuwa ameajiriwa, inabidi umwambie arudi kwa mwajiri wake.
Kwa hiyo kwa hawa walimu wapya nawashauri waende kuripoti katika vituo walivyopangiwa na wakubali kufanya kazi katika maeneo hayo, sio waripoti halafu waondoke,” alisema.
Wakati huohuo, Serikali imewataka Makatibu Tawala wa Mikoa ambayo shule zake zimefungwa kwa madai ya ukosefu wa chakula, kuwachukulia hatua wakuu wa shule hizo, kwa kile kilichoelezwa kuwa wamekiuka utaratibu kutangaza hivyo ilhali serikali ilishatuma fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.
Shule zilizofungwa kwa tatizo hilo na mikoa yake kwenye mabano ni Rugambwa, Kahororo, Nyakato na Ihungo (Kagera), Lyamungo (Kilimanjaro), Mpwapwa na Abeid Karume (Dodoma), Kazima, Milambo, Wavulana Tabora na Wasichana Tabora (Tabora).
Uamuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini aliyesema serikali imeshatoa asilimia 66.7 ambazo ni Sh bilioni 28.1 zilizotengwa kwa mwaka 2014/2015.
Alisema serikali imetoa fedha hizo katika kipindi cha mwezi Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule za sekondari, zinazomilikiwa na serikali. Sagini alisema serikali ilitenga Sh bilioni 42.1 kwa mwaka 2014/2015, ambapo kati ya fedha hizo kiasi kilichobaki ni Sh bilioni 13.9, sawa na asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa.
“Kwa ufupi, serikali haijafunga shule na wakuu wa shule waliotangaza kufunga shule hizo chache wamefanya makosa kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka husika ili kupata kibali kama kungekuwa na sababu ya kufanya hivyo, naamini mamlaka husika zitawachukulia hatua,” alisema Sagini.
Alisema wamiliki wa shule ni Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambazo watendaji wake ni wakurugenzi na wakuu wa shule ni viongozi wasimamizi wa shule hizo, hivyo hawana mamlaka ya kutangaza kufunga shule kwa sababu yoyote bila kibali cha mwenye shule.
Kwa mujibu wa Sagini, kuna utaratibu wa kufunga shule ambapo katika kipindi hiki, shule nyingi zilikuwa zimefungwa kwa mapumziko mafupi kati ya Machi 28 hadi Aprili 12, ambapo katika shule hizo zilizofungwa wanafunzi walilazimika kurudi makwao kutokana na kutangaziwa na wakuu wao wa shule.CHANZO: HABARI LEO (Muro)

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA