UCHAMBUZI WA MALISA; KUSHUPAA NI TABIA IMFAAYO MPUMBAVU; NA SERIKALI INAYOSHUPAA NI SERIKALI YA KIPUMBAVU


Na Malisa GJ,

Mpumbavu ni mtu anayeshupaza shingo yake anapoelekezwa jambo lenye manufaa. Akielekezwa haelewi na hata akielewa hataki kufuata. Kwa mujibu wa Profesa Kabudi wa chuo kikuu cha Dar (UDSM) "Mpumbavu ana tabia ya kushupaa, while mjinga ana tabia ya kuduwaa."

Yani ukimwambia mjinga usifanye jambo fulani atakuuliza kwanini? Ukimpa sababu za kuridhisha atabaki kuduwaa maana alikua hajui, na akishajua atafanyia kazi uliyomueleza.

Lakini ukimwambia mpumbavu usifanye jambo fulani badala ya kukuuliza kwanini ATASHUPAA kulifanya. Na hata ukimueleza sababu za kutokufanya atazidi kushupaa hadi afanye. Hiyo ndio tabia ya mpumbavu.

Kwa wale wakristo mpumbavu ametajwa mara nyingi sana ktk Biblia. Adhabu ya mpumbavu imetajwa kuwa ni kuvunjika shingo ghafa. Ktk kitabu cha Mithali 29:1, Biblia inasema "aonywaye mara nyingi na kushupaza shingo yake atavunjika ghafla na hatapata tiba".. Kuvunjika shingo kwa mpumbavu ndiyo malipo yanayomstahili maana huwa hasikii.

Nimeeleza hivi kwa sababu serikali ya CCM imekuwa na tabia ya KUSHUPAA kwa muda mrefu. Hata inaposhauriwa for its own good bado inashupaa na kusimamia misimamo yake isiyo na mantiki. Serikali ya CCM imeshupaa kwenye mambo mengi yasiyo na tija lakini leo nitazungumzia matatu ya msingi.

HOJA YA KWANZA;
Serikali iliagiza wafanyabiashara wanunue mashine za EFD nchi nzima. Mashine zinauzwa kuanzia laki 8, lakini ajabu ni kuwa hata wenye mitaji ya laki tano wanalazimishwa kununua mashine hizo. Yani mtu afilisi duka lake lote ili anunue mashine ya EFD? So what? Akishanunua hiyo EFD na mtaji wake wote umeisha, atakula hiyo mashine au?

Wenye akili walishauri serikali iuze mashine hizo kwa wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa tu, maana wadogo hawawezi kumudu. Au mashine zitolewe bure then kodi wanayotozwa wafanyabiashara hao ifidie kwenye mashine. Lakini serikali IKASHUPAA. Kushupaa ni tabia imfaayo MPUMBAVU.

Ikalazimisha kila mfanyabiashara anunue mashine hizo. Matokeo yake wamegoma na jamii ikathirika kwa kukosa mahitaji. Takribani wiki nzima sasa, maduka yote mkoani Iringa na Njombe yamefungwa kama sehemu ya muendelezo wa mgomo huo.

Serikali imeshauriwa itafute suluhu na wafanya biashara, lakini serikali kupitia TRA imeendelea KUSHUPAA. Kushupaa ni tabia imfaayo MPUMBAVU.

HOJA YA PILI;
Serikali ilishauriwa kuhusu kura ya maoni. Ikaambiwa kuwa HAIWEZEKANI kura ya maoni kufanyika April 30 mwaka huu. Lakini "mkuu wa kaya" AKASHUPAA na na kutangaza kwa "mbwembwe" kuwa kura ya maoni itakuwa April 30 mwaka huu.

Wakati huo mashine za BVR za kuandikisha wapiga kura hazikuwa zimefika nchini. Baadae zikafika chache zinazotumika kuandikisha mkoa wa Njombe kwa sasa. Wenye akili wakashauri serikali iahirishe zoezi hili lakini "Mtoto wa mkulima" wakati akiahirisha bunge majuzi AKASHUPAA. Akasema zoezii la kura ya maoni liko palepale.

Kesho yake Mwenyekiti wa NEC Jaji Lubuva akatangaza kuahirishwa kwa kura ya maoni. Nikajiuliza hivi "Mtoto wa mkulima" alikua ANASHUPAA nini? Nikagundua kushupaa ni yabia ya mpumbavu.!

Baada ya siku mbili katibu mwenezi wa ccm akajitokeza hadharani na kumshambulia Jaji Lubuva eti ajiuzulu kwa kushindwa kufanikisha kura ya maoni April 30. Kwa lugha rahisi Nape alikua ANASHUPAA ili kura ya maoni ifanyike April 30. Kushupaa ni tabia imfaayo mpumbavu. Nikajiuliza kumbe kaNape nako ni kapumbuavu?

Jaji Lubuva alisema wana mashine za BVR 300, na wanategemea kupata BVR nyingine 7700 kufikia katikati ya mwezi huu. Hivyo tu-assume kufikia tar.15 April tutakuwa na mashine za BVR 8000 kwa nchi nzima.

Sasa twende kwenye hesabu rahisi za darasa la tano (Simple Arithmetic). Mashine moja ya BVR ina uwezo wa kuandikisha watu 60 kwa siku. Inadaiwa ofisi ya Waziri Mkuu imelazimisha ziweze kufikisha watu 100 kwa siku. Anyway twende na data za Pinda za watu 100 kwa siku.

Mashine 8000 "tukizi-overdose" zikaandikisha watu 100 kila moja kwa kwa siku ni jumla ya watu laki nane (800,000). Kwa kuwa mashine zote zinategemea kufika ifikapo April 15 (though we are not sure), zitakuwa zimebaki siku 15 tu kufikia April 30.

Mashine zote zitakuwa na uwezo wa kuandikisha watu laki nane kwa siku, that means mashine zote zitaandikisha watu milioni 12 tu kufikia April 30.

Lakini wapiga kura wa nchi hii wanakadiriwa kuwa watu milioni 28. So hata mashine zote za BVR zingefika na kuanza kuandikisha watu siku hiyohiyo (hapo tumeondoa muda utakaotumika kuzisambaza) bado haziwezi kuandikisha watu wote mil.28.

Zitaishia kuandikisha watu mil.12 tu sawa na asilimia 42 ya wapiga kura wote (42%). Kwa lugha rahisi hazitaweza kuandikisha hata nusu ya wapiga kura. Sasa Pinda na Nape walikua WANASHUPAA nini kuwa lazima kura ya maoni ifanyike kufikia April 30? Kushupaa ni tabia imfaayo mpumbavu.

HOJA YA TATU;
Nimesikia mgomo wa madereva unaotarajiwa kuanza kesho kwa nchi nzima. Mgomo huo unatarajiwa kuhusisha magari yote ya abiria na mizigo hadi bodaboda. Hoja za madereva hao ni kuhusu leseni zao za udereva.

Utaratibu wa sasa wa kurenew leseni unamtaka dereva arudi upya darasani akasome na afanye majaribio ndio apewe leseni mpya. Kwenda kusoma it means dereva aache kazi, aingie darasani mwezi mzima asome upya then akimaliza afanyiwe testing na Vehicle Inspector ndio apewe leseni.

Madereva wana familia zinazowategemea. Wana watoto, wazazi, wake, ndugu etc.. hivi wakienda kusoma mwezi mzima bila kufanya kazi nani atahudumia familia zao? Na je wakirudi kutoka kusoma waajiri watawarudisha kazini au watakuta wameshaajiri madereva wengine?

Wenye akili wameishauri serikali itafute utaratibu mwingine mzuri zaidi utakaotumika kupima competency ya madereva badala ya kuwarudisha shule mwezi mzima, lakini serikali ya CCM IMESHUPAA. Kushupaa ni tabia imfaayo MPUMBAVU.

Pia madereva wamehoji uhalali wa malipo ya Shilingi Laki 6 wanayotakiwa kulipa ili kupata mafunzo ya udereva ya mwezi mmoja yatakayowawezesha kupata leseni mpya. Kwanini laki 6? Na kwanini vyuo wanavyotakiwa kusoma wanaelekezwa na serikali? Hivi hii si mbinu ya serikali kuchuma fedha kwa madereva kwa kigezo cha leseni?

Hivi unamwambiaje dereva mwenye uzoefu wa miaka 30 aache kazi na kwenda driving school mwezi mmoja eti kusomea udereva huohuo alioufanyia kazi miaka 30? Serikali ya CCM imeshauriwa kutafuta mbinu mbadala lakini IMESHUPAA. Kushupaa ni tabia imfaayo Mpumbavu.!

Nimesikia jeshi la Polisi likiSHUPAA eti kesho hakuna mgomo wa madereva na yeyote atakayegoma atakiona. Hii ni approach ya kijinga sana ya kukabiliana na tatizo. Vitisho si njia sahihi ya kutafuta suluhu.

Cha ajabu wakati Polisi wakitishia kuwa kesho hamna mgomo tayari kuna maeneo nchi hii wameshajiandaa kugoma. Huku Njombe malori kesho yatazuia njia zote asubuhi na mapena ili gari zisiweze kutoka wala kuingia (isipokuwa gari binafsi tu). Na mikoa mingine hali ni hiyohiyo.

Wenye akili wameshauri serikali itafute suluhu na madereva kwa kukaa nao na kuwasikiliza badala ya kuwatisha kwa kutumia Polisi. Lakini serikali ya CCM imekataa ushauri huo na imeendelea KUSHUPAA na kushikilia msimamo wake.

Kushupaa ni tabia imfaayo mpumbavu; na serikali inayoshupaa ni serikali ya kipumbavu. Maandiko yanasema adhabu ya mpumbavu (mwenye tabia ya kushupaa) ni kuvunjika shingo na hakuna Dawa. Naiona serikali ya CCM ikivunjika shingo na haitapata dawa. Dawa yake ni kaburi. Naliona kaburi la CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.

JIPU LIMEPASUKA, SIWEZI KUWA ADUI KWA KUSEMA UKWELI.

Malisa GJ || Your Partner In Critical Thinking.!

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA