Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bandari atimuliwa

SAMUEL Sitta-Waziri wa Uchukuzi, amemng’oa rasmi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (PTA), Madeni Kipande, ambapo sasa anarejeshwa idara kuu ya utumishi ili kupangiwa majukumu mengine.

Kipande ambaye alisimamishwa kazi 16 Februari, 2015, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yake, sasa nafasi yake itaendelea kukaimiwa na Awadhi Massawe.

Wakati akimsimamisha Kipande, Sitta alisema ni kutokana na kukiuka taratibu za manunuzi na zabuni na kuwa na mahusiano mabovu na wadau wa mamlaka hiyo na hivyo kuunda tume ya uchunguzi ambapo taarifa yake imetolewa leo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Sitta amesema tume ilikamilisha kazi yake 20 Machi, 2015 na kumkabidhi taarifa ya uchunguzi wao 24 Machi 2015 kwa hatua zaidi.

“Baada ya kuisoma taarifa ya tume na hatimaye kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo mashaka yoyote kwamba isingefaa Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza PTA. 
“Hii ni kutokana na kudhihirika utawala mbovu aliouendesha uliosababisha manung’uniko mengi miongoni mwa wateja na wadau wa bandari na mgawanyiko mkubwa na wafanyakazi,”amesema Sitta.

Aidha, Sitta alitumia muda huo kutoa ufafanuzi wa uchunguzi kuhusu ununuzi wa mabehewa mabovu katika kampuni ya Reli Tanzania (TRL), akisema ameagiza Bodi ya Wakurugenzi wa TRL kuipitia taarifa hiyo ya tume na kutoa maelezo.

“Kwa ujumla imebainika kwamba; mabehewa mengi kati ya yaliyoagizwa yana kasoro, kulikuwa na uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kiwandani yalipokuwa yanatengenezwa na kulikuwa na uzembe katika kuendelea kuyapokea pamoja na ubovu wake kujulikana,”amesema.

Sitta ameongeza “siku ya Jumatatu tarehe 13 Aprili, 2015, wizara imeshtushwa kugundua kinyume na taarifa za awali na kinyume na masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo mabovu yamefanyika kikamilifu.”

Amesema kuwa watengenezaji wamelipwa asilimia 100 ya fedha kinyume na masharti ya mkataba na kwamba wizara inaona kuwa utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi wala sio uzembe.

Kufuatia hali hiyo, Sitta ameagiza uchunguzi wa kubaini uwezekano wa hujuma ufanyike na kwamba madhumuni hayo amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara yake asimamie kuundwa kwa kamati ya uchunguzi.

Amesema kuwa kamati hiyo itaongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akishirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Sitta ameipa kamati hiyo wiki tatu kuanzia 20 Aprili, 2015, kukamilisha uchunguzi huo, na katika kipindi hicho viongozi wakuu wa TRL wanawajibika na mkondo wa kashfa hiyo wote wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi.

Sitta amewataja viongozi hao kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu, mhandisi mkuu wa mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, mhasibu mkuu, Mbaraka Mchopa, mkaguzi mkuu wa ndani, Jasper Kisiraga na meneja mkuu wa manunuzi, Ferdinand Soka.

  • Taarifa ya Sarafina Lidwino via MwanaHALIASI Online

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA