SERIKALI YAAGIZA SHULE ZIFUNGULIWE MARA MOJA ZILIZOFUNGWA KWA KUKOSA CHAKULA



Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Jumanne Sagini ameagiza kufunguliwa mara moja kwa shule za Sekondari zilizofungwa kutokana na ukosefu wa chakula na wanafunzi kurejea makwao.


Sagini amesema kuwa Serikali imeshapeleka asilimia 67% ya fedha katika Halmashauri zote nchini, kwa ajili ya chakula hivyo hakuna uhalali wa Wazabuni kushindwa kutoa huduma kwa sababu ya madeni.

Wiki iliyopita, wanafunzi katika shule 10 za Sekondari katika mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Dodoma na Tabora walilazimika kusitisha masomo na kurejea majumbani kutokana na ukosefu wa chakula.

Leo, gazeti la NIPASHE limeripoti taarifa ifuatayo:

Hali ni tete katika shule za kutwa za sekondari nchini, kutokana na kile kinachoelezwa ni kukosekana kwa chakula baada ya wazabuni kugoma kupeleka vyakula kutokana na kutolipwa fedha wanaozidai shule.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mikoa kadhaa nchini, kuwa baadhi ya shule zimelazimika kufungwa kutokana na kukosa chakula na kuwaacha wanafunzi wenye mitihani ya Taifa wa kidato cha pili, nne na sita.

Mkoani Kagera, shule saba za sekondari zimefungwa kutokana na ukosefu wa chakula na wanafunzi wa kidato cha kwanza, tatu na tano wakirudishwa nyumbani kwa muda usiojulikana.

Hali hiyo inatokana na wazabuni wanaotoa huduma ya chakula kwa shule hizo kutolipwa fedha wanazodai.

Ofisa Elimu wa mkoa wa Kagera, Florian Kimolo, alisema wanafunzi katika shule hizo wameongezewa muda wa kukaa nyumbani wakati huu ambao serikali inatafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

Alizitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni Rugambwa, Kahororo, Ihungo, Nyakato, Kimolo, Rukore, Kabanga na Muyenze za

Wilayani Ngara na kuwa tayari wamepeleka taarifa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa ajili ya kupatiwa fedha za chakula ili wanafunzi warudi kuendelea na masomo.

“Kawaida binadamu yeyote anahitaji chakula na kinapokosekana siyo rahisi kuendelea kuishi na kuwa kumbakiza mwanafunzi shuleni bila kumpa chakula kuna athari kubwa kiafya,” alibainisha na kuongeza: “Kuwarudisha nyumbani kuna athari maana kunapunguza siku zao za masomo na wanaweza wasifundishwe baadhi ya mada.” “Sifahamu lini wanafunzi hao watarejeshwa shuleni, lakini sisi kama serikali tunafahamu madhara ya tatizo hilo, ndiyo maana tunafanya kila jitihada ili warejee mapema iwezekanavyo” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chacha Mwita, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo katika shule za sekondari za bweni na kuwa jitihada zinaendelea ili wanafunzi warejee shuleni mapema iwezekanavyo.

Chacha alisema kuna madeni na kudai kuwa wazabuni hawajagoma kutoa huduma na kuwa kuna kikao kimefanyika na mawasiliano yanaendelea kufanyika ili waendelee kutoa chakula shuleni.

Hata hivyo, hakubainisha kiasi cha chakula kinachohitajika kwa shule zote na kuahidi kutoa taarifa kamili siku zijazo.

Mkoani Dodoma, shule za sekondari za bweni zimefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na ukosefu wa chakula kwa wanafunzi.

Taarifa zilizolifikia NIPASHE zinaeleza kuwa moja ya shule hizo ni Shule ya Sekondari Mpwapwa ambayo ilitakiwa kufunguliwa baada ya likizo fupi ya sikukuu ya Pasaka lakini mpaka sasa haijulikani itafunguliwa lini.

Mkuu wa shule hiyo, Nelson Mbilinyi, alisema wanafunzi walitakiwa kufungua shule siku tatu zilizopita, lakini hadi sasa wameshindwa kufungua shule kutokana na ukosefu wa chakula.

“Tulikuwa tufungue Aprili 8, mwaka huu, lakini hatujafungua hadi sasa chakula cha kuwalisha wanafunzi hakuna,” alisema.

Alisema bado hawajajua shule hiyo itafunguliwa lini, lakini kitu ambacho anakijua ni kwamba leo kuna kikao na Afisa Elimu wa Mkoa.

Katika shule ya sekondari ya Wasichana Msalato iliyopo, Mkuu wa Shule hiyo, Mwasi Chibuni, alisema shule hiyo haijafungwa isipokuwa hali ya chakula si nzuri.

“Licha ya wanafunzi kuendelea na masomo, lakini hali ya chakula siyo nzuri na shule haijafungwa tunaendelea tuone tutaishia wapi,” alisema.

Alibainisha kuwa wataendelea kujisogeza hivyo hivyo na kama watashindwa, watalazimika kufunga shule.

Katika wilaya ya Kondoa, kuna taarifa kuwa hali ya chakula katika shule ya wasichana ya Kondoa ni mbaya na inaweza kufungwa.

Hata hivyo, Afisa Elimu sekondari wa wilaya hiyo, Lucy Gurtu, alikanusha kuwa hakuna shule iliyofungwa kutokana na uhaba wa chakula.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, alipoulizwa kuhusu tatizo hilo, alijibu kuwa hana taarifa kwa sasa analifuatilia.

Mkoani Kilimanjaro, Serikali imesema itamchukulia hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi, Mkuu yeyote wa shule ya sekondari atakayebainika kushindwa kufungua shule kuanzia leo kwa kisingizio kwamba shule yake haina chakula.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Alfred Shayo, aliiambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kwamba, tayari wamepokea fedha kutoka Hazina, kwa ajili ya kuzihudumia shule za serikali.

“Kama kuna mkuu wa shule ambaye hatafungua shule katika muda uliopangwa, atachukuliwa hatua za kisheria kwa sababu Hazina

iliyopo chini ya Wizara ya Fedha, imekwishaleta hizo fedha za chakula, ila kama zimechelewa kuwafikia wakuu wa shule, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa haina taarifa hizo...Kwa maana hiyo shule zote zitafunguliwa leo kama kawaida.

Alisema ofisi hiyo haina taarifa yeyote ya shule za serikali mkoani hapa kubadili ratiba ya masomo baada ya kumalizika kwa mapumziko ya Pasaka kutokana na uhaba wa chakula.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema anachofahamu ni wazabuni wengi kutolipwa fedha zao na kwamba hana takwimu za kiasi wanachodai na shule zenye uhaba.

Shule nyingine zilizofungwani shule ya wavulana na wasichana Tabora za mkoani Tabora, shule ya wavulana Nsumba mkoani Mwanza, shule ya wasichana Masasi, Ndanda za mkoani Mtwara na shule ya sekondari ya wavulana ya Songea, mkoani Ruvuma.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Ndanda ambaye hakutaja kutajwa jina lake, alisema wametakiwa kurudi nyumbani mwishoni mwa wiki kwa kuwa hakuna chakula.

Shule ya wasichana ya Tabora, mmoja wa wanafunzi alithibitisha kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi wasio na mitihani ya Taifa mwaka huu, tangu Machi 24, mwaka huu, kutokana na uhaba wa chakula.

MKURUGENZI TAMISEMI

Mkurugenzi wa Sekondari wa TAMISEMI, Paulina Nkwama, alipoulizwa na NIPASHE juu ya suala hilo, alisema amepata taarifahizo, lakini anachofahamu shule zinapelekewa fedha za kulipa madeni ya wazabuni.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi, alisema yeye si msemaji wa Wizara na kumtaka mwandishi kumtafuta Waziri husika.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia (pichani) na Naibu wake, Kassimu Majaliwa, walipotafutwa na NIPASHE simu zao ziliita bila kupokelewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anna Kilango, alisema suala hilo lipo chini ya Tamisemi na kwamba waulizwe mawaziri husika.

Jitihada za kuwapata Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, na Naibu Mwigulu Nchemba, simu zao ziliita bila kupokelewa na hata walivyotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

Imeandikwa na Lilian Lugakingira (Bukoba), Augusta Njoji, (Dodoma), Godfrey Mushi (Moshi) na Salome Kitomari (Dar).

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA