Karafuu hotel yateketea kwa moto

Hoteli ya kitalii ya Karafuu iliopo Michamvi mkoa wa kusini Unguja imeteketea kwa moto katika baadhi ya sehemu zake na kusababisha hasara kubwa.

Meneja wa hoteli hiyo Juma Abdalla alisema chanzo cha moto huo hadi sasa hakijafahamika pamoja na hasara kamili inayotokana na moto huo.

Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yameathirika na moto huo ni pamoja na sehemu ya mabanda ya kupikia na katika vyumba vya wageni ambao walitolewa nje bila ya madhara.

'Chanzo cha moto huu hadi sasa hakijafahamika tunafanya uchunguzi zaidi kujuwa pamoja na hasara kamili'alisema.

Afisa mkuu wa Zima moto katika kituo cha Kitogani Hamad Ali Abdalla alisema wamefanikiwa kuzima moto huo ambao ulikuwa na kasi kubwa ambao ulikuwa ukisaidiwa na
upepo.

Alisema walilazimika kuomba msaada wa kuzima moto huo kutoka makao makuu mjini ambapo kazi hiyo ilifanikiwa.

Hata hivyo aliziomba hoteli za kitalii uongozi wake kuhakikisha kwamba wanaweka vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto.

Alisema moto huo ungelizimwa haraka sana na wafanyakazi wenyewe wa hoteli hiyo lakini kwa bahati mbaya hakuna vifaa vya kuzima moto huo.

'Tunawaomba viongozi wa hoteli kubwa za kitalii kuhakikisha kwamba wanaweka vifaa vya kukabiliana na majanga kama moto kwa ajili ya kuzima haraka'alisema.

Hilo ni tukio la pili la hoteli za kitalii kuathirika na majanga ya moto ambapo miezi miwili iliyopita huko Nungwi mkoa wa kaskazini Unguja hoteli mbili ziliteketea
kwa moto.

Hoteli nyingi ziliopo katika mwambao wa pwaniwa Zanzibar zimeezekwa kwa kutumia makuti ambayo huwa rahisi kushika moto wakati yanapotokezea majanga kama hayo.

  • via Lukwangule blog

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA