MZEE HASSAN MOYO AFUKUZWA CCM

Hassan Nassoro Moyo
Hassan Nassoro Moyo

MWANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenye kadi namba saba Mzee Hassan Nassoro Moyo amefukuzwa katika chama hicho.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 81 ambaye amekuwa na msimamo tofauti na chama chake kuhusu Zanzibar ametimuliwa na mkoa wa kichama wa Magharibi Unguja.

Wamesema sababu ya kumtimua uanachama wa CCM, chama ambacho alishiriki kukiasisi, ni matendo yake kwenda kinyume na maadili na sera za chama hicho.

Kauli ya kutimuliwa imetolewa na katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Unguja Aziza Iddi Mapuri. Katibu huyo amesema matamshi mbalimbali aliyokuwa akiyatoa Mzee Moyo katika mikutano ya hadhara inayofanywa na chama cha wananchi, CUF inaonesha kwamba amekisaliti chama chake.

Taarifa hiyo imetoa mfano, tarehe 30-4-2014 katika mkutano wa CUF uliofanyika Kibanda Maiti, Katibu wa CUF, Seif Sharif Hamad alimsimamisha Mzee Moyo ambaye alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari wote.

Aidha, katika mkutano uliofanyika Tibirinzi huko Pemba tarehe 9-2-2014 Mzee Moyo alijitambulisha kwamba ni mwenyekiti wa maridhiano kutoka CCM wakati siyo kweli kwani Chama Cha Mapinduzi hakimtambui kiongozi huyo.

Taarifa hiyo imesema CCM baada ya kutafakari kwa kina imebaini kwamba kiongozi huyo amekuwa akiongoza upotoshaji wa hali ya juu na hafai kuendelea kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Iemtoa mfano kuwa, wakati akihutubia kongamano la CUF katika ukumbi wa taasisi ya Kiswahili na lugha za Kigeni, Moyo alibeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kusema Mkataba wa Muungano wa tarehe 22-4-1964 haujulikani uliopo na wabunge wa Bunge Maalum la Katiba walikuwa hawajui wanachokifanya.

Hatua ya kumfukuza Mzee Moyo inaashiria kuwa Kamati ya Maridhiano iliyokuwa na wajumbe sita, 3 kutoka CCM na 3 kutoka Chama cha Wananchi, CUF, ni shubiri kwa CCM ambayo baadhi ya viongozi wake wakuu wanataka serikali ya umoja wa kitaifa ivunjwe.

Wawakilishi wa CCM katika Kamati ya Maridhiano waliokuwa pamoja na Mzee Moyo, tayari walishafukuzwa uanachama, hivyo tukio la hili linahitimisha kuwamaliza wanachama hao walioleta maridhiano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Waliokuwa na Mzee Moyo kwenye Kamati ya Maridhiano ni Mansour Yusuf Himid ambaye alifukuzwa Agosti 2013 na Mohammed (Eddy) Riyami aliyejiondoa.

Wote sasa wanafanya kazi na CUF kusaidia kampeni ya kupatikana Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Mansour ambaye ameteuliwa kuwa katibu wa kamati ya mkakati ya kuhakikisha ushindi wa Maalim Seif Sharrif Hamad, ameshatangaza kugombea uwakilishi jimbo la Kiembesamki.

Mzee Moyo aliliambia gazeti la MwanaHALISI Online kuwa taarifa hizo amezisikia juu juu tu, kwani hajapewa taarifa rasmi ya kufukuzwa uanachama wake.

“Mimi sipo Zanzibar, taarifa hizo nimezisikia juu juu tu, lakini muda muafaka ukifika nitatoa tamko rasmi,” anasema Mzee Moyo anayemiliki kadi namba saba.

Mzee Moyo anasema, hashangai kusikia kuwa amefukuzwa kwani mara kadhaa viongozi wa CCM wa mkoa wa Wilaya, walikuwa wanamtaka awarushie kadi yake ya uanachama, lakini aligoma na kuwaambia labda akiitaka Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Vuguvugu la kumvua uanachama Mzee Moyo ulianza tangu kamati yake ya Maridhiano ilipofanikisha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada uchaguzi 2010 amekuwa akipigania kuwepo Muungano wa serikali anaosema ndio wa haki na utaipa Zanzibar serikali yenye mamlaka kamili kinyume na ilivyo uhai wote wa Muungano miaka zaidi ya hamsini.

Msimamo huu unapingana na sera ya CCM inayoshikilia Muungano wa Serikali mbili. Msimamo wake unachukuliwa kama ni msimamo unaoendana na CUF hivyo kuwekwa kundi la kusaliti CCM.

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA