BURUNDI: UFUNGUZI WA MAZUNGUMZO KATIKA HALI YA MVUTANO
Na RFI
Mkutano kati ya serikali ya Bujumbura, upinzani na vyama vya kiraia umeanza umechelewa, lakini mazungumzo hayo yamefunguliwa rasmi nchini Uganda, chini ya upatanishi wa rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Mazungumzo hayo yalikua yamesimama kwa muda wa miezi mitano. Mazungumzo ambayo ni moja ya njia ya kumaliza mgogoro unayoikumba Burundi tangu rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais.
Sherehe zimefanyika katika ukumbi wa Ikulu ya rais katika mji wa Entebbe, nchini Uganda, pamoja na wawakilishi wa serikali, upinzani na vyama vya kiraia. Pande zote zimeketi kwenye meza moja chini ya shinikizo la kimataifa.
Watu zaidi ya mia moja, vyama kumi na tano, vimekuwepo Jumatatu hii asubuhi katika kikao cha ufunguzi wa mazungumzo hayo ili kila upande sauti yake isikike. Uwepo wao katika mji wa Entebbe umeonyesha matumaini, licha ya kutokea kwa mvutano na miguno kati ya wadau katika mgogoro huo.
Rais wa Uganda ameanza kuwasilikiza washirika mbalimbali wa kimataifa: Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa. Mashirika mbalimbali yameunga mkono upatanishi kwa kukomesha haraka mgogoro unaoikabili Burundi, lakini pia wameweka mbele wasiwasi wao.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametoa wito kwa pande zote kutoweka masharti ili kuwezesha mazungumzo kusonga mbele.
Hata hivyo kila upande umeonekana ukitoa maneno makali dhidi ya mwengine. Muungano wa wanasiasa wanaotetea Mkataba wa mani wa Arusha na marejesho ya utawala wa sheria nchini Burundi (CNARED) umelaani maneno yanayotolewa na serikali kwamba muungano huo unaundwa na watua waliohusika katika jaribio la mapinduzi la Mei 13. Muungano huo umeinyooshea kidole cha lawama serikali kwamba inahusika na mauaji ya kikatili kwa watu waliokua mikononi mwa ngazi za serikali.
Mazungumzo yataendelea Arusha Januari 6
Mkutano ujao umepangwa Januari 6 mjini Arusha, nchini Tanzania. Tangazo hilo limeikera serikali ya Burundi, ambayo imeshtumu kutoshirikishwa kwa kuandaa na kupanga tarehe hiyo na sehemu mazungumzo yajao yatakapofanyika. Serikali pia imesikitishwa na kualikwa kwa muungano wa wanasiasa walio ukimbizini (CNARED) katika mazungumzo hayo, ambapo serikali imesema muungano huo hautambiliwi na sheria za Burundi.
Upinzani umekaribisha tangazo hilo la mkutano ujao na kusema kuwa una imani kuwa ratiba itawekwa sawa na wazi pamoja na mwelekeo kwa ajili ya mazungumzo. Jumatatu hii asubuhi, chama tawala, cha CNDD-FDD, kimefutilia mbali mazungumzo ya aina yoyote na muungano huo wa wanasiasa walio ukimbizini (CNARED)
Comments
Post a Comment