Maagizo ya Mawaziri tangu kuapishwa Desemba 12




Ni mwendo wa maagizo. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kila waziri anayefanya ziara katika idara au taasisi zilizoko chini yake kutoa maagizo kudhihirisha uwepo wao.

Mawaziri hao ambao waliapishwa Desemba 12, mwaka huu, wameanza kazi kwa kasi kama ilivyokuwa kwa Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambao walianza kazi kwa kuwasimamisha maofisa wa umma na wajumbe wa bodi zaidi ya 83 katika muda mfupi, kutokana na makosa mbalimbali.

Baada ya kuapishwa, siku hiyo hiyo baadhi ya mawaziri na manaibu wao walianza kazi kwa kutembelea idara zilizo chini ya wizara zao na wengine wakienda kuripoti wizarani, ikiwa ni kutimiza kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu!

Muhongo atoa siku 30


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi mkoani Iringa, alikutana na mameneja wa kanda wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kuwataka kuhakikisha ifikapo Januari 15, mwakani kazi ya kuwaunganishia umeme waombaji wa siku nyingi iwe imekamilika.

Profesa Muhongo ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini alisema meneja yeyote atakayeshindwa kutimiza agizo hilo aache kazi mwenyewe au ajiandae kufukuzwa.

“Ikitokea wananchi wakalalamika kucheleweshewa huduma kufikia tarehe 15 mwezi ujao, muwe tayari kuacha kazi wenyewe,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Pia alisema kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wananchi, juu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kucheleweshewa huduma ya kuunganishiwa umeme na mita za Luku.

“Mameneja wote ifikapo Jumamosi ya tarehe 19 mwezi huu, muwe na majibu ya kero mbalimbali zinazohusu umeme,” alisema.


Jafo atoa siku 26


Akizungumza na wafanyakazi na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Bahi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo, alitoa siku 26 kwa halmshauri zote nchini kukamilisha na kuanza kuutumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato.

Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, alisema atawawajibisha wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato ifikapo Januari 10 mwakani.

“Mkurugenzi atakayeshindwa kutimiza agizo hili aandike barua kwa Katibu Mkuu TAMISEMI kujieleza kwamba ameshindwa, kila mkurugenzi atawajibika katika hili kwa kushiriki ufisadi wa kuikosesha halmashauri mapato,” alisema.

“Mfumo huu ulitakiwa kuwepo kuanza kutumika tangu Julai mwaka huu, lakini hadi sasa zipo halmashauri hazijaanza kuutekeleza katika idara zake hali inayosababisha upotevu wa mapato.

“Wilaya ya Bahi ilitakiwa kuwa ya mfano kwa kuweka mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato lakini kutokana na uzembe na inawezekana umecheleweshwa kwa makusudi ili kuendelea kutoa mianya ya watu kujipatia fedha,” alisema.

Mhagama atoa siku 26


Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alitoa siku tano kwa Manispaa ya Ilala kuvunja mkataba na mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa mtaro uliopo Buguruni kwa Mnyamani, kutokana na kujenga chini ya kiwango.

Akitoa agizo hilo, Mhagama alisema ofisi yake haitatoa fedha za kumlipa mkandarasi huyo na kama manispaa imemlipa fedha zozote, wazirudishe na ikibidi waliozilipa wazitoe mifukoni mwao.

Kutokana na mafuriko katika eneo hilo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, wakati wa uongozi wake alifika eneo hilo na kutaka baadhi ya nyumba zivunjwe na ujenzi uanze.

“Kama hamjamlipa mkandarasi serikali haitahusika na deni hilo na kama mmemlipa fedha hizo mkurugenzi na timu yako zitoke mifukoni mwenu, haiwezekani mkandarasi ajenge chini ya kiwango halafu mnamwangalia tu,” alisema Jenista.

Waziri huyo pia alitoa tangazo kwa vyombo vya habari, akiwapa siku saba waajiri wote nchini kuhakikisha wametoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na kuruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho, aliwataka waajiri hao ndani ya muda huo wawe wameandikisha wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na kupeleka michango yao kwa wakati.

Pia alitoa siku 14 waajiri ambao wana watumishi wasio raia wa Tanzania, wawe wamewachukulia vibali vya kufanya kazi kutoka kwa Kamishina wa Kazi kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya mwaka 2015.

Mbarawa na DAWASCO


Naye Waziri wa Maji, Makame Mbarawa alilitaka Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es salaam (Dawasco), kuhakikisha kuwa hadi kufikia Juni mwakani wateja milioni moja wawe wamepatiwa huduma ya maji.

Mbarawa alimtaka Mkurugenzi wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, kuongeza kadirio la wateja walilokuwa wamejiwekea la wateja 148,000 hadi kufikia milioni moja.

“Naamini pindi tutakapofanya mazungumzo ya kina tutafikisha kiasi hicho cha wateja hiyo Juni na hilo mtalipima kwenye tathimini tutakapokutana Februari,” alisema Mbarawa.

Lukuvi atoa siku saba


Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alitoa siku saba kwa wakuu wa idara za ofisi yake kuhakikisha wanaenda Kituo cha Uwekezaji (TIC), kukagua maeneo waliyopewa wakezaji kama yanaendelezwa kwa makusudi yaliyotarajiwa.

Lukuvi alisema, wapo wawekezaji ambao waliomba na kupewa maeneo ambayo wameyageuza matumizi bila taarifa, hivyo ni vyema wakafuatiliwa ili kuwabaini.

“ Tunafahamu wapo walioomba maeneo makubwa wakidai wanaendeleza miradi ya mifugo, viwanda wengine wameyatelekeza huku wakibadilisha matumizi wafuatiliwe tujue undani wake,” alisema.

Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani, alisema ana amini uendelezaji wa nyumba na makazi bora ya wananchi hauwezi kukamilika kwa kumtegemea mtu mmoja.

Kutokana na hali hiyo, amelitaka Shirika la Nyumba (NHC) kuja na mpango maalumu wa kuhakikisha wanawafanyia nini wananchi wenye hali za chini.

Kigwangalla atoa siku saba


Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, alitoa siku saba kwa wakuu wa mikoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha wanasimamia zoezi la uondoaji taka zilizokusanywa Desemba 9, mwaka huu.

Kigwangala ambaye ni Mbunge wa Nzega Vijijini, alisema baada ya kupita kwa muda huo, atafuatilia na iwapo atagundua kuwapo kwa mtendaji aliyezembea agizo hilo, atamjulisha Rais Magufuli ili achukuliwe hatua.

“Hatutakuwa na utani katika hili kwa sababu hatutaki kuwa na wagonjwa wapya wa kipindupindu, tutakuwa vimbelembele kushtaki kwa rais na tutapendekeza hatua za kuwachukulia. Katika hili mtusamehe kwa sababu hatutakuwa tayari kufukuzwa,” alisema.

Mwigulu atoa siku tano


Akiwa mkoani Pwani, Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwigulu Nchemba, alitoa siku tano kwa Kampuni ya Sparkle Way lMT ya jijini Dar es salam ambayo ni mnunuzi wa zao la korosho, kulipa Sh bilion 3.4 ili wakulima wapewe fedha zao.

Alimtaka mnunuzi huyo kuhakikisha anaingiza fedha hizo katika akaunti ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Pwani (CORECU), ifikapo Jumatatu ya wiki ijayo.

“Nakuagiza kuanzia kesho (leo), hakikisha unaanza kuingiza fedha hizi kwenye akaunti ya chama cha ushirika kufikia Jumatatu wakulima waanze kulipwa,” alisema.

Kitwanga atoa siku mbili


Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ametoa siku mbili kwa Jeshi la Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali zinazohusiana na uhalifu na usalama wa raia.

Kitwanga aliyasema hayo jijini Dar es salaam alipofanya ziara ya kutembelea kambi kuu ya polisi iliyopo barabara ya Kilwa maarufu kama Polisi Barracks pamoja na vituo vya polisi.

Miongoni mwa mambo ambayo waziri huyo alitaka apewe ufafanuzi ni suala zima la polisi kutokushiriki katika ulinzi wa Bandari na badala yake kuacha bandari ikilindwa na walinzi wa makampuni binafsi.

Pia alitaka ufafanuzi kuhusu kuendelea kushamiri kwa ugaidi unaoambatana na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya nchini, ambapo alitaka kupelekewa majibu ofisini kwake.

“Sote ni watu wazima, kama tulikosea kipindi cha nyuma hayo yameshapita lakini hatutavumiliana kama tutakosea huko tunapokwenda,” alisema Kitwanga.
  • via MTANZANIA

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA