Sekretarieti ya Ajira yataadharisha waombaji Ajira Kupitia mtandao Kujihadhari na Matapeli
Waombaji wa Ajira wajihadhari na Matapeli |
Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma inaendelea kutoa tahadhari kwa mara
nyingine tena kwa waombaji wote wa fursa za ajira Serikalini kupita
Sekretarieti ya Ajira kuepuka matapeli wanaowaomba fedha au rushwa ya
aina yeyote ile ili kuwasaidia kupata kazi au kuwapatia mafunzo kabla ya
kuanza kazi.
Tunalazimika kutoa tahadhari hii kwa kuwa tumepata taarifa ya malalamiko ya wadau wetu kutapeliwa ambapo yamekuwa yakiongezeka licha ya kuwatahadharisha mara kwa mara. Tunaendelea kuwafahamisha na kuwatahadharisha wateja wetu kuwa wasikubali kupokea simu zenye kuwaomba fedha au kutoa kitu chochote wakati wanapokuja kwenye usaili au baada ya usaili. Huo sio utaratibu wa Sekretarieti ya Ajira. Katibu wa Sekretarieti ya ajira anatoa tahadhari hii baada ya ofisi yake kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waombaji kazi waliofanya usaili hivi karibuni ambao wamedai kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kama Maafisa wa Sekretarieti ya Ajira na kuwadai kiasi cha fedha kama sharti ya kupangiwa vituo vya kazi. Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma haina utaratibu wa kuomba fedha au zawadi ya aina yeyote kwa wasailiwa kama sharti la kupangiwa kituo cha kazi. Ieleweke vizuri kuwa uendeshaji wa mchakato wa Ajira Serikalini unazingatia Sheria, kanuni na Taratibu, pia unatawaliwa na usawa na uwazi kwa kuzingatia sifa ya mwombaji na si vinginevyo. Mbali na hilo hatua za mchakato wa ajira zimekuwa zikifanyika kwa uwazi kuanzia hatua ya kutoa matangazo ya kazi, matangazo ya kuitwa kwenye usaili na matangazo ya wanaopangiwa vituo vya kazi. Tunaendelea kuwataadharisha waombaji kazi wote kuwa makini katika kujiunga na kutumia baadhi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa huko wamekuwa wakijaza taarifa nyingi za msingi na wengine wakiweka maisha yao wazi kiasi ambacho hata watu wenye dhamira ya ulaghai wameweza kutumia kuwapata kwa urahisi. Endapo baadhi ya wadau wetu wanapenda kutuma baadhi ya taarifa zao binafsi kwenye baadhi ya mitandao tunawashauri wawe waangalifu na kuhakikisha kuwa mitandao hiyo ni salama na haitawaletea madhara yoyote. Vilevile, tunatoa tahadhari kwa waombaji kazi wanaojaza taarifa zao kwenye mfumo wa ajira (Recruitment Portal) kwa kutumia kompyuta za ''Internet Café'' wakumbuke kufuta taarifa hizo wanapomaliza kazi zao ili kuepuka watumiaji wengine kupakua taarifa hizo. Pia unapotumia kompyuta za jamii si vyema kukubali ikumbuke anwani ya siri ''password'' ya barua pepe yako kwa kuwa mtu mwingine atakayeitumia anaweza kutumia taarifa zako kukuweka matatani. Ni imani yetu kwamba wakati Ofisi yetu ikiendelea na uchunguzi wa kuwabaini matapeli hao ili kuwachukulia hatua za kisheria, wadau wetu wataongeza umakini na kuchukua tahadhari binafsi na watu wa namna hiyo. Kwa kuwa ofisi yetu haina utaratibu wa kuomba wala kupokea chochote ili kumsaidia msailiwa kupata kazi zaidi ya kuangalia kama mwombaji wa kazi katimiza vigezo na amefaulu usaili husika. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma 04 Disemba, 2015. |
Comments
Post a Comment