Maagizo ya Waziri Prof. Muhongo alipozuru mabwawa ya Kihansi na Kidatu



Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza Meneja wa Kituo cha Kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji, Mhandisi Pakaya Mtamakaya (kushoto) akizungumzia kuhusu uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kihansi.

Maombi ya siku za nyuma uunganishaji Umeme na Luku ukomo Januari 15


Mameneja wa Kanda wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wametakiwa kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 15 Januari mwakani kazi ya kuwaunganishia umeme na LUKU waombaji wa muda mrefu iwe imekamilika.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwenye Kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi wakati alipokutana na Mameneja wote wa Kanda wa Shirika hilo.

Alionya kuwa Meneja yoyote atakaeshindwa kutimiza agizo hilo awe tayari kuacha ama kuachishwa kazi.

"Ikitokea Watanzania wakalalamika kucheleweshewa huduma kufikia tarehe 15 mwezi ujao, muwe tayari kuacha kazi," alisisitiza.

Profesa Muhongo alisema Watanzania wamechoshwa na utendaji duni wa Tanesco na kuagiza wahakikishe wanabadilika kwa kuwatumikia vyema wananchi.

Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi huku kubwa zaidi ikiwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara na kucheleweshewa huduma ya kuunganishiwa umeme na Luku.

Alisema kwa sasa anazungukia mitambo yote ya uzalishaji umeme nchini kufanya tathmini ili kuelewa hali halisi ya umeme na kuwataka kukomesha mara moja hali ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi.

Vilevile Profesa Muhongo aliwaeleza Mameneja hao kuwa ifikapo siku ya Jumamosi ya tarehe 19 mwezi huu wawe na majibu ya kero mbalimbali za umeme nchini.

Alisema siku hiyo atakutana na Mameneja hao pamoja na watendaji wa taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya nishati nchini.

"Nimewaeleza hawa Mameneja kuwa siku ya jumamosi nitakuwa na kikao nao pamoja na watendaji wengine. Nataka waje na majibu ya kisayansi," alisema Profesa Muhongo.

Jambo jingine ambalo Waziri huyo anataka kutoka kwa Mameneja hao ni mkakati waliouandaa kuhakikisha bei ya umeme nchini inashuka.

"Watanzania wanauliza vipi tutafaidika na gesi yetu? Nataka mje na mkakati wa kupunguza bei ya umeme," alisema Muhongo.

Aidha, alizungumzia suala la kuongeza makusanyo ya mapato ya huduma ya umeme ambapo aliwaagiza Mameneja hao kuongeza mara mbili ya malengo ya ukusanyaji mapato waliyokuwa wamewekewa hapo awali.

Waziri Muhongo tayari amekwishatembelea vituo vya kuzalisha umeme vya Hale, Pangani, Nyumba ya Mungu, Mtera na Kihansi.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kushoto) akikagua Kituo cha Kuzalisha umeme cha Kihansi. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba. Waziri Muhongo alifanya ziara kituoni hapo kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa umeme kituoni hapo.
Meneja wa Kituo cha Kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji cha Kihansi, Mhandisi Pakaya Mtamakaya (kulia) akimuelezea kwa mchoro muundo wa bwawa la Kihansi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) wakati alipofanya ziara kwenye bwawa hilo ili kujionea hali ya maji. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mtambo mmojawapo wa kuzalisha umeme wa kituo cha Kihansi ambao uwezo wake ni kuzalisha Megawati 60. Kituo hicho cha Kihansi kina jumla ya mitambo mitatu ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji ambapo kila mtambo inao uwezo wa kuzalisha kiasi cha Megawati 60 lakini kutokana na tatizo la maji mitambo hiyo inashindwa kuzalisha kiasi hicho.

Muhongo Aagiza kufungwa matoleo ya umwagiliaji


Serikali imeagiza matoleo ya maji ya kumwagilia mashamba yanayotumia maji ya mito inayotiririsha kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ya Mtera na Kidatu yafungwe.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipotembelea Bwawa la Kidatu na kujionea namna ambavyo kina cha maji kwenye bwawa hilo kilivyopungua.

Waziri Muhongo alisema tatizo kubwa la uzalishaji mdogo wa umeme wa maji nchini ni umwagiliaji usio zingatia taratibu za matumizi sahihi ya maji.

Alisema mfumo wa umwagiliaji unaotumika ni wa kienyeji sio wa kitaalamu. "Nimeshuhudia mtu anazuia maji kutiririka kwa kutumia mawe, magogo ama viroba vya mchanga; hii sio sahihi," alisema.

Akizungumzia umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji, Waziri Muhongo alisema kwa hivi sasa ni asilimia ishirini tu inayozalishwa kutoka kwenye vyanzo vya maji nchini.

Alisema jumla ya uwezo wa mitambo yote ya maji (installed capacity) ni Megawati 561.84 ambapo wastani wa uzalishaji kwa sasa kutoka kwenye mitambo hiyo ni Megawati 110 hiyo ni kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 mwezi huu.

"Nimetembelea Nyumba ya Mungu, Hale, Pangani, Mtera, Kihansi na Kidatu na kugundua kwamba tatizo sugu ni umwagiliaji na siyo tabianchi," alisema.

Alisema mashamba ya umwagiliaji yanaongezeka Mikoani Mbeya, Iringa na Morogoro.

Aliongeza kuwa vibali vya umwagiliaji vimetolewa kienyeji bila kutafakari athari itakayotokea.

Profesa Muhongo alisema kipindi hiki ni cha mvua hivyo wenye mashamba ya umwagiliaji watumie maji ya mvua badala ya kuendelea kutumia mito.

Alisema wakati mazungumzo yanaendelea, Bodi ya Maji- Bonde la Rufiji wahakikishe wanakagua mifereji yote ya umwagiliaji inayoingiza maji kwenye Mto wa Ruaha mkuu na kuifunga ili kuruhusu bwawa la Mtera kupata maji.

Alieleza kwamba kwa kufunga mifereji hiyo ndani ya siku nne hadi tano maji yatakua yameingia kwenye bwawa la Mtera na hivyo kuweza kuendesha mitambo.

Awali akimueleza Waziri hali halisi ya uzalishaji umeme kwenye kituo hicho cha Kidatu, Meneja wa Kituo, Mhandisi Justus Mtolera alisema umeme unaozalishwa kituoni hapo kwa sasa ni megawati 50 wakati kituo hicho kinao uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 204.

Mhandisi Justus alisema kituo hicho kinayo mitambo minne ya kuzalisha umeme lakini kutokana na tatizo la maji, mitambo miwili tu inafanya kazi ambapo kila mmoja unazalisha kiasi cha Megawati 25.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza jambo wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu. Katikati ni Meneja wa Kituo hicho cha Kidatu, Mhandisi Justus Mtolera na anayemfuatia ni Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera, Mhandisi Abdallah Ikwasa.

Bwawa la maji la kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme la Kidatu likionekana katika hali ya kupungukiwa na maji

Comments

Popular posts from this blog

PATA UKWELI KUHUSU MWANAMALUNDI, MTU WA MAAJABU ALIYEWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA YA KABILA LA KISUKUMA